Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Demokrasia mjini Unguja Jumamosi Agosti 3.2016 |
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeipongeza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanzia Dkt. John Pombe Magufuli aliyotoa katika ziara zake Zanzibar, iliyosisitiza dhamira ya serikali kuharakisha maendeleo kwa wananchi bila ya kujali tofauti za kisiasa.
CCM imesema inaunga mkono na kupongeza kwa dhati hotuba hizo zilizotolewa Unguja na Pemba ziliyosisitiza dhamira ya serikali zote mbili ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na Zanzibar kuwaletea wananchi maendeleo bila ya kujali itikadi za kisiasa.
Akizungumza Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar wa Idara ya ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakar Jabu |
Vuai alieleza kwamba ziara hiyo imetoa muongozo imara wa kuwakumbusha watendaji na viongozi nchini juu ya dhamana na mambo ya msingi wanayotakiwa kuyatekeleza kwa wananchi.
“CCM tunaunga mkono kwa nguvu zote hotuba ya Rais wetu Dkt. John Magufuli kwani imezungumzia na kugusia mambo ya msingi yanayogusa maisha ya wananchi hasa wa kipato cha chini na kutoa muongozo wa namna gani serikali zetu zinaendelea na mikakati imara ya kuimarisha uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Pia tunatakiwa kuendelea kuwa wamoja na wazalendo bila ya kujali tofauti zetu za kidini, kisiasa na kikabila kwa kulinda amani na utulivu wa nchi zetu kwani ndio siri ya mafanikio ya nchi zetu.”, Alisisitiza Waride.
Katibu huyo , alisema Dkt. Magufuli ameonyesha nia ya dhati ya kuendelea kutafuta fursa mbali mbali za miradi ya maendeleo itakayoweza kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.
Alisema miongozo mwa mambo ya msingi yaliyosisitizwa na Dkt. Magufuli pia yanaungwa mkono na CCM Zanzibar ni dhamira ya kuhakikisha Zanzibar inakuwa ni nchi ya Viwanda vya kusindika samaki wanaotokana na Uvuvi wa Kisasa wa Bahari kuu vitakavyotoa fursa za ajira kwa vijana na wananchi.
Waride, alipongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua milango ya wawekezaji wakubwa kuwekeza Zanzibar huku wakitafuta wahisani kutoa mamilioni ya fedha za kuendesha miradi ya kijamii ukiwemo mradi wa maji safi Unguja uliotolewa fedha za mkopo na Serikali ya India.
Alisema kwa ushirikiano wa Rais Dkt. Magufuli na Dkt. Shein, CCM inaamini kwamba Tanzania bara na Zanzibar kwa ujumla zitakuwa nchi za kupigiwa mfano duniani katika nyanja mbali mbali za kimaendeleo, kisiasa na kijamii.
Alifafanua kwamba CCM Zanzibar, inaungana na Dkt. Magufuli kupinga siasa za misimamo mikali na utengano zinazofanywa na baadhi ya vyama vya kisiasa Zanzibar kuwa haziwezi kuleta maendeleo ya nchi badala yake zitajenga migogoro isiyokuwa ya lazima.
Alisema CCM inasifu msimamo wa Dkt. Magufuli wa kulinda Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 huku akiahidi kuendelea kulinda amani na Utulivu wa nchi kwa gharama yoyote.
Pamoja na hayo Waride aliahidi kuwa CCM itaendelea kuwa balozi mzuri wa kuwasihi wafuasi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kufanya siasa za maendeleo zitakazoweza kwenda sambamba na malengo ya serikali.
Aidha Waride alipongeza juhudi za Rais wa Zanzibar, Dkt. Shein za kuongoza nchi kwa ufanisi mkubwa licha ya kuwepo na changamoto mbali mbali za kisiasa nchini.
Alielezea kuridhishwa kwake na kauli ya Dkt. Shein ya kuwataka wapinzani kusahau Serikali ya Mpito kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi huku akisisitiza hakuna sababu ya kuwa na aina ya serikali hiyo kwa sababu uchaguzi umefanyika kwa njia ya huru na haki.
Katika Mkutano huo, Dk Shein alisema kazi kubwa inayofanywa kwa sasa ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015, huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa katika hatua ya mwisho ya kuanza kazi za kuchimba mafuta na ges ili kutoa hatua pana ya ajira kwa wananchi.
Alisema muswada wa mafuta na gesi tayari umewasilishwa katika Baraza la Wawakilishi na kusomwa kwa mara ya kwanza ambapo katika kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi kitakachofanyika Septemba 26 utasomwa kwa mara ya pili na kusubiri saini yake.
Ziara hiyo ya Dkt. Magufuli ya kuwashukru wananchi wa Zanzibar kwa kumchagua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi Mkuu uliopita, imefanyika katika maeneo mbali mbali Pemba na Unguja.