Home » » Butiku apongeza serikali ya JPM

Butiku apongeza serikali ya JPM

Written By CCMdijitali on Saturday, October 22, 2016 | October 22, 2016

MWENYEKITI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku
 
MWENYEKITI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amepongeza ukaguzi wa vyeti pamoja na mfumo wa uchumi, unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli.

Alisema kuwa ni hatua nzuri ya kurejesha nidhamu na maendeleo ya nchi na kuwataka wananchi kumuunga mkono na sio kulalamika.

Butiku alisema hayo juzi kwenye mazungumzo maalumu na gazeti hili, ambapo alisema kuwa kinachoendelea kwa sasa ni utekelezaji wa sheria na kanuni ambazo awali zilichezewa.

Alisema kushindwa kufuatwa kwa taratibu kulitengeneza mianya mbalimbali kwa wananchi kujiamulia mambo yao, huku wengine wakiichezea elimu ambayo ndio msingi wa taifa.

Butiku alionesha kukerwa zaidi na utitiri wa vyeti vya kufoji, uliokuwa umekithiri serikalini na kuipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kukabiliana na hali hiyo sasa, kwa kufanya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma.

Alisema kuwa inashangaza kuona kuwa kuna watu walikuwa wamefikia hadi hatua ya kuwa na vyeti vya juu vya Shahada ya Uzamili (Masters) na Uzamivu (PHD), lakini vya kidato cha nne hawana.

“Kile kinachoendelea kwa sasa ni utekelezaji wa ahadi ya kurejesha mifumo ya nidhamu kwenye serikali, sasa kinachotakiwa ni kuunga mkono kwa kuhakikisha kuwa malengo ya Rais yanatimia kwa sasa,” alisema Butiku.

Alisema anashangazwa kwa uwepo wa wanafunzi hewa katika ngazi ya vyuo na hasa vyuo vikuu, kwa kusema kuwa hiyo ni ishara ya ukosefu wa umakini katika elimu.

“Mimi nikitoa mfano wa miaka yetu wakati tunasoma, ni matokeo yetu mazuri tu ndio yaliyokuwa yakitubeba na kuendelea zaidi ngazi za juu hadi mimi ninafikia kusoma Chuo Kikuu cha Makerere Uganda ni matokeo mazuri tu, lakini kuna muda hapa nchini ilikuwa fedha inaweza kukubeba,” alisema Butiku.

Butiku ambaye aliwahi kuwa Msaidizi wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, aligusia kuhusu mfumo wa sasa wa kiuchumi, ambapo alimpongeza Rais Magufuli kwa kurejesha fedha katika mfumo unaostahili.

Alisema kuwa ili uchumi uweze kusonga mbele ni dhahiri kuwa lazima fedha ziende kwa wazalishaji, akiwa na maana ya watu ambao wanazizungusha na kuendesha maendeleo.

Butiku alisema kuwa kwa sasa kinachofanyika ni fedha kurejea kwenye matumizi stahiki na yenye tija kwa nchi nzima, huku akiwalaumu wale wanaolalamika kuwa walikuwa wamezoea aina ya maisha ya matumizi na kwa sasa wanakabwa na upangwaji wa bajeti.

Alisema hatua aliyochukua Rais Magufuli ni kuonesha umakini, hasa anapokabiliana na vitendo vya uovu hasa rushwa na ubadhirifu na kuwa hiyo inasaidia kurejesha heshima ya kimamlaka. Butiku alimtaka kutumia fedha zaidi katika kuimarisha mifumo ya elimu na hasa kuwasomesha vizuri vijana ili watumie elimu yao kwa tija ya taifa.

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuwa ikishughulikia kwa kina suala la elimu kwa kuendesha misako ya kubaini watumishi hewa serikalini, pamoja na kukabiliana na matumizi mabaya ya fedha, ambapo ni pamoja na kuzuia matumizi yasiyokuwa ya lazima hasa kwa watendaji wa serikali.


 Imeandikwa na Evance Ng’ingo   | Habari Leo

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link