Home » » Ndege za ATCL kutua Septemba 19, 25

Ndege za ATCL kutua Septemba 19, 25

Written By CCMdijitali on Saturday, September 3, 2016 | September 03, 2016

Imeandikwa na Katuma Masamba | Habari Leo

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa
WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema ndege ya pili iliyoagizwa na Serikali itaingia Septemba 25, mwaka huu baada ya ndege ya kwanza kuingia, Septemba 19.

Aidha, alisema, wanafanya uchunguzi katika viwanja viwili vya ndege vya Dar es Salaam na Mwanza kama Rais John Magufuli alivyoagiza na pia watachunguza ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mbeya.

Profesa Mbarawa aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu ufafanuzi wa ndege hizo, na kueleza kuwa uamuzi wa serikali kununua ndege hizo, umezingatia hali halisi ya viwanja vya ndege vya nchini.

Alisema ndege hiyo itachukua wastani wa abiria 76 na ina uwezo wa kutua katika viwanja vyote nchini ambavyo vingi vina urefu wa kawaida.

Alisema viwanja vingi nchini vina urefu wa kilometa 1.5 hadi 1.6, lakini ndege hiyo ina uwezo wa kuruka kwenye uwanja wenye urefu wa kilometa 1.4 na kutua kwenye urefu wa kilometa 1.2.

Alisema, ndege hiyo itatumia saa 1:35 katika safari ya Dar es Salaam hadi Mwanza na itatumia kiasi kidogo cha mafuta ambayo ni tani 1.8 ikilinganishwa na ndege kubwa kama Airbus 319 inayosafiri umbali huo kwa saa 1:10 na kutumia mafuta tani 3.78.

Akizungumzia jinsi ndege hizo zitakavyochangia uchumi, Profesa Mbarawa alisema, ndege hizo zitakuwa chini ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na zitachangia uchumi kama shirika lingine lolote nchini na hivyo serikali itapata faida ya mapato pamoja na faida nyingine na pia zitafungua milango ya utalii kwa kiasi kikubwa kwani kutokuwepo kwa safari za uhakika katika mikoa mbalimbali zilikuwa zikiwafanya watalii washindwe kufika katika vivutio mbalimbali vya utalii.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link