Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino Prof Makame Mbarawa
Imeandikwa na Mwandishi Wetu | Habari Leo
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino Prof Makame Mbarawa ameteua wajumbe sita wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania.
Hatua hiyo inafuatia Rais Dk John Magufuli kumteua Luteni Kanali Mstaafu, Haroun Ramadhan Kondo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya ya Shirika la Posta Tanzania hivi karibuni.
Taarifa ya Katibu Mkuu Wizara hiyo anayeshughulikia Mawasiliano, Prof Faustine Kamuzora imesema Prof Mbarawa ametangaza uteuzi huo leo kwa mujibu wa sheria za shirika la Posta Tanzania No 19 ya mwaka 1993 kifungu cha 1(b) na uteuzi huo ulianza tangu Septemba 5 mwaka huu.
Wajumbe walioteuliwa kusaidiana na Luteni Kanali Mstaafu Kondo na watadumu katika nyadhifa hizo kwa kipindi cha miaka mitatu ni pamoja na Mhadhiri wa sheria za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) na Mkuu wa Idara ya Mafunzo Chuo Kikuu Mzumbe, Dk Ubena John, Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jasson Bagonza, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Benki ya TIB, Stella Nghambi.
Wajumbe wengine ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Inonovex, Leonard Kitoka, aliyekuwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Posta Tanzania, Zanzibar, Fatma Juma Bakari na Mratibu Mkazi wa Misaada ya Nje, Wizara ya Afya Zanzibar, Khadija Khamis Shaaban.