Home » » Waziri Nape Nnauye azindua Miradi Nane inayofadhiliwa na Tanzania Media Foundation

Waziri Nape Nnauye azindua Miradi Nane inayofadhiliwa na Tanzania Media Foundation

Written By CCMdijitali on Wednesday, July 13, 2016 | July 13, 2016

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (kulia) akipokea zawadi ya bango la picha zilizopigwa na baadhi ya Waandishi wa Habari waliowahi kujengewa uwezo na Tanzania Media Foundation toka kwa Mkufunzi wa Picha, Bw. Mwanzo Millinga 12 Julai, 2016 jijini Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (kushoto) akipokea bahasha yenye mafanikio ya Tanzania Media Foundation ambayo yamefanywa nchini katika kuwajengea uwezo Waandishi wa habari toka kwa Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation, Bw. Ernest Sungura 12 Julai, 2016 jjijjini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye akiongea na wageni waalikwa pamoja na baadhi ya Waandishi wa habari waliohudhuria hafla ya unzinduzi wa Miradi Nane inayofadhiliwa na Tanzania Media Foundation 12 Julai, 2016 jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Wageni waalikwa pamoja na waandshi wa habari wakifuatilia hafla ya Uzinduzi wa Miradi nane inayodhaminiwa na Tanzania Media Foundation 12 Julai, 2016 jijini Dar es Salaam.

(Picha/Stori na Benedict Liwenga)

Serikali kwa kushirikiana na Uongozi wa Tanzania Media Foundation itaendelea kushirikiana bega kwa bega katika kuwawezesha Waandishi wa Habari nchini kupenda kutembelea maeneo ya vijijini na kuandika habari mbalimbali kuhusu changamoto za maeneo hayo.
 
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye wakati akizindua Miradi Nane ambayo inafadhiliwa na Taasisi hiyo ambayo unahusisha Waaandishi wa Habari kutembelea maeneo ya vijijini na kuandika habari mbalimbali kwa lengo la kuelimisha Umma.
 
Mhe. Nnauye amesema kuwa, Serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na Taasisi hiyo ya kuwajengea uwezo Waandishi wa habari na kuwawezesha kifedha kwa ajili ya kwenda kutafuta habari mbalimbali katika maeneo ya vijijini.
 
‘’Ni muhimu kwa waandishi wa habari kufika maeneo ya vijijini na kuapata habari mbalimbali kwa jili ya kuhabarisha umma, hivyo Serikali bado iko na nyie na itaendelea kuwaunga mkono na endeleeni na kazi hiyo nzuri’’, alisema Mhe. Nnauye.
 
Ameongeza kuwa, kuna haja ya Taasisi hiyo kuendelea kujenga uwezo wa kusaidia kupata umakini katika kazi za habari ili jamii iweze kuwa na imani na Serikali pamoja na Vyombo vya habari na pia kuonyesha juhudi ya kuendelea kuwajengea uwezo wanahabari ili waweze kuwafikia watu wenye mahitaji makubwa ya habari ambao ni watu wa vijijjini ambao wakati mwingi wamekuwa wakichelewa kupata habari.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation, Bw. Ernest Sungura ameyataja baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa na Taasisi hiyo katika kuwajengea uwezo wanahabari nchini ambapo amesema kuwa, mpaka sasa wameweza kuwajengea uwezo jumla ya Waandishi wa habari wapatao 700 pamoja na Vyombo vya Habari 135.
 
Mbali na kuanza na miradi ya mwandishi mmoja mmoja, kwa sasa wanatarajia kuanza na miradi mingine inayoanza mwishoni mwa mwezi huu na itakuwa ni ya Awamu ya Pili ambapo itahusisha jumla ya Waandishi wa habari wapatao 30 kwenda vijijini kufanya kazi za kihabari na kupewa mafunzo ya namna ya kuandika habari za vijijini.
 
‘’Kwa sasa tumeanza mradi wa watu kubobea katika eneo maalum na safari hii tutajikita katika masuala ya Viwanda yaani kuwaandaa waandishi wa habari watakaobobea katika masuala ya viwanda na tayari tumeshamdokeza Waziri wa Viwanda kuhusu taarifa hizo kwa ajili ya kuizindua miradi hiyo’’, alisema Sungura.
 
Ameongeza kuwa katika kuandika masuala ya viwanda, tayari kuna waandishi wa habari wapatao 10 ambao hivi sasa wanajengewa uwezo ili waweze kuendana na kasi ya Serikali na katika suala la kuwandaa waandishi hao wanatumia Waandishi wa habari wazoefu pamoja na wadau wengine.
 
Amefafanua kuwa, lengo kubwa la kazi hizo zote ni kuwawezesha waandishi nchini kuweza kuyafikia maeneo ambayo yamekuwa hayafikiki, hivyo wanatoa rasimali fedha kwa waandshi hao ili kuweza kutembelea maeneo hayo na kuhabarisha umma.
 
‘’Ziko takwimu nyingi kila mahali kama vile za maji, afya, alimu lakini baadhi ya waandishi wetu hawafanyi ule uandishi wa kuzifanya takwimu hizo zieleweke na ziwe na manufaa kwa walaji, hivyo sisi tumeamua kuwajengea waandishi katika maeneo hayo’’, alisema Sungura.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link