Home » » Magufuli awavaa JKT, Magereza

Magufuli awavaa JKT, Magereza

Written By CCMdijitali on Wednesday, July 13, 2016 | July 13, 2016

Rais John Magufuli akimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azzan Zungu madawati yaliyotolewa na Ofisi ya Bunge kwa niaba ya wabunge wa majimbo yote nchini, baada ya kukabidhiwa na watengenezaji JKT na Magereza kwenye hafla iliyofanyika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana. Wanaoshuhudia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson (wa pili kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. (Picha na Yusuf Badi).

    Imeandikwa na Halima Mlacha - Habari Leo



RAIS John Magufuli amewataka wananchi na wadau wa maendeleo nchini kuendeleza hamasa, mwamko na nguvu walizozionesha kwenye oparesheni ya upatikanaji wa madawati katika ujenzi wa madarasa.

Aidha, Dk Magufuli amebainisha kuwa pamoja na kuwepo kwa changamoto za uhaba wa madawati, uhaba wa vyumba vya madarasa na vyoo, mfumo mpya wa elimu bure katika shule za msingi na sekondari umeonesha mafanikio hasa katika ongezeko la udahili wa wanafunzi wa darasa la kwanza.

Pamoja na hayo, ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utengenezaji wa madawati inayofanywa na majeshi mawili ya Kujenga Taifa (JKT) na Magereza, baada ya vyombo hivyo vya dola kutumia siku 90 kutengeneza madawati 60,000 kati ya 120,000 waliyotakiwa kutengeneza kwa fedha za Bunge.

Rais Magufuli aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kukabidhi madawati yaliyotengenezwa kutokana na Sh bilioni sita zilizotolewa na Ofisi ya Bunge baada ya kufanikisha mpango wa kubana matumizi yake na kuamua zitumike kununulia madawati.

Alisema tangu atoe agizo la kila halmashauri kuhakikisha shule zake zina madawati ya kutosha, wananchi, wadau na mashirika mbalimbali ya umma na binafsi vikiwemo vyombo vya habari vimeitikia kwa hamasa oparesheni hiyo na kwa mwamko mkubwa.

Alibainisha kuwa baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kutekeleza ahadi yake ya kuanzisha mfumo wa elimu bure, idadi ya udahili iliongezeka maradufu ya awali kwa wanafunzi wanaojiunga na darasa la kwanza.

Alisema kuanzia Januari mwaka huu, jumla ya wanafunzi milioni 1.8 sawa na asilimia 84.5 walidahiliwa kujiunga darasa la kwanza tofauti na mwaka jana ambako wanafunzi 128,000 tu ndio waliodahiliwa.

“Hata hivyo, hakuna jambo zuri linalokosa changamoto, kutokana na ongezeko hili la idadi ya wanafunzi, tumekumbwa na tatizo kubwa la uhaba wa madawati, vyumba vya madarasa na vyoo,” alisema.

Alisema tangu mfumo huo uanze, Tanzania ilikabiliwa na upungufu wa madawati milioni 1.4 kati ya hayo shule za msingi pekee zilikuwa na upungufu wa madawati milioni 1.1.

Dk Magufuli alisema kutokana na changamoto hizo, wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa Machi mwaka huu, aliwaagiza wakuu wa mikoa na watendaji wengine kuhakikisha wanaanzisha oparesheni katika maeneo ili kila mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari apate dawati.

Alisema kutokana na agizo hilo na uhamasishaji uliofanywa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyombo vya habari nchini, wadau mbalimbali walijitokeza zikiwemo kampuni binafsi, mashirika ya umma, wasanii na watu binafsi kuchangia katika oparesheni hiyo.

Alieleza kuwa hadi sasa zaidi ya madawati milioni moja yamepatikana kati ya madawati hayo asilimia 88 yamepelekwa katika shule za msingi na asilimia 95.8 shule za sekondari.

“Kwa maana hiyo kwa shule za msingi kwa sasa tumebakiza asilimia 11.2 tu ya madawati na sekondari asilimia 4.2 ili tufikie lengo la madawati yanayohitajika,” alisisitiza Rais Magufuli.

“Nimefarijika sana kuona Watanzania wote tumeungana kufanikisha oparesheni hii. Hii ndio Tanzania ninayoitaka, na kwa moyo huu tuliouonesha katika suala hili la madawati naomba tukimaliza hapa tuuhamishie kwenye madarasa,” alisisitiza Magufuli.

Aidha, alisema kwa mujibu wa taarifa alizopatiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, takribani halmashauri 24 zimefikia malengo ya kupata madawati kwa asilimia 100 katika shule za msingi na halmashauri 46 katika shule za sekondari.

Halikadhalika, Dk Magufuli alisema taasisi za Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni wa PPF na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zilimuahidi na kutangaza hadharani kuwa nazo zitachangia fedha kwa ajili ya kutengenezea madawati, lakini hadi sasa hajakabidhiwa fedha hizo.

“Pamoja na taasisi hizi kutangaza hadharani hasa BoT iliyoahidi kutoa shilingi bilioni nne, hazijanipatia fedha zao ila nikizipata nitazielekeza kwenye madawati,” alisema.

Dk Magufuli pia alipongeza hatua ya wabunge kushirikiana bila kujali itikadi na vyama vyao na kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha suala la upatikanaji wa madawati na kusisitiza kuwa ni wakati sasa kwa Watanzania kuweka mbele uzalendo na maslahi ya taifa badala ya vyama vyao.

