Na Stella Kalinga, Simiyu
Zaidi ya Vijiji 63 vya wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu vinatarajia kupata umeme kupitia
Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya III inayoanza mwishoni mwa Mwezi
Septemba, 2016.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Merdard Kalemani
alipozungumza na wananchi wa maeneo tofauti ya wilaya ya Itilima wakati wa Ziara yake ya
kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.
Pamoja na kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi kutoka katika vijiji hivyo 63 Dkt.
Kalemani amesema Serikali imedhamiria kupeleka huduma ya umeme katika Taasisi za
Serikali zikiwemo shule za Msingi na Sekondari Ofisi za Serikali, Vituo Vya Afya na
Zahanati na katika maeneo ya miradi ya maji.
Dkt. Kalemani ameelekeza Serikali za vijiji kwa kushirikana na Shirika la Ugavi wa Umeme
(TANESCO) kuainisha wananchi wanaohitaji huduma ya umeme ili mradi utakapoanza
kutekelezwa waanze kupata huduma hiyo mara moja.
Wakati Serikali ikiweka mikakati ya kujenga Ofisi za TANESCO Wilaya, Naibu Waziri
Nishati na Madini amemuagiza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Rehema
Mashinji kuteua maafisa watatu kutoka katika Ofisi yake watakaowafuata wananchi vijijini
badala ya wananchi kuifuata huduma maofisini.
Aidha, Dkt Kalemani amelitaka Shirika la Umeme TANESCO kuainisha wataalam wake
wanaohusika na REA, kupeleka Orodha yao katika Ofisi za Vijiji na kutoa elimu juu ya
gharama na taratibu za kuunganisha umeme ili wananchi wasidanganywe.
“Ili kudhibiti ulaghai wa kuongeza gharama ambazo hazipo kila mtaalam awe na muhuri na
majina yote ya wataalam wa TANESCO yapelekwe katika Ofisi za Vijiji tuweze kuwatambua
vishoka. Kuna watu wanaweza kuwaongezea wanachi gharama wakati gharama halisi ni
shilingi 27,000/= kwa yule ambaye ameshasuka nyaya kwenye nyumba yake, na fomu
anachukua bure.” Alisema Kalemani.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga amesema anaishukuru
Serikali kwa kuwaweka katika mpango wa kupata umeme wananchi wa Wilaya ya Itilima na
akawataka Wenyeviti wa Serikali za Vijiji kupita katika kaya zote na kusaidia kubaini kaya
zisizona umeme katika maeneo yao.
Wakati huo huo Mhe. Dkt. Kalemani amekitambulisha kifaa cha kuweka umeme bila kusuka
nyaya ndani ya nyumba kiitwacho UMETA kinachotumika kuunganisha umeme kwa
gharama isiyozidi 36,000/=,ambapo amesema kifaa hicho kinaweza kuwasaidia wananchi
wasio na uwezo wa kusuka nyaya katika nyumba zao
Akizungumza mara baada ya hotuba ya Naibu Waziri, Bibi.Milembe Katani mkazi wa Kijiji
cha Nanga Kata ya Chinamili amesema anaishukuru Serikali kwa kuweka mikakati ya
kuwapelekea umeme kwa kuwa utasaidia vijana wao kujiajri katika saluni, kuchomelea
vyuma, na kuwekeza katika Mashine za kukamua alizeti na kukoboa mpunga.
Naibu Waziri Dkt. Kalemani yuko Mkoani Simiyu kwa ajili ya ziara ya Siku tatu ambapo
amekagua miradi mbalimbali ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika Wilaya za Busega,
Bariadi na Itilima.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani akizungumza na
wananchi wa kata ya Sawida wilayani Itilima (hawapo pichani) , wakati wa Ziara yake ya
kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani (wa pili kushoto)
na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji (wa nne kulia mbele) walipokutana katika ukaguzi
wa Mradi wa Kisima kilichochimwa kwa ushirikiano wa Misri na Tanzania, wakati wa Ziara
zao wilayani Itilima; Mhe.Kalemani alikuwa akikagua miundombinu ya umeme katika mradi
na Mhe. Kamwelwe kukagua miradi ya Maji.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani (kushoto) na
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe (kulia) wakishauriana jambo
walipokutana katika ukaguzi wa Mradi wa Kisima kilichochimbwa kwa ushirikiano wa Misri
na Tanzania, wakati wa Ziara zao wilayani Itilima; Mhe.Kalemani alikuwa akikagua
miundombinu ya umeme katika mradi huo na Mhe. Kamwelwe kukagua mradi huo wa maji,
(katikati) Mbunge wa Jimbo la Itilima, Njalu Silanga.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Sawida wakionesha mabango yao wa Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani(hayupo pichani) wakati wa Ziara
yake ya kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani (kulia)
akimkabidhi Milembe Katani, Mkazi wa Kijiji cha Nanga Wilayani Itilima kifaa cha UMETA
, wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II
Mkoani Simiyu.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Chinamili wilayani Itilima wakimshangilia Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani(hayupo pichani) wakati wa Ziara
yake ya kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani akizungumza na
wananchi wa kata ya Chinamili wilayani Itilima(hawapo pichani) , wakati wa Ziara yake ya
kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu