Home » » Naona akili za Msigwa ndizo zimedumaa huku Sabrina, Matiko wakiwa janga kubwa bungeni

Naona akili za Msigwa ndizo zimedumaa huku Sabrina, Matiko wakiwa janga kubwa bungeni

Written By CCMdijitali on Tuesday, May 24, 2016 | May 24, 2016


Na Charles Charles

MEI 12, mwaka huu, Mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Peter Msigwa aliliambia bunge linaloendelea mjini Dodoma kuwa mawaziri wa serikali ya sasa wana udumavu wa akili!

Msigwa aliyekuwa akichangia hoja wakati bunge lilipokaa kama Kamati ya Matumizi ili kupitisha bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka 2016/2017, alidai Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano wanashindwa hata kufikiri na hawana uwezo wa kubuni kitu chochote katika utendaji wa kazi zao.

“Unakuta mawaziri wanashangaa eti bandarini kuna makontena 70 ya sukari, yaani kwa fikra zao wanaona ni mengi wakati mtu kama (Saidi) Bakhresa kuwa na tani hadi 100,000 kwenye ghala ni kitu cha kawaida, lakini hayo ndiyo madhara ya udumavu (wa akili)”, alisema, kauli iliyomuudhi Waziri wa Wizara hiyo, Ummy Mwalimu na kumtaka ataje aliokuwa akiwalenga au adhibitishe tuhuma zake, jambo ambalo kwa hakika mbunge huyo alishindwa kulifanya.

Siku sita baadaye ilipofika Jumatano iliyopita, wabunge wawili wa Chadema, Esther Matiko wa Tarime Mjini na Sabrina Sungura wa Viti Maalum walitaka kumshushia kipigo Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jacquiline Ngonyani anayetokea mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza katika bunge hilo pia, Jacquiline alisema kambi hiyo ya upinzani katika chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi una wabunge wawili tu wenye michango ya maana, wale aliokuja kuwataja kwamba ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza na Mbunge wa Kaliua katika mkoa wa Tabora kutoka chama cha Civic United Front (CUF), Magdalena Sakaya.

Akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Jacquiline alisema kuna “mlevi” aliyeishambulia serikali kuhusiana na uuzwaji wa nyumba za umma wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu, kisha akasema kuwa mhusika mkubwa katika jambo hilo alikuwa Waziri Mkuu aliyekuwepo madarakani wakati huo, Frederick Sumaye.

Akizidi kubainisha, mbunge huyo alisema kwamba duniani kote hakuna mwanamke anayeweza kumsifu mke mwenza, hivyo upinzani kamwe hauwezi kuisifia CCM au
serikali yake kuwa inafanya kazi kubwa na nzuri.

Hata hivyo, mchango wake huo uliamsha hasira za Sabrina na Esther Matiko ambao baada ya kikao cha siku hiyo kuahirishwa, wote kwa pamoja walimfuatilia nje ya ukumbi ili kumchapa makonde, lakini bahati nzuri alipotoka tu aliondoka moja kwa moja katika viwanja hivyo vya bunge.

Alipoulizwa baadaye na mwandishi wa gazeti moja litolewalo kila siku nchini, Sabrina alisema kama Jacquiline angesimama alipotoka ukumbini “wangemshughulikia”.

Kwanza ninakiri kuwa sipendi uchangiaji wa vijembe, kejeli au mashambulizi yoyote dhidi ya mbunge, bunge lenyewe, serikali wala chama cha siasa na kadhalika, na pia sifurahishwi na dharau inayofanywa mara kwa mara na baadhi ya wabunge wanaopata nafasi ya kuchangia chochote katika chombo hicho.

Kana kwamba haitoshi, sipendi pia kuona wabunge wakichangia mambo yasiyokuwa na tija kwa taifa hata kama hawatoi vijembe kwa yeyote, halafu sifurahishwi na wale wanaotaka kuligeuza bunge hilo kuwa kama jukwaa la maigizo ili kutafuta umaarufu wa kijinga.

Mathalani, mchango wa mbunge aliyetaka sanamu ya askari iliyopo katika Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam iondolewe na kuwekwa ya mwimbaji wa muziki wa kizazi kipya au bongo fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond’ kwa hakika “ni utumbo” mtupu!

Sikufarahishwa hata kidogo na mchango wa Msigwa aliposema Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano hawawezi kufikiri kwa vile wana udumavu wa akili, kauli ambayo ililenga kuwadhalilisha kutokana na chuki zake za kisiasa dhidi yao.

