Home » » Ukeketaji ni janga la kitaifa -Waziri Ummy

Ukeketaji ni janga la kitaifa -Waziri Ummy

Written By CCMdijitali on Monday, February 8, 2016 | February 08, 2016


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiongea na wanahabari.

 Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma

SERIKALI imetangaza kuwa ukeketaji wa watoto na wanawake ni janga la kitaifa, hivyo jitihada zinahitajika kuhakikisha unakomeshwa. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitangaza hivyo juzi mjini hapa wakati akizungumza kwenye siku ya kupinga ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wanawake.

Ilielezwa kuwa, katika mikoa ya Manyara katika kila watoto 100, watoto 71 wamekeketwa, Dodoma kwa kila watoto 100, watoto 64 wamekeketwa, Arusha kwa kila watoto 100, watoto 59 wamekeketwa, mkoani Singida kila watoto 100, watoto 51 wamekeketwa na mkoani Mara kwa kila watoto 100, watoto 40 wamekeketwa.

Waziri Mwalimu alisema kuwa hilo ni janga la kitaifa na ni lazima kupambana nalo. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 15 ya wanawake nchini wamekeketwa. Kwa maelezo ya Mwalimu, ukubwa wa tatizo la ukeketaji katika mikoa hiyo linatokana na imani potofu ambayo kwa sasa imeanza kujitokeza katika mikoa mingine kama Dar es Salaam, Morogoro na Pwani kutokana na watu wa makabila mbalimbali kuhamia mikoani humo.

“Serikali inapinga, inalaani na kukemea tabia ya kuendelezwa kwa vitendo hivi vya ukatili unaodhalilisha mtoto wa kike na mwanamke. Ukeketaji unamsababishia madhara makubwa mtoto wa kike na mwanamke kiafya, kielimu, kisaikolojia na kimaendeleo. Ndani ya Serikali ya Rais John Magufuli tutamaliza vitendo vya ukeketaji,” alieleza.

Alitoa rai kwa jamii kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili mangariba na wakala wao wajulikane na kuchukuliwa hatua. Aliongeza kuwa, Serikali itaendelea kutekeleza programu mbalimbali za hamasa na elimu kwa jamii zinazojikita katika kubadili fikra na mitazamo ya wananchi dhidi ya ukeketaji.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link