Na Charles Charles
WIKI iliyopita, kambi ya upinzani bungeni ilitangaza, kisha ikaanza kususia vikao vyote vya chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi ambavyo vinaongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson ikidai kuwa haina imani naye.
Katika msimamo wao, wabunge hao ambao wanaungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba walitoa sababu sita za kufanya hivyo.
“Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ameweka mbele maslahi ya chama chake cha siasa (akimaanisha Chama Cha Mapinduzi au CCM) kuliko ya bunge kinyume cha Kanuni ya 8(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge”, alisema Mbunge wa Simanjiro mkoani Manyara kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), James ole Millya.
Alisema kanuni hiyo inakataza upendeleo na kutaja pia Kanuni ya 5(1) akisema inamtaka spika kuzingatia mila, desturi na uamuzi wa maspika wa mabunge mengine duniani, lakini akashindwa kutolea mfano angalau mmoja tu.
Wakati Millya akija na madai hayo mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma, kwa niaba ya wapinzani wenzake na akiwa amefuatana pamoja na Mbunge wa Viti Maalum kutoka chama cha Civic United Front (CUF), Riziki Shaali Mngwali, bunge katika upande wake kama taasisi nalo lilizungumza vinginevyo.
Katika kufanya hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah alisema msimamo wa wabunge hao wa upinzani kamwe hauwezi kuathiri shughuli za chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi, kisha akaongeza kuwa uongozi wake haujaona tatizo la kumnyoshea kidole Dk. Tulia.
Akitoa ufafanuzi, Dk. Kashililah alisema kama wabunge hao wanapinga uamuzi wa Naibu Spika wa kuzuia mjadala wa sakata la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), walipaswa kutumia Kanuni ya 5(4) – (6) kwa kumwandikia barua Katibu wa Bunge hilo ambaye angeiwasilisha kwa Spika, jambo waliloshindwa kulifanya.
“Bunge linaongozwa kwa kanuni na huu ndio utaratibu. Mimi kama kama katibu wa bunge hadi sasa (akimaanisha wakati huo bado) sijapata malalamiko kutoka kwa mbunge yeyote chini ya kanuni hii. Kwa hiyo wanachofanya wanajua wenyewe, lakini utaratibu uko wazi”, alisema.
Akimgeukia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro (Chadema), Dk. Kashililah alimshangaa kwa kuwadanganya Watanzania alipodai kwamba naibu spika alikwenda kinyume cha maelekezo ya Kamati ya Uongozi kuhusu suala hilo la UDOM.
“Kwanza (hata) kwenye kikao (huyo Mbowe) hakuwepo, aliwakilishwa na Mbunge wa Vunjo (kupitia chama cha NCCR – Mageuzi, James) Mbatia na kulikuwa na hoja mbili.
“Moja ni kuangalia uwezekano wa suala la wanafunzi (hao) kupelekwa katika Kamati ya Maendeleo na Huduma za Jamii.
Pili, Waziri (wa Wizara inayohusika) akatoe taarifa ya kina (bungeni) maana ile ya kwanza ilionekana kutojitosheleza”, alisema katibu huyo wa bunge.
Kwanza ninaomba niseme kuwa msimamo huo imara na madhubuti kwa maneno, vitendo na hata vinginevyo wa naibu huyo wa spika hata miye ninauunga mkono.
Nafahamu pia kuwa idadi kubwa ya Watanzania nao wanauunga mkono, na tatu hata baadhi ya wanachama, viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani ambavyo ni pamoja na Chadema yenyewe, CUF na NCCR – Mageuzi wasiokuwa wanafiki mioyoni mwao nao wapo upande wake.
Kama taifa na bila ya kujali itikadi za kisiasa kamwe hatuwezi, kwa namna yoyote ile kukubaliana na na kikundi kidogo tu cha wabunge, wafanyabiashara au wanasiasa wenye nia mbaya na nchi yetu hata kama babu zetu, bibi zetu, baba zetu, mama zetu, wajomba zetu, shangazi zetu, kaka zetu, dada zetu, binamu zetu ama rafiki zetu wa karibu.
