MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amemtaka Katibu Tawala wa mkoa huo, Richard Kwitega kufuatilia aliyetoa taarifa ya uongo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa wa Arusha kuhusu Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kutokuwa na upungufu wa madawati kabisa.
Alitoa agizo hilo baada ya taarifa iliyokuwa ikitolewa na Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Arusha, Nestory Mroka kumshangaza yeye na baadhi ya wajumbe wa kikao hicho kutoka wilayani Ngorongoro wakiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Mfaume Taka na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mathew Siloma.
Alisema alifanya ziara Ngorongoro na kujionea hali halisi ya upungufu wa madawati na kutoa maagizo kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuhakikisha inakamilisha ahadi ya kuchangia madawati 2,000.
“Hizi taarifa umezipata wapi na kwa nini useme Ngorongoro haina uhaba wa madawati wakati nimefanya ziara mwenyewe na kujionea hali halisi, naomba RAS (Katibu Tawala) ufuatilie hii taarifa ya madawati ili kujua ni nani ameitoa nichukue hatua stahiki … naomba ufuatilie hii taarifa ili kubaini ni nani ameileta hapa kwa sababu ni ya uongo…Ngorongoro ina upungufu wa madawati na nyie mnasema hakuna, hapana hii taarifa inadanganya,” alisema.
Mashaka ya Gambo dhidi ya taarifa hiyo yaliungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro aliyesema wilaya yake ina upungufu mkubwa wa madawati na baadhi ya wanafunzi wanakaa chini, hivyo hafahamu ni kwa nini taarifa hiyo inasomwa kuwa hakuna upungufu wa madawati.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Siloma alisema hadi hivi sasa NCAA imetoa madawati 500 tu kati ya yaliyoahidiwa.
Imeandikwa na Veronica Mheta, Arusha | Habari Leo