Home » » Kitanzi kingine watumishi wa umma

Kitanzi kingine watumishi wa umma

Written By CCMdijitali on Sunday, September 25, 2016 | September 25, 2016

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki

Imeandikwa na Ikunda Erick | Habari Leo


MWAROBAINI wa uwepo wa watumishi hewa katika sekta ya umma umepatikana ambapo kuanzia Oktoba 3, mwaka huu, utambuzi wa watumishi wote wa umma kwa kutumia mfumo mmoja wa kukusanya na kuhifadhi taarifa, utaanza huku watumishi wote wa umma, wakitakiwa kupeleka nyaraka muhimu ndani ya wiki mbili.

Utambuzi huo, utafanywa na serikali kwa kushirikisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huku uhakiki na utambuzi huo ukiwalenga watumishi wote wa umma walio kwenye wizara, idara za serikali zinazojitegemea na tawala za mikoa.

Wengine ni mamlaka za serikali za mitaa, wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma, ambapo watumishi wote wa umma wametakiwa kupeleka taarifa zote muhimu zinazowatambulisha katika mamlaka zilizotajwa.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usajili wa vitambulisho vya taifa kwa watumishi wa umma.

Akifafanua lengo la utambuzi huo, Kairuki alisema lengo ni kuwa na mfumo mmoja wa taarifa sahihi za watumishi wa umma, ili kuondoa uwepo wa watumishi hewa, unaoigharimu serikali mabilioni ya fedha, ambazo zingetumika kufanya kazi nyingine za maendeleo.

“Tulikaa na NEC na NIDA, na tukaona tunaweza kuboresha mfumo wetu wa taarifa na tukaona tuchukue ile kanzi data ya NEC na tumeiingiza kwenye mfumo wa NIDA na kuangalia taarifa za watumishi wetu wa umma, na sasa tuna alama zao za vidole, tunahakikisha tuna taarifa zao sahihi hadi anuani yake,” alisema Kairuki.

Alisema kupitia mfumo huo wa utambuzi, watumishi wote wa umma wanaopaswa kupeleka taarifa zote muhimu kama vile hati ya malipo ya mshahara, cheti cha kuzaliwa, vyeti vya kitaaluma, kitambulisho cha kazi, kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi, hati ya kusafiria na kadi ya mpiga kura.

Kufuatia uhakiki huo, Kairuki alizitaka ofisi zote na taasisi za serikali zilizobainishwa kuwasiliana na NIDA ili kupanga mpango kazi wa kufanya shughuli hiyo na kuandaa ratiba itakayowawezesha watumishi wa umma kufanya usajili bila kuathiri utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, ofisi na taasisi hizo zimetakiwa kuandaa mazingira wezeshi ya kufanikisha kazi hiyo kwa kuandaa ofisi mahususi zitakazotumika kuendesha kazi hiyo na kuteua Ofisa Mwandamizi atakayeshirikiana na maofisa kutoka NIDA, na Ofisi ya Rais Utumishi katika kutekeleza hayo.

Pia taasisi na ofisi hizo zimetakiwa kuainisha magari na madereva kwa ajili ya kufanya kazi hiyo kwenye mamlaka ya serikali za mitaa na kwamba kwa ofisi ambazo makao makuu yake yako mkoani Dar es Salaam, watumishi wake watasajiliwa katika ofisi hizo.

Waziri Kairuki alisema kwa watumishi ambao wako katika ofisi za matawi mikoani watafanya usajili katika vituo vya usajili kwenye halmashauri zilizopo ofisi husika.

Akizungumzia hatua zitakazochukuliwa kwa watumishi watakaokaidi agizo hilo ndani ya muda uliopangwa, Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma , Dk Lauren Ndumbaro alisema hilo ni kosa na adhabu zake zimeainishwa kwenye kanuni za utumishi wa umma.

“Kwa wale watakaokaidi kutekeleza agizo hilo ndani ya muda uliowekwa, wanafahamu kwamba ni kosa kisheria na wanaweza kujifukuzisha kazi wenyewe,” alisema Dk Ndumbaro.

Hata hivyo alisema kabla ya hatua hizo hazijachukuliwa nafasi ya utetezi itatolewa kwa watumishi walioshindwa kutekeleza ndani ya muda uliopangwa, ili kubaini wenye sababu za msingi na kwa wale wasio na sababu za msingi, sheria itachukua mkondo wake.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mifumo ya Tehama wa NIDA, Muhammed Hamis, alisema baada ya usajili huo kufanywa kwa watumishi wa umma watapewa vitambulisho vyenye saini, tofauti na vile vya awali ambavyo havikuwa na saini.

“Lakini tumeanza kusajili Septemba 14, mwaka huu kwa wale ambao hawakuwa na vitambulisho vya taifa, ila waliokuwa navyo ila havina saini watapewa baada ya wale ambao hawakuwa navyo kabisa kupata,” alisema Hamis.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema serikali itachukua hatua kwa watumishi hewa waliobainika katika Mamlaka ya Usimazi wa Bandari (TPA), ambao wameambiwa na mwajiri kuacha kazi wenyewe. “Nimesikia taarifa hiyo, ila sisi serikali hatuwezi kuliacha, ni lazima hatua zichukuliwe,” alisema Waziri Kairuki.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link