Imeandikwa na Fadhili Abdallah, Kigoma | Habari Leo
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji wa umeme nchini yataifikisha nchi kwenye uchumi wa kati kwa kuwa itakuwa ni ya viwanda.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku tano mkoani Kigoma, akiwa na viongozi wa Serikali na taasisi za Serikali zilizo chini ya wizara yake, Muhongo alisema kwa sasa uhakika wa kuwa na umeme wa uhakika kutokana na gesi asilia upo.
Alisema miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa nchini ni kielelezo kwamba dhamira ya Serikali kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati inatekelezeka. Aliwataka wananchi wajiandae kutumia fursa zitakazotokana na kuwepo kwa viwanda vingi nchini.
Akielezea hilo, Profesa Muhongo alisema tayari tafiti zimeonesha gesi asilia iliyopo Ruvu mkoani Pwani ina uwezo wa kuzalisha megawati 10,000, umeme ambao pamoja na matumizi ya nchi, unaweza kuuzwa nje na kuliingizia taifa fedha za kigeni.
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, alisema Serikali imeridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kwamba kazi kubwa ya kusafirisha umeme kwenda maeneo mbalimbali ya vijijini imekamilika.
"Natoa wito kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge na madiwani kuwahamasisha wananchi kutumia fursa hii kuunganisha umeme kwenye maeneo yao," alisema Profesa Muhongo.