Aliyekuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Bi. Mwanahija Almas Ali amesema hatosahau ushirikiano alioupata kutoka kwa wafanyakazi wa Shirika hilo katika kipindi chake cha uongozi wa Shirika hilo kwa vile ulimpa urahisi wa kuliendesha Shirika hilo kwa mafanikio.
Aliyasema hayo katika hafla ya kuagwa rasmi iliyoandaliwa na wafanyakazi wa ZSTC katika ukumbi wa Eneo Tengefu Saateni, Zanzibar.
Bi. Mwanahija alisema katika uongozi wake mambo mengi yaliwezakanana kufanikiwa kutokana na kuwepo kwa mashirikiano ya dhati baina yake, Bodi ya Wakurugenzi, Wafanyakazi wa Shirika pamoja na wadau wa Sekta ya karafuu.
“Nakushukuruni sana kwa mashirikiano mlonipa wakati nilipokuwa naliongoza Shirika hili na naona ufahari leo hii tukiagana kwa amani na upendo,” alisema Bi. Mwnahija.
Aidha Bi. Mwanahija aliwaomba wafanyakazi hao wa Shirikala la ZSTC kuendeleza mashirikiano hayo kwa Mkurugenzi mpya Dk. Said Seif Mzee ili Shirika liendelee kupata mafanikio zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la ZSTC, Maalim Kassim Suleiman alisema Sekta ya Karafuu haiwezi kumsahau Bi. Mwanahija kutokana na jitihada zake kubwa alizofanya katika kuendelza zao la karafuu.
Alimuelezea Bi. Mwanahija kuwa ni kiongozi mzalendo aliyeweza kutekeleza majukumu yake vyema kwa misingi ya uadilifu na kauli mbiu za viongozi wa kitaifa za ‘kutokufanya kazi kwa mazoea’ na ‘Hapa kazi tu’ wakati akiwa ZSTC.
“Tunaahidi yale yote mazuri uliyotuachia tutayaendeleza, tukikwama tutakuja kuomba ushauri kwako na wala usichoke kutusaidia," alisema Maalim Kassim alisema.
Alielezea imani yake kwa Mkurugenzi mpya wa Shirika hilo Dk. Said kuwa anaweza kuvaa viatu vyake vya uongozi wa Shirika hilo.
Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC Dk. Said Seif Mzee amempongeza Bi. Mwanahija kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika kipindi chake cha uongozi katika kuhakikisha Shirika la ZSTC linakwenda mbele na kuwa na faida kwa wananchi na Taifa.
Akisoma risala ya wafanyakazi, Mkurugenzi Masoko wa ZSTC Salum Abdalla Kibe alisema Shirika linatambua mchango mkubwa alioutoa Bi. Mwanahija na kutoa wito kwa wafanyakazi kuenzi mafanikio yaliyopatikana katika kupindi hicho.
Alisema katika kipindi kifupi cha miaka minne (Septemba 2012 hadi Juni 2016) mafanikio mengi yamepatikana hivyo wafanyakazi hawana budi kushukuru na kuufanyia kazi mchango wake.
Aliyataja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu, kustaafishwa kwa baadhi ya wafanyazi na kulipwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria ambapo ilikuwa ni utekelezaji wa mageuzi ya Shirika.
Aliyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na Shirika kujiendesha kwa faida pamoja na kulipa kodi zote za Serikali, kuimarisha vitendea kazi na kujengwa vituo vya kisasa vya ununuzi wa karafuu.
Aliongeza katika kipindi hicho Shirika lilipata ithibati ya kuzalisha bidhaa za Kilimo Hai kutoka Tancert na ubora wa bidhaa kutoka TBS.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC Bi. Mwanahija Alimas Ali (kulia) akipokea cheti cha Shukurani kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo Maalim Kassim Suleiman (kushoto) Mkurugenzi Mpya Dr. Said Seif Mzee (katikati) akishuhudia.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC Bi. Mwanahija Alimas Ali akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Shirika la ZSTC.