Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Kamishna, Valentino Mlowola
Habari Leo
SIKU chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuahidi serikali kuangalia uwezekano wa kuishtaki Benki ya Standard ICBC ya Uingereza kuhusiana na ufisadi uliofanyika katika mkopo wa Dola za Marekani milioni 600 (Sh trilioni 1.2) ambazo serikali ilikopa kwa kutumia Hati Fungani, imebainika kuwa uchunguzi kuhusiana na suala hilo upo katika hatua za mwisho.
Benki hiyo inadaiwa kutoa hongo ya dola za Marekani milioni 6 (Sh bilioni 12) kama rushwa kwa maofisa wa serikali ili iweze kupata biashara hiyo nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa akizungumza na gazeti hili hivi karibuni alisema serikali itafanyia kazi maoni ya wadau mbalimbali wakiwemo wabunge wanaoshauri kushtakiwa kwa benki hiyo kutokana na kashfa hiyo.
“Sisi kama Serikali tutaifanyia kazi na pale tutakapoona tumefikia katika hatua ya kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na utekelezaji wa ushauri huo, tutafanya hivyo,” alisema Waziri Mkuu.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Kamishna Valentino Mlowola alisema taasisi hiyo inaendelea na uchunguzi huo ulio katika hatua za mwisho ikishirikiana na vyombo mbalimbali vya uchunguzi vya ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi huyo alisema uchunguzi huo utakapokamilika hivi karibuni, serikali itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuamua kuhusu benki hiyo kushtakiwa au kutoshtakiwa kuhusiana na suala hilo.
“Wakati wowote uchunguzi huu utakamilika na hivyo suala hilo litapatiwa ufumbuzi na taarifa rasmi itatolewa kwa wananchi ili wajue hatma ya fedha zao zilizochukuliwa isivyo halali katika suala hili,” alisema Mlowola.
Inadaiwa kuwa Machi 8, 2013 Serikali ya Tanzania ilikopa fedha dola za Marekani milioni 600 sawa na Sh trilioni 1.2 kutoka nje kwa msaada wa Benki ya Standard ya Uingereza ambayo sasa inaitwa Standard Bank ICIC Plc kwa kuweka Hati Fungani.
Mkopo huo wenye riba yenye kuweza kupanda ulianza kulipwa mwezi Machi mwaka huu na utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo 9 inayolingana.
Ifikapo mwaka 2020, Tanzania italipa deni hilo pamoja na riba jumla ya Dola za Marekani milioni 897 (karibu Sh trilioni 2), lakini hata hivyo wadau mbalimbali wakiwemo wabunge wanadai kuwa mkopo huo umegubikwa na ufisadi huku benki hiyo ikidaiwa kutoa hongo ya dola za Marekani milioni 6 (Sh bilioni 12) kama rushwa kwa maofisa wa serikali ili iweze kupata biashara hiyo.
Baada ya kuibuka kwa sakata hilo, Takukuru walitumia taarifa ya Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Uingereza (SFO) katika kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika sakata hilo. Hata hivyo inalalamikiwa kuwa SFO haikufanya uchunguzi dhidi ya Benki ya Uingereza ya Standard.
Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT- Wazalendo) alisema maslahi ya Tanzania katika sakata hilo yatakuwa makubwa endapo serikali itaweza kufanikiwa kuonesha kuwa Benki ya Standard ilihonga kupata biashara hiyo nchini.
Akitaja faida hizo Zitto alisema, “ moja, itakuwa ni fundisho kubwa kwa kampuni za kimataifa kwamba Afrika si mahala pa kuhonga na kupata kazi na kutoadhibiwa. Mbili, Tanzania haitalipa mkopo huu na riba zake. Tutakuwa tumeokoa zaidi ya Sh trilioni 2 katika Deni la Taifa na kuelekeza fedha tulizokuwa tulipe riba kwenda kwenye kuhudumia wananchi wetu kwenye afya na elimu,” alisema Zitto.