“Kwa mwelekeo wa leo (jana) nadiriki kusema Tanzania tumeweka historia mpya. Ndugu zangu Tanzania ni yetu sote na ndio maana hata katika kampeni zangu nilisema tuweke maslahi ya watanzania mbele, tushirikiane bila kujali vyama vyetu kutatua shida za Watanzania,” alisisitiza.

Pia alimpongeza Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita (Chadema), kwa kauli zake zenye mlengo wa maendeleo alizokuwa akizitoa katika maeneo mbalimbali. “Kauli zako nyingi ni za maendeleo, ila wasije wakakufukuza kwa kuwa nimekusifia. Wakikufukuza nina nafasi nitakupa kwa sababu unapenda maendeleo,” alieleza.

Alishukuru na kulipongeza Bunge kwa kuamua kwa makusudi kubana matumizi na kukubali fedha walizomkabidhi Rais ziende kwenye madawati.

“Mfano mzuri ni leo hii watoto wetu sasa wanakaa kwenye madawati, ukiwaona huwezi kujua nani baba yake ni Chadema, ACT-Wazalendo wala CCM. Utakachokina wote ni watoto wa Watanzania,” alifafanua.

Akizungumzia kazi ya kutengeneza madawati hayo iliyofanywa na JKT na Magereza, pamoja na kupongeza ubora wa madawati hayo, alibainisha wazi kusikitishwa na kasi ya utengenezwaji wake ambayo haiendani na uharaka wa upatikanaji wa madawati hayo.

Alisema majeshi hayo yalikabidhiwa fedha hizo Sh bilioni sita na Bunge tangu Aprili 11, mwaka huu hadi jana tayari zilishapita siku 90, lakini yameweza kukabidhi madawati 60,000 tu kati ya madawati 120,000 waliyotakiwa kutengeneza.

“JKT ina kambi zaidi ya 10 nchi nzima, na kila kambi kuna kuruta na wale wanaopewa adhabu, inawezekana vipi jeshi hili litengeneze madawati 30,000 kwa siku 90, yaani ina maana lilikuwa linatengeneza madawati 30 kwa siku?” alihoji.

Kuhusu Magereza, alisema pia jeshi hilo limemuangusha kwa kuwa pamoja na kuwepo kwa magereza ya wafungwa katika kila mkoa na wilaya isipokuwa wilaya mpya, pia jeshi hilo limetengeneza madawati 30,000 kwa miezi mitatu kwa maana ya madawati 30 kwa siku.

“Wafungwa wako wengi na wengine hata leo wamefungwa, kila mkoa kuna magereza ukiacha wilayani, na Serikali imekuwa ikitenga fedha za kutosha kwa ajili ya chakula cha wafungwa hawa, kwanini haingii akilini eti wametengeneza madawati 30 tu kwa siku,” alisisitiza.

Aliyataka majeshi hayo kujipanga na kuja na mikakati itakayoyaweza kutengeneza kwa kasi madawati pindi wanapopatiwa zabuni, ili wanapojitokeza wafadhili wengine, majeshi hayo yaendelee kutengeneza madawati hayo.

Kwa upande wa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema kazi ya utengenezaji wa madawati 60,000 katika awamu ya kwanza imekamilika na kwamba hadi jana jumla ya madawati 53,450 yalikamilika na kukabidhiwa kwa taasisi hiyo.

Alisema ofisi hiyo ya Bunge ilitarajia kukabidhiwa awamu ya kwanza ya madawati hayo leo, lakini kutokana na changamoto katika utekelezaji wake kazi hiyo haikukamilika kama ilivyopangwa hivyo madawati yote ya awamu ya kwanza yatakamilika rasmi Julai 30, mwaka huu na awamu ya pili yatakamilika Septemba 30.

Alisema katika awamu ya kwanza kwa mujibu wa Tume ya Utumishi wa Bunge madawati hayo yatakabidhiwa kwa mikoa 15 ambayo ni Pwani, Morogoro, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba, Tanga na Dar es Salaam.

Mbunge wa Ilala, Musa Azzan Zungu alikabidhiwa madawati 537 kwa ajili ya Jimbo la Ilala na madawati mengine yaliyobaki kwa niaba ya wabunge wote wa majimbo nchini. Awamu ya kwanza jumla ya majimbo 155 kati ya majimbo 264 yatapatiwa madawati sawa na asilimia 59 ya madawati yote.

Kwa mujibu wa Dk Tulia, ugawaji wa madawati hayo umezingatia ukaribu wa mikoa na maeneo yalikotengenezewa ambayo ni Ukonga-Magereza, JKT-Chang’ombe, Itende-Mbeya, Mafinga-Iringa, Mlale-Songea na Maramba-Tanga.

Awamu ya pili, madawati hayo yatagawiwa katika kanda mbili ambazo ni Kanda ya Kati, Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Magharibi. Awamu hiyo ya pili madawati hayo yatatengenezwa katika maeneo ya JKT Kanembwa na Mtabila mkoani Kigoma, Uyui-Tabora, Samani- Arusha na Kiwira-Mbeya.

Aprili 11, mwaka huu, Bunge lilimkabidhi Rais Magufuli Sh bilioni sita ilizoziokoa kwa kubana matumizi katika maeneo mbalimbali kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, ikiwemo posho, safari za nje na viburudisho ambazo Rais huyo aliagiza zitumike kununua madawati kwa kila jimbo.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link