Ilikuwa kauli itokanayo na upeo mfupi wa kufikiri na kama ni udumavu wa akili basi inawezekana zake ‘zimeoza’, hivyo inakuwa kazi ngumu kabisa kwake kuyapima au kuyatathmini maneno yake kabla ya kuanza kuyazungumza mbele ya halaiki ukumbini, barabarani na hata vinginevyo.

Nasema kwamba ni ujinga wa kufikiri kwa mbunge kusimama hadharani ili kuunadi umbumbumbu alionao kichwani, lakini inatisha zaidi kama anakuwa waziri kivuli kwa sababu ameaminiwa kwa namna moja ama nyingine, hivyo anapokuwa mropokaji na muongo anathibitisha kuwa hatoshi hata kupewa tu ukiranja wa shule ya chekechea.

Katika hali hiyo ama ya chuki, Msigwa alipaswa atafute lugha inayoweza kuwa ya staha hata kama tuhuma zake alidhani kuwa za kweli, jambo ambalo hata hivyo ni
uzushi na ndiyo maana alipoombwa athibitishe madai hayo alishindwa.

“Hivi Msigwa ukiambiwa ulete huo uthibitisho wa waziri mwenyewe udumavu wa akili utauleta?” Aliulizwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu lakini hakusema “ndiyo” kwa sababu hakuwa nao, na pia alishindwa kusema “hapana” kwa vile aliogopa kuaibika.

Msigwa aliyeshika nafasi hiyo kwa mara yake ya kwanza mwaka 2010 kwa kubebwa na mzozo wa kisiasa wa ndani ya CCM, kisha akachaguliwa kwa hujuma na usaliti uliofanywa na baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hichohicho katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015 anajua bunge hilo la 11 litakuwa la mwisho kwake kuwa mbunge tena.

Pamoja na kudai ni mchungaji kanisani, mbunge huyo kwa hakika amethibitisha kwa kauli kwamba anaweza akazungumza chochote wakati wowote na mahali popote, hivyo wananchi wa jimbo lake inabidi wafahamu kwamba hawana mwakilishi makini katika chombo hicho cha kutunga sheria.

Mbunge huyo kwa namna zote amekuwa ni mpotoshaji na mzushi, yule ambaye kwake kumtungia uongo mtu yeyote ili kumvunjia heshima yake popote umekuwa ni kama utamaduni wa kwake.

Ingawa sina hakika sana, lakini inawezekana anafanya hivyo kwa vile anajua kwamba hatarudi tena bungeni mwaka 2020 iwe katika jimbo hilo la sasa, na pia anaelewa kuwa haiwezekani kwake kwenda kushinda kiti cha ubunge wa Isimani, jimbo ambalo sasa linaongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Tokea awe mbunge karibu miaka sita iliyopita, Msigwa amejitokeza kuwa mahiri wa uongo, uzushi na kiongozi mwenye maneno machafu kinywani huku akijifanya eti ni mchungaji, hivyo sikushangazwa sana na madai aliyotoa dhidi ya mawaziri wa serikali ya sasa na huenda upeo wake wa kisiasa ni mdogo sana.

Wananchi wa jimbo lake ukiondoa vichwamaji na wapambe wake wachache ambao kuna wengine nawajua kwa majina, sura zao na kadhalika wanafahamu kwamba watahangaika kwa miaka mitano , lakini wasiporekebisha makosa yao mwaka 2020 itakuwa moja kwa moja “imekula kwao” tena.

Ndiyo maana pale alipofanya vurugu kwenye mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera, Februari mwaka huu na kuomba apelekwe mahabusu akidhani angepata umaarufu watu wengi walishangazwa na kitendo chake hicho, kisha wengi wakahoji kuhusu uwezo wake wa kufikiri.

Ndiyo maana pia madai yake haya ya sasa ninaweza kuyafananisha kwa namna moja ama nyingine na ajabu mpya ya dunia. Amebaki kubwabwaja au kuropoka lolote na mahali popote, mtu ambaye anaweza akazungumza chochote ili kukidhi matakwa yake yenye chuki za chiki.

Mbali na Mbunge Peter Msigwa, hatua ya Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko pamoja na Mbunge wa Viti Maalum, Sabrina Sungura ambao pia ni kutoka Chadema ya kutaka kumshushia kipigo Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Jacquiline Ngonyani, Jumatano iliyopita pia nayo ni ujinga wa kufikiri!

