Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Lu Youqing kati kati akielezea mikakati atakayoitekeleza katika kuratibu usimamizi wa miradi ya Zanzibar iliyopata ufadhili wa Nchi yake ya China.
Makamu wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Lu Youqing mara baada ya mazungumzo yao ya kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na China.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Nchini Tanzania Bwana Lu Youqing ameahidi kufanya jitihada za makusudi katika kufuatilia taratibu za Mikataba ya makubaliano kwa upande wa Nchi yake ili kuona kwamba miradi yote ya Zanzibar iliyopata ufadhili wa Nchi hiyo inaanza, inaendelea na kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Akizungumza na Makamu wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipomtembelea Ofisini kwake katika Jengo la SMZ Magogoni Jijiji Dar es salaam Balozi Lu Youqing aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duri, ukamilishaji wa ujenzi wa eneo la maegesho ya Ndege kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar pamoja na Mradi wa Kisasa wa mawasiliano kwenye ofisi zote za SMZ { E government }.
Balozi Lu Youqing. alisema zipo taratibu za ukamilishaji wa Miradi iliyoanzishwa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili ambayo imeonekana kuchelewa kiasi kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Jamuhuri ya China kwa Uongozi wa Benki ya Taifa ya China { Exim Bank }.
Alisema jukumu alilonalo kwa sasa ni kuzungumza moja kwa moja na Uongozi wa Benki hiyo kupitia Wizara ya mambo ya Nje ya China ili kupata uelewa wa masuala hayo katika azma ya kuangalia mapungufu yaliyojitokeza ya miradi hiyo na kutafuta mbinu za pamoja za kuyakamilisha.
Balozi Youqing Alieleza kwamba hatua hiyo inafuatia kuheshimu Vikao na mazungumzo ya pamoja kati ya Viongozi Wakuu Rais Shii Jinping wa Jamuhuri ya Watu wa China na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barazala la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kuhusu Miradi hiyo ya Kiuchumi na Maendeleo.
Alifahamisha kwamba Historia inaonyesha wazi kwamba Visiwa vya Zanzibar vina kumbukumbu ndefu ya kuwa Kituo cha Kibiashara Duniani kwa karne nyingi zilizopita kikitumiwa pia na wafanyabiashara wa Bara la Asia wakiwemo wale wa Jamuhuri ya Watu wa China.
Balozi Youqing aliahidi kwamba kwa kutumia uwezo wake wa Kidiplomasia atahakikisha kwamba Nchi yake inaendelea kufanyakazi pamoja na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika kuimarisha miundombinu itakayosaidia kukuza kwa uchumi wa Tanzania hasa sekta ya Kibiashara itakayosaidia kustawisha wananchi walio wengi.
“ Nitafanya juhudi za makusudi kwa kuuhimiza Uongozi wa Exim Benki ya China inayoratibu uwezeshaji wa miradi ya Kiuchumi na Maendeleo katika Mataifa rafiki hasa yale ya Bara la Afrika kukamilisha taratibu ili kutoa fursa ya kukamilisha miradi yote iliyoanzishwa ”. Alisema Balozi Youqing
Alisema Benki hiyo ya Exim imekuwa na mpango Maalum kwa uratibu wa Nchi hiyo kuunga mkono ufadhili wa Uwezeshaji wa Miradi mikubwa iliyoanzishwa na Mataifa Rafiki na Nchi hiyo katika kipindi cha Miaka Kumi.
Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Nchini Tanzania amwapongeza Wananchi wa Zanzibar kwa jitihada zao za kukamilisha zoezi la Pili la Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Machi mwaka huu kwa misingi ya amani na utulivu.
Alisema China imeguswa na hali hiyo kiasi kinachoonyesha kuridhika kwake na kuwa na shauku ya kuzidi kuunga mkono maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar katika kujikwamua Kiuchumi.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Balozi Zake za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kusaidia miradi ya Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema China imeonyesha wazi imani yake kwa Zanzibar katika kusaidia kuunga mkono miradi ya ujenzi wa Gati ya Kwampigaduri Maruhubi, Maegesho ya Ndege katika uwanja wa Ndege wa Zanzibar pamoja na ukamilishaji wa Mradi wa Kisasa wa mawasiliano kwenye Ofisi za SMZ { E. government }.
Alisema muendelezo wa Serikali ya China katika kuiunga mkono Zanzibar unaleta faraja na matumaini makubwa kwa Wananchi waliowengi wa Visiwa vya Zanzibar katika kukomboka kiuchumi.
Balozi Seif alitolea mfano ukombozi huo ni ule ujenzi wa Gati ya Kisasa ya Mpigaduri ambao utasaidia kukwamua msongamano mkubwa uliopo hivi sasa katika Bandari Kuu ya Malindi hasa uhifadhi wa Makontena yanayoshushwa na kuingia kwa kasi kubwa.
Alimfahamisha Balozi huyo wa Jamuhuri ya Watu wa China kwamba hivi karibuni alijionea hali halisi ya mrundikano wa Makontena yanayozagaa na kushindwa hifadhi ndani ya Bandari ya Malindi hali ambayo imeleta wasi wasi mkubwa kwa wafanyabiashara wengi walioagiza bidhaa zao kwa ajili ya Siku Kuu ya Iddi el-Fitri.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/7/2016.