Home » » Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Mwinyi aongoza matembezi ya hisani ya “Walk for Kagera” Jijini Dar es Salaam

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Mwinyi aongoza matembezi ya hisani ya “Walk for Kagera” Jijini Dar es Salaam

Written By CCMdijitali on Saturday, September 17, 2016 | September 17, 2016

Na: Frank Shija, MAELEZO

TAKRIBANI shilingi bilioni 1.5 zimechangwa kufuatia matembezi ya hisani
yaliyopewa jina la “Walk for Kagera” yaliyofanyika leo Jijini Dar es
Salaam kwa lengo la kusaidia wahanga wa Tetemeko la Ardhi lililotokea
tarehe 10 septemba mwaka huu mjini Bukoba Mkoani Kagera.

Akizungumza mara baada ya matembezi hayo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe Ally
Hassan Mwinyi aliwashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza na kushiriki
matembezi hayo ya hisani.

“Nawapongeza sana wadau wote mlioshiriki katika matembezi haya, 
mmeonyesha  mshikamano mkubwa kwa umoja wenu mmeweza kuchangisha 
jumla ya  shilingi 1,502,680,000  hii inatia faraja sana muendelee na moyo huo” 
Alisema Mzee Mwinyi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amewahakikishia
wananchi wa Mkoa wa Kagera kuwa Serikali inafanya kila liwezekanalo
kuhakikisha wahanga wa tetemeko hilo wanapatiwa huduma stahiki na kwa
wakati.

Balozi Kijazi aliongeza kuwa kutokana na kuguswa na tatizo hilo Serikali pamoja na 
Taasisi zake imetoa msaada wake ambao unakadiriwa kuwa zaidi ya shilingi bilioni moja 
ikiwa ni kuthamini utu wa wahanga.

“Najua kuna athari kubwa imetokea kutokana na
tetemeko hili, sisi kama Serikali tunafanya kila jitihada kuhakikisha
wahanga wote wanapata misaada na kurejesha huduma zote katika hali yake”
Alisema Balozi Kijazi.

Awali akisoma maelezo ya tathmini ya
athari za tetemeko hilo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu –
Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Abdallah Posi
amesema kuwa hadi kufikia tarehe 16 idadi ya vifo ni 17, nyumba
zilizoanguka zimefikia 840 huku zilizoharibika zikiwa ni 1264 na majengo
44 mali ya Taasisi za umma yameharibika.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mabalozi nchi, Balozi wa Zimbabwe ametoa pole kwa 
wahanga wa tukio hilo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania 
pale panapo hitaji msaada wao.

Matembezi hayo ya hisani kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia wahanga wa 
tetemeko la Ardhi yaliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa 
Afrika Mashariki ,Ofisi ya Waziri Mkuu na Ikulu.


 Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ally Hassan Mwinyi akishiriki Matembezi ya Hisani kwa ajili ya kuchangia wahanga wa Tetemeko Mkoani Kagera “Walk For Kagera” leo Jijini Dar es Salaam. Katika matembezi hayo kiasi cha shilingi 1,502,680,000/= kimepatikana. 

 Baadhi ya washiriki wa  hafla ya kuchangia wahanga wa Tetemeko lililotokea mkoani Kagera  iliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na Ikulu wakifuatilia mtukio katika hafla hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilitanguliwa na Matembezi ya Hisani ambapo kiasi cha shilingi 1,502,680,000/= zilipatikana. 


 Wawakilishi wa Jumuiya ya Wabohora nchini  wakimkabidhi Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ally Hassan Mwinyi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni kumi kwa ajili ya kuchangia wahanga wa Tetemeko Mkoani Kagera kwa Rasi wakati wa Matembezi ya hisani yalioyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF Bw. William Erio na Afisa Uhusiano wa PPF, Lulu Mengele wakimkabidhi Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ally Hassan Mwinyi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni kumi kwa ajili ya kusaidia wahanga wa Tetemeko Mkoani Kagera wakati wa Matembezi ya hisani yalioyofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Wapili kutoka kushoto ni Waziri wa Mmbo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Agustine Mahiga.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ally Hassan Mwinyi akimkabidhi cheti cha utambuzi wa mchango wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashari katika kufanikisha Matembezi ya hisani ya “ Walk for Kagera” Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB Ineke Busemaker akipokea cheti kwa ajili ya kutambua udhamini wa Benki hiyo katika kufanyikisha matembezi ya hisani kwa ajili ya kuchangia wahanga wa Tetemeko la Kagera leo Jijini Dar es Salaam.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link