Ni ujinga kwa sababu kama wangekuwa wanachukia dharau, kebehi, uzushi na uongo wangekerwa na kauli ya Msigwa alipodai siku sita kabla ya hapo kuwa mawaziri wana udumavu wa akili, madai ambayo kwa hakika yanatia ‘kichefuchefu’ zaidi kuyasikia masikioni na hata vinginevyo.

Walipaswa wathibitishe kukerwa kwao na uzushi, uongo na upotoshaji wake huo hasa kwa vile anajidai ni Mtumishi wa Mungu aliye hai, lakini hawakusema wala kufanya chochote dhidi yake hadi jana, Jumatatu Mei 23 nilipokuwa ninaandika makala yangu hii.

Kauli ya Msigwa inaweza ikafanana kwa namna moja ama nyingine na ile iliyowahi kutolewa na aliyekuwa Mbunge wa Ubungo jijini Dar es Salaam (Chadema), John Mnyika ambaye hivi sasa ni Mbunge wa Kibamba aliyedai katika bunge lililopita kwamba aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alikuwa ni “dhaifu sana”.

Pamoja na kutakiwa afute kauli yake ama athibitishe tuhuma zake, Mnyika alisema alikuwa radhi na tayari kuuwasilisha popote ushahidi wake, lakini alipopewa muda wa kufanya hivyo kwa Katibu wa Bunge alishindwa na kuadhibiwa kwa uongo na uzushi bungeni.

Nafahamu kuwa Sabrina, Matiko na wabunge wote wa Chadema wanajua kwamba alichofanya Msigwa siku hiyo ni kusema uongo, uzushi na alilenga kuwavunjia heshima mawaziri kwa sababu za kisiasa, hivyo isingewezekana kwao kumpinga na kuhatarisha maslahi ya chama chao kwa vile wote hawana chembe yoyote ya uzalendo kwa nchi yao.

Badala ya kuukemea uzushi wa Msigwa ambao ni hatari zaidi, Sabrina na Matiko kwa
pamoja walishindwa na kuleta unafiki mkubwa wa kutaka kumshushia kipigo Mbunge Jacquiline Ngonyani, tena kwa sababu eti alisema kambi hiyo ya upinzani inao wabunge wawili tu wenye michango ya maana wanapozungumza bungeni!

Badala ya kujibu tuhuma zake kwa hoja ili kumuumbua endapo siyo kweli, wabunge hao wanawake wa Chadema walijifanya kuwa vibaka kwa kutangulia nje ya ukumbi ili kwenda kumvizia, kisha wamshushie kipigo kwa sababu hiyo tu!

Katika hali zote na hata vinginevyo, mimi sioni tatizo lililopo katika mchango huo wa Jacquiline, hivyo kwa hakika ni ujinga wa kufikiri kupanga kumpiga katika hali yoyote.

Kama Sabrina na Matiko wangeshindwa kujibu alicholiambia bunge hilo wangekuwa na busara zaidi kukiomba mwongozo kiti cha spika ili athibitishe tuhuma zake, halafu akishindwa angetakiwa afute kauli yake na kuonekana muongo na mzushi.

Lakini waliposhindwa kutumia njia zote hizo zinazotambuliwa na kanuni za kudumu za bunge na kutaka wamuonyeshe ubabe wa masumbwi nje ya ukumbi, wale wenye busara iwe bungeni na mahali pengine waliwaona wabunge hao kuwa upeo wao wa kisiasa na kibunge ni mdogo sana.

Mbali na sababu nyingine, mimi ninaamini pia kuwa Sabrina, Matiko na wabunge wote wa Chadema walishindwa kuipangua hoja nzito ya Jacqiline aliposema mhusika mkuu wa sakata la uuzwaji wa nyumba za serikali wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu, kwa namna yoyote alikuwa Waziri Mkuu wa kipindi hicho, Frederick Sumaye.

Walishindwa kuipangua kwa vile Ibara ya 52(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inasema kwamba “Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli (zote) za Serikali ya Jamhuri ya Muungano” (mwisho wa kunukuu).

Katika hali hiyo na hata vinginevyo, kwangu mimi ninaona kuwa akili za Msigwa ndizo zimedumaa huku Sabrina na Matiko wakiwa janga kubwa na hatari bungeni.

Mungu Ibariki Tanzania!

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Itikadi na Uenezi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. 

Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link