Home » » Muhongo: Fanyeni utafiti wa kutosha

Muhongo: Fanyeni utafiti wa kutosha

Written By CCMdijitali on Tuesday, February 16, 2016 | February 16, 2016

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo


WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wawekezaji katika sekta za nishati na madini kufanya utafiti wa kutosha katika maeneo husika kabla ya kuendelea na miradi yao.

Profesa Muhongo aliyasema hayo katika mkutano baina yake na wawakilishi kutoka Kampuni ya Lake Holdings ukiwa ni moja kati ya mikutano kadhaa inayoendelea wiki nzima baina ya Wizara na wawekezaji wa sekta hizo.

Kampuni hiyo iliyosajiliwa mwaka 2012 ina mpango ya kujenga kituo cha kuzalisha umeme chenye uwezo wa megawati 300 hadi megawati 450 wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Huo ni mradi mkubwa zaidi ukilinganishwa na mradi wao wa awali katika Kata ya Kiwira wilayani Rungwe, Mbeya uliolenga megawati 200 za umeme.

Akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa mradi huo, Profesa Runyoro alieleza kuwa changamoto kuu waliyoipata katika kutekeleza mradi huo ni upatikanaji wa makaa ya mawe ambayo yanahitajika kwa kiasi kikubwa (tani milioni moja) ili kuwezesha mradi huo, huku maeneo mengi yameshachimbwa na watu wengine.

Akizungumzia suala hilo, Profesa Muhongo aliwataka wawekezaji waache ubahili na badala yake waende wenyewe katika maeneo hayo ili kujua kiasi cha makaa ya mawe yanayopatikana kwani mradi huo ni mkubwa na utahitaji uwekezaji mkubwa, hivyo kuwataka kufanya upimaji wa kijiografia na kisha kutoa majibu baada ya mwezi.

Aidha, alilitaka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufanya kazi kwa karibu na Lake Holdings ili waafikiane juu ya suala hilo na wawekezaji hao wapate maeneo ya kuchimbia makaa ya mawe.

Aliwataka wawekezaji kutochukua maeneo na kuyaacha na hivyo kupoteza muda wa Watanzania, badala yake wayafanyie kazi ili Watanzania wanufaike na rasilimali hiyo.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link