Home » » Mgunduzi kutoka Veta kuileta dunia Tanzania

Mgunduzi kutoka Veta kuileta dunia Tanzania

Written By CCMdijitali on Wednesday, September 28, 2016 | September 28, 2016

Mgunduzi wa kifaa kipya cha mitaala ya elimu ya anga, mfumo wa jua na sayari zake, Ernest Maranya akitoa maelezo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamiseni), Selemani Jafo, juu ya namna kifaa hicho kinavyofanya kazi.

Imeandikwa na Sifa Lubasi| Habari Leo


INGAWA ni kiziwi, Ernest Maranya (36), mkazi wa Dar es Salaam, ana kila sababu ya kuifanya dunia kuelekeza macho na masikio yao Tanzania kutokana na kugundua kifaa kipya cha kufundishia elimu ya anga, mfumo wa jua na sayari zake, huku akitoa makosa kwenye ugunduzi uliofanywa na wakongwe wa sayansi kama Newton.

Kwa ubunifu huo, sasa anaweza kufaidi matunda ya kazi yake mara tu kifaa hicho kitakapoanza kutumika shuleni na pengine wanasayansi wakaja kujifunza kitu Tanzania. Kifaa hicho cha kimaabara kwa ajili ya kufundishia kinatoa taarifa mpya zinazohusu mfumo wa jua baada ya kukifanyia utafiti kwa zaidi ya miaka 10. Kwa upande wake, serikali inasema kifaa hicho kitafungwa katika shule kadhaa za sekondari kwa kuanzia na shule 20 huku ikielekeza wahusika ‘kulinda’ haki miliki ya ugunduzi huo wa kijana wa Kitanzania.

“Tangu nimegundua kifaa hiki, naweza kusema sijapata manufaa kama ilivyotarajiwa, lakini sasa nashukuru kuona kuwa kilio changu kimesikika, nina matumaini makubwa kwamba sasa nitafaidika na ugunduzi huu,” anasema Maranya.

Anasema kwa sasa anafundisha katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) jijini Dar es Salaam kama msaidizi wa mwalimu. Anasema taarifa alizonazo ni kwamba endapo serikali itaanza kununua vifaa hivyo kwa ajili ya kufundishia shuleni anaweza akawa anaiuzia serikali seti moja kwa Sh 600,000 na bei hiyo inaweza kupungua.

Elimu ya anga na tabia za sumaku

Anasema elimu ya anga imegawanyika katika madaraja ambayo yanahusu nishati ya mvutano kati ya jua na sayari inayoliwezesha jua kuzishikilia sayari angani na kuziwezesha kulizunguka jua. Anasema uvumbuzi wake hauna uhusiano kwa namna yoyote na nishati ambayo inaliwezesha jua na nyota kuwaka na kutoa joto na mwanga.

Anasema msingi wa ugunduzi wake ni matokeo ya kugunduliwa kwa kanuni au tabia mpya ya tatu ya usumaku, na kwamba tabia hiyo ya tatu ya usumaku ni matokeo ya kuunganishwa kwa kanuni au tabia kuu mbili za sumaku. Anafafanua kwamba ncha mbili mfanano za sumaku husukumana na ncha tofauti za sumaku huvutana.

Anasema matokeo ya kuunganishwa kwa kanuni hizo kuu mbili za sumaku hufanya masharti ya sumaku kubadilika kuwa nishati ya mvutano mithili ya mifumo ya jua. Anasema ugunduzi huo unaleta taarifa mpya za kisayansi kwamba asili ya nishati hiyo ya mvutano katika anga, kikanuni inatokana na muunganiko wa kanuni au sheria kuu mbili za sumaku (the nature of the universe gravitational potential energy is magnetic two laws combination).

“Hii ni kinyume na ilivyoelezwa na mwanasayansi Isaac Newton kwamba asili ya nishati hiyo ni uzito. (Universe gravitational potential energy is mass). “Kutokana na kugundua msingi huu wa muunganiko wa sheria hizo mbili za sumaku uliniwezesha kutumia sumaku za kawaida kubuni nyenzo hii sambamba na nishati ya mvutano katika anga, mahususi kwa matumizi ya kimaabara mashuleni katika shule za msingi na sekondari,” anasema Maranya.

