Wa kwanza kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mheshimiwa Mwanajuma Majid Abdullah.
Haiba ya muonekano wa Majengo ya Mapya ya Hospitali ya Abdulla Mzee yanavyopendeza yakiwa katika hatua za mwisho kumalizika kwake.
Picha na –OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Mradi Mkubwa wa ujenzi wa Hospitali ya rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo
Mkoani Kisiwani Pemba tayari umeshaweka alama ya Kihistoria
itakayoendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya
Jamuhuri ya Watu wa China na Zanzibar ambao
una zaidi ya miaka 52 sasa.
Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Nchini Tanzania Bwana Lu Youqing
alisema hayo wakati akipokea salamu za shukrani kutoka Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar zilizowasilishwa kwake na Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Nyumbani kwake Mtaa wa Namanga
Barabara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam.
Balozi Lu alisema Serikali ya nchi yake kwa makusudi imeamua kufanya
ushirikiano wa kina na wa ndani kati yake na Zanzibar kutokana na
Viongozi Wakuu wa pande hizo mbili kuasisi mafungano hayo yenye kuleta
faraja na upendo baina ya wananchi wa sehemu hizo mbili.
Alisema upo ushahidi wa wazi unaothibitisha ushirikiano wa pande hizo
mbili ukijikita zaidi katika uanzishwaji wa miradi ya maendeleo ya
kiuchumi na ustawi wa jamii Visiwani Zanzibar na kuungwa mkono wa
kiuwezeshaji na ndugu zao hao nwa Jamuhuri ya Watu wa China.
Balozi Lu Youqing alielezea faraja yake kutokana na mabadiliko makubwa
ya teknolojia ya Kisasa yanayoendelea kupamba moto ndani ya Visiwa vya
Zanzibar jambo ambalo hukleta matumaini kwa Wananchi wake hawa Vijana.
Akizungumzia utanuzi wa eneo la maegesho ya ndege katika Uwanja wa
ndege wa Kimataifa wa Zanzibar {Terminal 2 } Balozi wa Jamuhuri ya
Watu wa China Bwana Lu Youqing alisema hakuna matatizo yoyote katika
uendelezaji wa mradi huo kwa Vile Benki ya Kimataifa ya Exim
imeshapata njia ya kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha wa mradi huo.
Balozi Lu Youqin kilichochelewesha kuendelea kukamilika kwa mradi huo
ni mabadiliko yaliyotokea ya Uongozi wa Benki ya Exim yaliyokwenda
sambamba na mabadiliko mengine ya Uongozi wa Wizara ya Fedha na
Mipango ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndio mratibu wa
mradi huo wa Kimataifa.
Bwana Lu Youqing alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China utatoa kipaumbele ombi la
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la ujenzi wa Nyumba za Madaktari
katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee Mkoani.
Alisema kipaumbele hicho kitaingizwa katika mipango inayokusudiwa
kutekelezwa na China katika kipindi cha mwaka ujao kupitia mpango wake
wa kuunga mkono mataifa ya Bara la Afrika.
Mapema akitoa ashukrani kwa niaba ya Serikali ya Ma9induzi ya
Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alieleza kwamba kazi inayofuatia kwa sasa na kutafuta mbinu za ujenzi
wa nyumba za Madaktari katika Hos9itali ya Abdulla Mzee.
Balozi Seif Alisema kazi hiyo itakwenda sambamba na Serikali
kujitahidi kutafuta madaktari mabingwa watakaoweza kutoa huduma za
afya kulingana na mahitaji halisi ya wagonjwa ndani ya Kisiwa cha
Pemba pamoja na maeneo jirani yaliyokizunguka kisiwa hicho.
Makamu wa ili wa Rais wa Zanzibar ameelezea faraja yake kutoka na
hatua kubwa na ya mwisho ilizofikiwa na wahandisi wa ujenzi wa
Hospitali hiyo itakayokuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi walio wengi.
Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani imejengwa katika mfumo wa teknolojia
ya kisasa utakaokuwa na uwezo wa kutoa huduma mbali mbali ikiwemo zile
za upasuaji mkubwa, uchunguzi wa maradhi mbali mbali itaweza kukidhi
mahitaji ya huduma za Kiafya kwa wancchi walio wengi ndani ya Visiwa
vya Zanzibar pamoja na ukanda wa mwambao wa Tanzania.
Wagonjwa wapatao 130 wanaweza kulazwa kwa wakati mmoja kwenye
Hospitali hiyo zikiwemo huduma zote muhimu kama vyumba Vitatu vya
upasuaji, chumba cha wagonjwa mahututi { ICU }, Wodi ya wazazi pamoja
na jengo la msikiti litakalotumiwa na wagonjwa pamoja na familia zao
kwa ajili ya inbada.
Balozi Seif alitumia mazungumzo hayo kuishukuru pia Serikali ya
Jamuhuri ya Watu wa China kwa kukubali kugharamia ujenzi wa uwanja wa
michezo wa Mao Tse Tung uliopo Mperani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema ujenzi wa uwanja huo utasaidia kurejesha hadhi ya jina la
Kiongozi na muasisi wa Taifa hilo lilioko katika Bara la Asia.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
21/10/2016.