Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe jana mjini hapa, Malecela alisema tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka jana, amekabidhi majukumu mengi ya serikali mikononi mwa vijana, kwa hiyo anadhani na chama kizingatie jambo hilo.
“Nitafurahi kwenye chama kama tutajaribu kutoa nafasi za utendaji kwa vijana kama ilivyofanyika kwenye serikali.
Kuna haja ya kuwa na mabadiliko ya namna hiyo ili CCM ya mbeleni ijengwe na vijana,”alisema Malecela, ambaye alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia mwaka 1990 hadi 1994.
Ushauri huo wa Malecela unaendana na kauli ya Rais Magufuli aliyoitoa Mei 26, mwaka huu, wakati alipofungua mkutano wa Bodi ya Makandarasi Tanzania, aliposema wazee ndiyo wameifikisha nchi hapa ilipo leo na kuona haja ya kuteua vijana wengi ili waendane na kasi yake.
AZUNGUMZIA KOFIA MBILI
Malecela alifafanua kuwa Rais Magufuli atakabidhiwa wadhifa wa Mwenyekiti wa CCM kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ambayo kuna ibara inayosema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atapaswa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
Mkutano Mkuu Maalum wa CCM unafanyika Jumamosi na Rais Magufuli anatazamiwa kukadhiwa kofia ya kuongoza chama hicho.
Katika siku za karibuni kumekuwa na minong’ono kuwa baadhi ya makada wa CCM wana hofu na Rais Magufuli na kutaka Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Jakaya Kikwete aendelee kushika nafasi hiyo.
Hata hivyo, CCM ilishaweka utaratibu wa Rais anayekuwapo madarakani kukabidhiwa uongozi wa chama hicho.
“Hapa ukiuliza uongozi wa CCM sijui utakuwa wa namna gani mimi naona utakuwa ule ule ambao unaongozwa na katiba na kanuni za CCM,” alisema Malecela, ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM kuanzia mwaka 1997 hadi 2007.
Kuhusu hofu ya kasi ya Rais Magufuli kukisambaratisha chama, Malecela alisema watu wanaotoa kauli hiyo wana mawazo potofu na hayana msingi kwa sababu Rais ameanza vizuri na anakwenda vizuri.
Alisema binafsi anaamini CCM mikononi mwa Rais Magufuli itakuwa salama kama vile serikali ya Jamhuri ya Muungano ilivyo salama mikononi mwake.
“Napenda kusisitiza kwa wale wote wanaofikiri tukimpa Magufuli chama basi atakisambaratisha, sijui wanapata mawazo haya kutoka wapi na misingi yao ni nini, kwa sababu huyu ni mtu ambaye kwa mara ya kwanza katika Tanzania alikifanya kitu kikaifanya nchi nzima kutoka nje na kufanya usafi barabara,” alibainisha Malacela ambaye ametumikia serikali kwa nyadhifa mbalimbali zikiwamo za uwaziri, ubalozi na mkuu wa mkoa.
Alisema kiongozi huyo ameweza kufanya maeneo ya nchi yamekuwa safi na kwa sasa hakuna mifuko ya plastiki inayoning’inia kwenye miti barabarani na kuongeza kwa kazi hiyo nzuri hawezi kukisambaratisha chama.
“Kama ameweza kurudisha imani kwenye serikali, kwenye chama atavuruga nini? Kwa hiyo mimi mawazo ya hawa watu wanaosema atasambaratisha chama wana mawazo potofu kabisa ambayo hayana msingi wowote,” aliongeza Malecela, ambaye alipachikwa jina la utani la `Tinga tinga’ kutokana umahiri wake kwenye kampeni katika kipindi akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM.
KATIBU MKUU WA CCM
Kadhalika, Malecela alizungumzia uteuzi wa Katibu Mkuu wa CCM ajaye, ambapo alishauri ni muhimu mwenyekiti huyo aamue kwa kupendekeza majina kadhaa ya watu ambao anadhani wataweza kuendana na kasi yake.
Katibu Mkuu wa sasa wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, ametangaza kuachia nafasi hiyo.
Malecela alionya si vizuri kila mwana CCM akashinikiza mtu wake, hali hiyo inaweza kusababisha ikafika mahali ikamchanganya mwenyekiti.
“Kwa maoni yangu nafikiri itakuwa muhimu yeye kama ni mtendaji mkuu wa serikali na sasa atakuwa Mwenyekiti wa chama, awe ana haki ya kusema kwamba nani awe Katibu Mkuu wa chama na anamfaa kutokana na kasi yake ya utendaji,”alishauri Malecela.
Malecela alisema Magufuli akitaka kupata Katibu Mkuu bora basi aangalie Katiba ya CCM na afuatilie rekodi za utendaji wa makatibu waliopita kama Kinana, Philip Mangula na Hayati Rashid Kawawa.
KATAZO LA MIKUTANO YA VYAMA VYA SIASA
Alipoulizwa kuhusu vyama vya siasa kuzuiwa kufanya siasa hadi 2020, kama si kuua demokrasia, Malecela alisema si vizuri kila wakati watu wa kuzozana watoe nafasi kwa chama kilichoshinda kitekeleze yale yaliyoahidiwa kwa wananchi kama nchi zingine zinavyofanya.
Alisema mara nyingi watanzania wanapoangalia hayo mambo hawachukui mifano kutoka nchi zingine kama vile Ufaransa.
Alibainisha nchi hiyo imefanya uchaguzi hivi karibuni na kuna vyama vya upinzani lakini hata siku moja havijawahi kulalamika kuminywa demokrasia au kiongozi wa upinzani kushindana na rais aliyepo madarakani.
“Wenzetu kule ukishashindwa uchaguzi basi unamwacha huyu aliyechaguliwa aendeshe nchi lakini sisi bahati mbaya upinzani wa kwetu unakuwa ni kama mtu umeshindwa kwenye mashindano ya mbio sasa unataka uoneshe kwamba unaweza kukimbia kwa kufanya mazoezi halafu inafika mahali unasema mimi nimepata nyingi kuliko za yule,” alisema Malecela.
Aliongeza kuwa hata Uingereza hivi karibuni wamepiga kura ya kutoka kwenye EU (Umoja wa Ulaya) na hivi sasa wanaendelea na mambo mengine ya nchi.
Alisema tatizo lililopo kwa Waafrika ni kwamba uchaguzi ukishamalizika wanaendelea kukabana shingo kati ya serikali na vyama vya upinzani na kutolea mifano yanayoendelea Tanzania na Kenya.
Alibainisha wanasiasa wa Tanzania wasipoondokana na tabia hiyo watabaki kila siku wao ni watu wa kuzozana na kushauri wapinzani watoe nafasi kwa vyama vilivyoshinda vitekeleze yale waliyowaahidi watu.