Anasema kifaa hicho alichokiita kwa jina la Kiingereza: A Teaching Aid Kit for Outer Space bodies ad/or Atomic part, kimelenga kuwa nyenzo ya majaribio ya awali ya kisayansi ili kusaidia zaidi utafiti wa mambo ya anga. Hii ni kwa sababu anasema kifaa hicho kinawezesha kuhakiki, mienendo tabia, matokeo na mahesabu ya utendaji wa vitu vyote vya anga kama vile vimondo, sayari, mwezi, nyota, sumaku za asili na zisizo za asili na tabia za nishati. Tofauti ya teknolojia yake na zilizopita.

Akizungumzia uhusiano na utofauti na vifaa au teknolojia zilizopita anasema vifaa mbalimbali vimetengenezwa ili kuhakiki namna ya mfumo wa jua na chembe za atomiki zinavyotenda kazi.

“Kwa bahati mbaya vifaa hivi hukosa sifa stahiki za mahusiano na tabia za utendaji wa mfumo wa jua au chembe za atomiki asilia kwa kuwa mara nyingi vifaa hivyo hujaribu kutumia njia za kimakenika kama matufe ya plastiki au shaba yaliyoshikiliwa kwa mifumo ya gia au vishikizo kama vile kamba na mpini na kuzungushwa kwa msaada wa mota za umeme,” anasema.

Anasema tofauti iliyopo kati ya teknolojia hizo na ugunduzi wake mpya ni kwamba vifaa hivyo havina uwezo wa kusanifu nguvu halisi ya mvutano ya mfumo wa jua katika anga inayotumiwa na mifumo halisi ya jua, nyota, sayari, vimondo, mwezi na mifumo ya chembe za atomiki.

“Kifaa hiki ndicho pekee chenye ufanisi wa asilimia 100 kwa kusanifu nguvu hiyo chenyewe kwa kutumia nguvu za sumaku pasipo kuhusisha umeme au nishati zingine. Hii ni kwa sababu, kiasilia na kisayansi, jua, sayari na nyota na chembe za atomiki ni sumaku,” anafafanua. Anasema ugunduzi huo pia unalenga kusaidia kubainisha na kusahihisha mapungufu ya baadhi ya taarifa za kisayansi zinazohusu mitaala ya elimu hiyo ya sayansi ya mfumo wa jua.

Anasema katika sayansi inayorasimishwa katika mitaala iliyopo, nadharia nyingi zimekuwa zikifundishwa kimakosa na mara nyingi hutolewa maelezo au majibu ya ubashiri tu pasipo uhakiki wa kimaabara.

“Ni vigumu kuthibitisha kwa sayansi iliyopo katika mitaala ya elimu kuhusu hisabati halisi ya kujipindua kwa mhimili wa dunia ili kuleta majira ya mwaka katika uso wa dunia kutokana na sayansi ya mitaala inafafanua na kutoa majibu ya kiimla tu. “Chanzo cha kujibetua (tilt) kwa mhimili wa dunia (axis) na kuleta majira ya mwaka ni mzunguko wa sayari kulizunguka jua yaani katika muda wa siku 365.24.

Anasema kimsingi matokeo haya ya kujibetua kwa mhimili wa dunia ndiyo elimu ya fizikia na wanasayansi walipaswa kuhakiki hisabati zake ili kubeba wazi chanzo halisi cha kujibetua kwa mhimili wa dunia na sio kutoa maelezo ya kiimla kuwa chanzo ni mzunguko (revolution), kwa sababu mbalimbali. Sababu mojawapo anasema ingewezekana kuwepo kwa majira ya mwaka katika uso wa dunia pasipo kuwepo kwa mzunguko wa dunia (revolution) endapo tu muhimili wa dunia utaweza kubadili vipimo vya egemeo lake la mtazamo wa jua.

“Pia pasingewezekana kuwepo kwa majira ya mwaka katika uso wa dunia endapo nishati ya usumaku wa jua lote, ungekuwa wa daraja moja tu la nishati hivyo uwepo wa mzunguko usingeweza kusaidia kubadili vipimo vya muhimili wa dunia bali muhimili huo ungebaki katika egemeo moja tu la nyuzi 23.5,” anasema.

Serikali kuanzia kutumia kifaa hicho

Akizungumza hivi karibuni wakati wa jopo la wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), walipokutana na mgunduzi huyo na kuona namna ya kifaa hicho kinavyofanya kazi, Naibu Waziri Tamisemi, Selemani Jafo anasema serikali itaanza kukitumia mashuleni kifaa hicho kilichobuniwa na Maranya.

