Home » » Magufuli afuta safari zote nje

Magufuli afuta safari zote nje

Written By CCMdijitali on Sunday, November 8, 2015 | November 08, 2015

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.

 Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika picha ya pamoja Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.
PICHA NA IKULU

WATENDAJI wote wa Serikali, wamepigwa marufuku kufanya safari za nje ya nchi na badala yake majukumu yanayowapeleka katika nchi hizo, wametakiwa wayakabidhi kwa mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi husika.

Rais John Magufuli ametoa agizo hilo jana katika siku yake ya tatu Ikulu, alipokutana na makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade.

“Nataka Serikali iendelee kwa nguvu zote na katika kutekeleza dhana ya ‘Hapa Kazi Tu’ na viongozi wazingatie na kukumbuka ahadi nilizotoa, ili zianze kuonekana na kufanyiwa kazi mara moja,” amesema Rais Magufuli katika taarifa iliyotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Katika kusisitiza katazo hilo la ziara za nje ya nchi, Rais Magufuli amesema pakitokea jambo la dharura sana, pamoja na udharura wake kabla ya mtendaji yeyote kwenda nje ya nchi, atalazimika kupata kibali kutoka kwa Rais au Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

*Vijijini, shule bure

Badala ya kufanya ziara katika nchi ambako Tanzania ina mabalozi, Rais amewataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi wa Tanzania.

Katika hilo, amesisitiza kwamba kuanzia Januari mwaka 2016, wanafunzi wote wanaoanza shule watasoma bure bila kulipa ada, ambapo Rais amewataka watendaji kuliwekea mikakati agizo hilo tayari kwa utekelezaji.

Agizo hilo ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi zilizoisha Oktoba 24 mwaka huu, kwamba kuanzia mwakani wanafunzi wote wanaosoma shule za Serikali kuanzia darasa la awali mpaka kidato cha nne, watasoma bure.

Kuhusu elimu ya juu, Rais Magufuli katika kikao hicho, ameagiza suala la mikopo ya wanafunzi lifanyiwe kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi. Rais ameelekeza watendaji hao wasimamie maagizo hayo, yawekewe mikakati na kuyapanga vizuri, ili atakapoteua Baraza la Mawaziri, watakaoteuliwa wakayasimamie bila kukosa.

*Mapato

Kuhusu ukusanyaji mapato, Rais Magufuli alitoa maagizo mahususi, alipomtaka Kamishna wa TRA, Bade kusimamia kwa makini ukusanyaji wa mapato nchini na kuhakikisha kero ndogo ndogo kwa wananchi, zinaanza kutatuliwa kama alivyoahidi.

Rais ameitaka TRA kukusanya mapato hayo kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa zaidi na wale wanaokwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote hapa Tanzania.

Katika kuweka msisitizo, Rais Magufuli alisema katika Serikali hii wa kutoa uamuzi vinginevyo zaidi ya huo, ni yeye Rais ama Makamu wake, Samia Suluhu Hassan.

*Ahadi zingine

Ahadi zingine zilizotolewa na Rais Magufuli wakati wa kampeni zake ambazo ametaka watendaji hao kuzizingatia ni pamoja na kushusha bei ya vifaa vya ujenzi hasa saruji, mabati na misumari, ili wananchi waweze kujenga nyumba bora.

Katika kuongeza idadi ya Watanzania wanaofanya kazi, alisema katika kila mtaa na kijiji, Serikali yake itatoa Sh milioni 50 kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara ndogo za wanawake na vijana.

Alisema atataka kila anayefanya kazi apate kipato kizuri kitakachomsaidia kukabiliana na mahitaji ya maisha yake, ikiwemo kujenga nyumba bora kutokana na kushushwa kwa bei za bidhaa za ujenzi.

Mbali na kutoa mikopo hiyo izunguke katika ngazi ya kijiji na mtaa, Dk Magufuli pia aliahidi kwamba Serikali yake itazuia kila aina ya usumbufu unaofanywa kwa wafanyabiashara hao, ikiwemo kukamatwa kwa bodaboda na mama ntilie.

Kwa wakulima, alisema atahakikisha pembejeo sahihi zinatolewa kwa wakati na mazao yatakayovunwa, itakuwa marufuku kwa Serikali kukopa mazao yao. Aidha aliahidi kuondoa ushuru unaosumbua wafanyabiashara wadogo na hasa wakulima, ili wafanye biashara kwa uhuru wajipatie kipato halali.

Rais Magufuli pia alisema baada ya kusambaza umeme, atahakikisha viwanda vidogo na vya kati vinajengwa vijijini kusindika mazao ya kilimo, ili kutoka shambani bidhaa za viwandani zikauzwe kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, Rais Magufuli alisema atatoa ardhi zaidi kwa ajili ya wakulima na wafugaji, ili kuondoa uhaba wa ardhi uliosababisha ugomvi wa maeneo ya kulishia mifugo na kulima.

Lakini pia aliahidi kunyang’anya mashamba ambayo yamehodhiwa na watu bila kutumiwa kwa ufugaji wala kilimo, na kuyagawa kwa wakulima na wafugaji wasio na maeneo ya kilimo wala eneo la kufugia.

Katika sekta ya afya, mbali na kuahidi kuendelea kujenga zahanati kwa kila kijiji na mtaa, kituo cha afya kwa kila kata na hospitali ya rufaa katika kila mkoa, aliahidi kukomesha kero ya kukosekana dawa katika hospitali za Serikali.

Katika kero ya maji, alisema kama amefanikiwa kujenga zaidi ya kilometa 17,000 za barabara, hatashindwa kuchimba mabwawa na kujenga mtandao wa mabomba kwenda kwa wananchi.

Maagizo hayo ya Rais Magufuli yamekuja siku ya tatu tu ya kuingia Ikulu, ambapo siku ya kwanza Alhamisi iliyopita, alianza kwa kumteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na siku ya pili, juzi alimuapisha na kufanya ziara ya ghafla katika ofisi za Wizara ya Fedha, Hazina, akakagua ofisi za watumishi wa ngazi za chini.

Baada ya kukagua ofisi hizo, ambako alikuta baadhi ya watendaji wamefika ofisini na kuondoka, alifanya mazungumzo na watendaji wakuu wa wizara hiyo na kusisitiza umuhimu wa kukusanya kodi.

Na Habari Leo.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link