Tangu mwaka 2005 baada ya kuingia kwa bunge la tisa hadi wakati wa bunge la 10 lililomaliza muda wake mwaka jana, wabunge wa upinzani walikigeuza chombo hicho kuwa kama jukwaa lao la kuchezea muziki wa dansi, hivyo ingawa sitaki kumnyoshea kidole mtu yeyote ninalazimika kusema kuwa miaka 10 ya mabunge hayo ndiyo iliwaharibu kwa kiwango kikubwa.
Walikuwa wakisema chochote bungeni, kuropoka chochote, kuchochea chochote, kupotosha chochote au kufanya vurugu za kupanga nje na ndani ya bunge, lakini waliachwa ama kuombwa wafute kauli zao pale wanaposema uongo huku wengine wakigoma kufanya hivyo ili kutafuta umaarufu usiokuwa na tija yoyote kwa taifa.
Wachache waliokubali kufuta kauli zao walifanya hivyo kwa nyodo zote midomoni au vinywani mwao, halafu kuna wengine walitekeleza agizo hilo kwa kuhitimisha na kusema “messege sent”.
Hata hivyo, wapo waliogoma moja kwa moja kufuta kauli za kusema uongo bungeni, uzushi na hata upotoshaji wa kichochezi huku wakidai kuwa wana ushahidi wa kauli hizo na kuahidi kuukabidhi kwenye kiti cha spika, lakini walipopewa muda wa kufanya hivyo walishindwa.
Ndivyo ilivyokuwa kwa mfano kwa aliyekuwa Mbunge wa Ubungo jijini Dar es
Salaam (Chadema), John Mnyika ambaye sasa ni Mbunge wa Kibamba aliyetoa kauli ya kuudhi, uongo na udhalilishaji dhidi ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete katika bunge lililopita.
Mazoea hayo ndiyo yaliwajengea kiburi cha misimamo, maneno na matendo hayo ya ovyo na ndiyo maana leo wamechanganyikiwa alipokuja naibu spika mpya, Dk. Tulia Ackson anayesimama kuzilinda kikamilifu Kanuni za Kudumu za Bunge.
“Kama naibu spika atakuwepo kwenye kiti kile (cha spika) hatatuona bungeni iwe leo, kesho au hata bunge lote. Tupo tayari kuchukua gharama hiyo (ya kususia vikao vyote vya bunge anavyoviongoza)”, alisema Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Huo ndio upuuzi na ujinga unapofanywa na wabunge hao nje na ndani ya bunge la nchi yetu. Nasema “ni ujinga” kwa sababu wanachofanya hakina tija yoyote kwao wala vyama vyao, majimbo yao, makundi yao au taifa lao Tanzania.
Ni ujinga na ndiyo maana sikutarajia kuona watu wazima na viongozi waandamizi wa umma kama wao, tena kwa sababu za kipuuzi wanafanya mambo hayo utadhani wanasesere au ni watoto wa chekechea.
Kitendo cha kususia kuhudhuria vikao vya bunge ambavyo vinaongozwa na mtu fulani awe ni spika mwenyewe, naibu spika au mwenyekiti wa bunge ni udhaifu wa kisiasa uliopitiliza.
Wabunge waliochaguliwa kwa kura kwenye majimbo yao kama akina Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini), Peter Msigwa (Iringa Mjini), James Mbatia (Vunjo), James ole Millya (Simanjiro) au David Silinde wa Momba na wengineo wanaotoka nje ya vikao vya bunge ambavyo vinaongozwa na naibu spika ni kama mazuzu yasiyojua lolote wala chochote.
Hiyo ni kwa sababu wanawakomoa wapiga kura kwenye majimbo yao, na pia wanaonyesha kwa wanachama, viongozi na wafuasi wa vyama vyao kwamba walipoteza muda wao bure kwa kuwanadi watu wenye ufahamu mdogo wa masuala ya uongozi wa kisiasa.