Ametoa maagizo kwa wataalamu wa wizara yake na wale wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kifaa hicho kinaanza kutumika shuleni pamoja na kumpatia mhusika hati miliki. Anasema wanaweza kuanza kwa kufunga kifaa hicho kwenye shule kongwe. Anawataka wataaluma wa Wizara ya Elimu na Tamisemi walinde ugunduzi huo kwani unaweza kuchukuliwa na wazungu na kuufanyia ukarabati kisha wakadai wamegundua wao.

“Angalau tuanze na shule 20 ili wanafunzi wafanye masomo kwa vitendo… Jambo hili ni kubwa sana hivyo ni wajibu wa wataalamu kuona ndani ya miaka mitano kitu kikubwa kikifanyika kutokana na ugunduzi huu,” anasema.

Tanzania kuna vipaji lukuki

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (Veta) kanda ya kati, Ramadhani Mataka anasema Tanzania ina vipaji vingi lakini vinashindwa kuendelezwa kutokana na mfumo wa elimu uliopo nchini.

Kwa upande wake, Dk Jane Namseda ambaye ni mtaalamu wa lugha, Ofisi ya Rais Tamisemi, anasema mgunduzi huyo amekuja na kitu kizuri hajakipika wala hajaota ndoto na kwamba kinatokana na utafiti mmoja unaofuatia utafiti mwingine. “Hiki ni kitu kikubwa sana nina PhD, lakini sijagundua kitu kama hiki lakini mtu aliyeishia kidato cha nne anagundua mambo makubwa kama haya. Tusipofanya kitu cha kutangaza uvumbuzi wa Tanzania duniani Mungu atatuona,” anasema.

Mtaalamu wa Idara ya Elimu kutoka Tamisemi, Benjamin Oganga anasema kupingana katika utafiti sio dhambi na ndicho kitu kinachotakiwa kufanyika na kwamba ugunduzi huo umehakikiwa na kuthibitishwa na japo la wataalamu kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za utafiti kupitia Wizara ya Sayansi na Teknolojia Chini ya uratibu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na kusajiliwa na Wizara ya Viwanda, Biashara kwa hati namba TZ/P/14/00372.

Historia ya Maranya

Akizungumzia historia yake, Maranya anasema: “Nilizaliwa mwaka 1980 mkoani Mara na kukulia Jijini Dar es Salaam. Makuzi yangu ya utotoni hayakuwa na malezi maalumu. Nilipitia malezi ya kuhamahama kwa kupitia mazingira magumu ikiwemo kutumikishwa katika mifugo na kazi ngumu,” anasema. Anasema hali hiyo iliathiri maendeleo yake kielimu na kuwa chanzo cha ulemavu wake wa masikio.

Mwaka 1992 alijiunga na elimu ya msingi na kuhitimu mwaka 1998 katika Shule ya Msingi Ukonga na baadaye, mwaka 1999 alijiunga na shule ya sekondari na kuhitimu mwaka 2002 katika shule ya sekondari ya Benjamin Mkapa. “Matokeo yangu ya kidato cha nne hayakuwa mazuri na ndipo nikajiunga na elimu ya ufundi (Veta ) mwaka 2004. Hiyo ilikuwa ni baada ya Veta kugundua kipaji changu cha ugunduzi na kunichukua kwa nia ya kuniendeleza zaidi kielimu,” anasema.

Kadhalika, anasema Veta walimfadhili kwa masomo ambapo alisomea kozi ya Welding and Metal Fabrication katika mafunzo aliyoanza 2004 hadi 2005 na kutunukiwa cheti. Mwaka 2006 alipewa ufadhili na mamlaka ya Veta kupitia chuo cha Chang’ombe ili kuendeleza utafiti wa pampu ya maji, utafiti ulikamilika mwaka 2007 ukiwa na matokeo makubwa hali iliyomwezesha kutambuliwa ngazi ya taifa kuwa mwanasayansi, mtafiti na mvumbuzi wa sayansi na teknolojia.

Anasema mwaka 2008 alitunukiwa tuzo ya taifa ya sayansi na teknolojia (Tasta Award 2008) na kwamba tangu wakati huo amefanya tafiti mbalimbali akishirikiana na mamlaka ya Veta zilizoleta matokeo chanya. Miongoni mwa tafiti hizo ni ugunduzi wa kifaa hicho kipya cha elimu ya anga, mfumo wa jua na sayari zake.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link