Home » » Utendaji wa Magufuli wavutia mameya Uganda

Utendaji wa Magufuli wavutia mameya Uganda

Written By CCMdijitali on Saturday, August 27, 2016 | August 27, 2016

Rais John Magufuli.

Imeandikwa na Sophia Mwambe | Habari Leo

JUMUIYA ya Mamlaka za Miji kutoka Uganda (UAAU), imesema imevutiwa na utendaji wa Rais John Magufuli.

Imesema hali hiyo ndiyo iliyowasukuma kuja nchini, kujifunza namna serikali inavyofanya kazi.

Hayo yamesemwa na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Koboko nchini Uganda, Sanya Wilson ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo. Alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipozungumzia ziara yao ya siku tatu nchini.

Alisema nchi yao imekuwa na amani kwa sababu ya Tanzania, na ndio maana wamekuja kujifunza namna serikali inavyofanya kazi kupitia halmashauri zake. Alisema wamekuja kuona ni mbinu gani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imetumia kudhibiti pikipiki kuingia mjini, kwani katika nchi yao tatizo hilo bado ni kubwa.

“Tunaamini elimu tutakayoipata hapa tutaipeleka Uganda ili itusaidie kumaliza changamoto ya pikipiki mijini ambayo bado inatusumbua,” alisema Wilson.

Aliongeza kuwa ziara hiyo, pia itatumika kujifunza namna Jiji la Dar es Salaam linavyodhibiti uchafu na kulifanya lionekane safi pamoja na kuangalia hali ilivyo pembezoni mwa bahari.

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema jumuiya hiyo ipo jijini kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yanayofanywa ikiwemo miundombinu, huduma za jamii na namna walivyoweza kuzuia pikipiki kuingia mjini na hali ilivyo pembezoni mwa bahari.

Alisema Tanzania na Uganda zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu, hivyo kupitia ziara hiyo ya siku tatu inayofanywa na wajumbe zaidi ya 200, mkoa huo utapata kitu cha kujifunza kutoka kwao.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link