Home » » Magufuli kufikia Lumumba

Magufuli kufikia Lumumba

Written By CCMdijitali on Friday, August 12, 2016 | August 12, 2016

Rais John Magufuli akiwa na mke wake Janeth Magufuli wakiingia katika ofisi ya ccm, Lumumba.picha maktaba.

Romana Mallya | Nipashe 

RAIS John Magufuli leo anatarajia kwenda moja kwa moja kwenye ofisi yake ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyopo Lumumba jijini Dar es Salaam, baada ya jana kumaliza ziara ya mikoa ya kanda za Kati na Ziwa, ikiwa ni mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Julai 23.

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka aliiambia Nipashe jijini Dar es Salaam jana kuwa Rais atakwenda moja kwa moja makao makuu ya CCM, Lumumba akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimtaifa wa Julius Nyerere.

Ole Sendeka alisema anatarajiwa kupokelewa na viongozi wa chama pamoja na wanachama wa chama hicho.

“Ujio huu ni wa kwanza tangu achaguliwe mjini Dodoma kuwa Mwenyekiti wa chama. Mambo mengine yatatokana na maelezo yake atakayotoa baada ya kutembelea ofisi yake na kujionea yaliyomo,” alisema.

Julai 23 wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CCM mjini Dodoma, walimchagua Rais Magufuli kwa asilimia 100 kuwa Mwenyekiti wa chama hicho akimrithi Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Kwenye mkutano huo aliainisha mambo kadhaa ambayo atakabiliana nayo katika kipindi chake cha kukiongoza chama hicho ili kiendelee kuwa kimbilio la Watanzania na kushinda kirahisi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Rais Magufuli aliahidi kushughulikia tatizo la ufisadi, utegemezi wa chama kwa matajiri ambao hupewa vyeo vya ukamanda wa vijana, rushwa katika mchakato wa kupata vyeo ndani ya CCM, ufisadi wa mali za chama na pia tatizo la ukosefu wa maadili.

Pia aliahidi kushughulikia tatizo la kuwapo kwa baadhi ya makada wanaojirundikia vyeo, udhaifu wa baadhi ya jumuiya za chama na umuhimu wake kwa Watanzania na suala la maslahi kwa watendaji wa CCM.

Magufuli pia aliahidi kupitiwa upya katiba ya chama hicho ili kuona uwezekano wa kuboresha baadhi ya maeneo anayoamini kuwa kwa sasa yamepitwa na wakati ikiwa ni pamoja na kuondoa utitiri wa vyeo kwa mwanachama mmoja.

Aidha, aliahidi kuweka watendaji wenye sifa na kuunda kikosi maalum ambacho kitahakiki mali zote za chama na kujua zipo wapi na zinatumiwa na nani.

Aliahidi pia kuongeza idadi ya wanachama ambao kwa sasa wapo milioni 8.7 na kuhakikisha wanalipa ada zao kwa njia ya kieletroniki.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link