Ndiyo maana wanasusia vikao vyote hivyo wakidhani, tena kwa uhakika vichwani mwao kuwa wanamkomoa Dk. Tulia Ackson huku ukweli ukiwa vinginevyo.
Fikiria kwa mfano kama itakuwa ni busara kwao wenyewe kususiwa na wake zao nyumbani, waume zao ama rafiki zao wengine eti kwa sababu tu eti wamewapa maelekezo ya msingi ya kufuata au ya kutii sheria yoyote, kanuni ama utaratibu unaopaswa kufuatwa iwe nyumbani, kazini na mahali pengine popote.
Hata hivyo, hatua ya kususia kwao na kukimbia vikao hivyo hakuwezi kutafsiriwa vinginevyo ila udhaifu wa kufikiri, uelewa mdogo wa masuala ya uongozi ama kwa Kiswahili cha kisasa ni kama ‘umbulula, unyumbu’ au wana akili za kupandikiziwa na watu wengine.
Ndiyo maana ‘wanaendeshwa’ kama gari bovu, watu ambao muda wote wanaishi kwa kuamrishwa na Mbowe kuanzia asubuhi hadi usiku.
Wamekuwa ni kama watumishi wake wa ndani nyumbani kwake,wakata majani ya kulishia mifugo yake, vijakazi wake au wakimwambia kwamba hawataki awaburuze kama ng’ombe wake basi ubunge wao nao unaishia palepale.
Ndiyo maana aliposema wanasusia kushiriki vikao vyote vya bunge vinavyokuwa chini ya Dk. Tulia iwe leo, kesho au siku zote watu kama Lwakatare, Onesmo ole Nangole na kadhalika waliokuwa wakidhaniwa kwamba wana hekima ya kutosha, busara za kutosha na uwezo mkubwa wa kufikiri nao tumeona wanavyotoka nje vya vikao kama watoto wa nguchiro.
Wameungana na ‘mbulula’ wengine wanaoishi bungeni kwa kuamrishwa na Mbowe kufanya kila akitakacho mwenyewe, hatua inayothibitisha ukweli wa kauli iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba “bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba”.
Sitaki kurejea kwa mawazo na maneno kuhusu madai waliyotoa ili kuhalalishia ujinga wao mkubwa kabisa wa kisiasa, na pia sina mpango wala dhamira yoyote ya kutaka kuwatetea kwani wanachofanya ni ujinga kama mwingine wowote duniani.
Kama wangekuwa wana hoja, busara ama uwezo kwa hakika wasingemkimbia naibu huyo wa spika, badala yake wangemkabili kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kanuni za Kudumu za Bunge na taratibu nyinginezo, lakini kwa sababu hawawezi ndiyo maana wameamua wamkimbie ili angalau wasiaibike bungeni.
Sina sababu ya kumjadili Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba aliyewatetea kwa sababu amesababisha yeye mwenyewe adharaulike kwa Watanzania wengi.
Badala ya kukemea mauaji hata kwa kudanganyia yakiwemo yaliyofanyika msikitini kule Mwanza, yale ya watu sita wa familia moja waliouawa Sngerema, mauaji ya binti aliyechinjwa jijini Dar es Salaam au ya wale watu wanane waliochinjwa huko Tanga hayo yote kwake hayana msingi wala maana yoyote.
Kitu kizito kabisa anachokipa umuhimu ni ‘mbulula’ wanaotoka nje ya vikao vya bunge ili kumkimbia naibu spika!
Wazalendo waaminifu kwa nchi yetu wanafahamu kuwa kundi hilo lote na watetezi wao, vibaraka wao na wafuasi wao ni adui wakubwa wa maendeleo iwe leo, kesho na hata milele na hawawezi kuliunga mkono.
Ndiyo maana ninasema kwa dhamira safi na kauli moja kuwa tulia Dk. Tulia ili ukomeshe upuuzi unaofanywa na ‘mbulula’ bungeni.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Itikadi na Uenezi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0787 088 870