JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
OFISI YA MKUU WA MKOA ARUSHA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo amekamilisha ziara yake ya kikazi ya SIKU TANO mfululizo aliyoifanya katika Wilaya ya Ngorongoro yenye lengo la kujitambulisha kwa wananchi wake, kufahamu changamoto na fursa zilizopo pamoja na kukagua miradi ya Maendeleo.
Katika ziara hiyo iliyokua na mafanikio makubwa Mhe. Gambo alitembelea Tarafa zote tatu ambazoni Sale, Loliondo na Ngorongoro kwenye Kata za Ngarasero, Pinyinyi, Oldonyosambu, Digodigo, Samunge, Olorien, Soitsambu, Ololosokwani, Piyaya, Nainokanoka pamoja na Kata ya Endulen. Pia alifanya mikutano ya hadhara kwenye kila kata ili kusikiliza kero za wananchi.
Aidha kupitia ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliweza kukutana na wafanyakazi wa Taasisi za Serikali zinazotoa huduma katika Wilaya ya Ngorongoro, Makapuni ya Utalii yaliyowekeza katika Wilaya hiyo, Baraza la wafugaji, taasisi binafsi pamoja na wafanyakazi wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.
Kupitia ziara hiyo ya kazi Mkuu wa Mkoa Mhe. Gambo alibaini na kutoa maelekezo katika maeneo yafuatayo:
- Ugonjwa wa ajabu wa kutapika damu kwa wakazi wa Kata ya Pinyinyi uliosababisha vifo vya watu 21, ambapo Mkuu wa Mkoa alimuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuleta wataalam kufanya tafiti na kupata ufumbuzi wa tatizo hilo na mpaka ziara inamalizika wataalamu toka Wizara ya Afya na Taasisi ya Utafiti ya magonjwa ya binadamu (NIMR) walikua wameshafika kwenye kata hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa maagizo hayo. Pia alimuagiza Mkurugenzi kuboresha Zahanati ya Kata hiyo iliyopo mpakani mwa Kenya na Tanzania yenye umbali wa zaidi ya Km 120 kutoka makao makuu ya Wilaya.
- Kutokuwa na mawasiliano ya mitandao ya Simu katika Tarafa ya Sale na baadhi ya Kata za Ngorongoro; ambapo Mkuu wa Mkoa ameahidi kukutana na makampuni ya Simu hasa yale yaliyoelekezwa kufikisha huduma za simu maeneo ya vijijini ili waweze kufikisha huduma hiyo maramoja.
- Matumizi mabaya ya Fedha za Umma; Kutokana na hili Mhe. Gambo aliwasimamisha kazi watumishi watatu wa Halmashauri ya Ngorongoro kwa tuhuma za ubadhifu wa fedha za uchaguzi pamoja na miradi mingine ya maendeleo yenye thamani zaidi ya Tsh 500 milioni. Watumishi hao ambao ni Mwekahazina Bw. Evans Mwalukasa, Mwanasheria Bw. Sembeli Siloma pamoja na Afisa Uchaguzi Bi. Hadija Mkumbwa. Sambamba na hilo Mhe. Gambo amezuia watendaji wa kata kuhudhuria vikao vya Baraza la madiwani kwa kuwa si wajumbe halali wa Kikao hicho na ambapo hadi sasa wamesababishia Halimashauri hasara ya Tsh 132 milioni. Aidha amemuagiza katibu Tawala Mkoa wa Arusha kumuandikia Katibu Mkuu Tamisemi ili awarudishe aliyekuwa Mkurugenzi wa Halimashauri ya Ngorongoro Bw. John Kulwa Mgalula na Afisa Mipango Bw. Louis Chambi pamoja na Mhandisi Eng. Maziku kuja kujibu tuhuma zinazowakabili. Rc Gambo amechukua hatua hizo mara baada ya kupokea taarifa ya kamati aliyoiunda kabla ya ziara hiyo.
- Madeni ya Walimu; Mkuu wa Mkoa aliagiza Halmashauri kulipa madeni ya walimu kwa kutuimia fedha za ndani ili kupunguza madeni yao. Aidha Rc Gambo alishangazwa kuona Halimashauri inadaiwa Million Tatu na laki Nane na walimu wa Sekondari Wilayani Ngorongoro na Halimashauri kusema inasubiri fedha kutoka Serikali Kuu. Alimuelekeza Mkurugenzi Mtendaji kulipa mara moja kwa kuwa hicho kiasi ni kidogo.
- Usafiri wa Madiwani; Mkuu wa Mkoa alitoa maagizo ya kusitishwa mara moja utaratibu wa Halimashauri kutuma gari za Serikali kumfuata kila Diwani nyumbani kwake maana taratibu hazisemi hivyo. Badala yake Mkurugenzi afanye jambo hilo kwa kufuata Sheria na Taratibu. Pia alimuelekeza Mwenyekiti wa Halimashauri hiyo kutumia gari ya Serikali mara mbili kwa wiki kama taratibu zinavyotaka. Aidha, fedha zitakazookolewa kwa utaratibu huu zielekezwe katika kupunguza madeni ya walimu wilayani hapo.
- Changamoto za huduma duni za afya, Elimu na maji; Mkuu wa Mkoa aliwataka Halmashauri kwa kushirikiana na wadau kuboresha huduma hizo na kuhakikisha wanajenga Vituo vya Afya badala ya zahanati ili wakina mama waweze kujifungua salama. Mhe Gambo alichangia bati zaidi ya 500 na fedha zaidi ya Tsh Mil. 3,000,000 ili kushughulikia matatizo hayo. Aidha, alisema hali ya usimamizi wa miradi ya Maji ni mbaya sana hivyo Halimashauri ijipange upya kusimamia miradi hiyo.
- Migogoro ya Ardhi inayotokana na kutopimwa kwa vijiji hivyo na kukosekana kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi; Mhe Gambo ameagiza uongozi wa Wilaya, kukaa pamoja na wawekezaji, Sekretarieti ya Mkoa na wadau wengine kumaliza migogoro kwa kujadiliana changamoto hizi na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu.
- Migogoro na wawekezaji; Mkuu wa Mkoa aliagiza wananchi kushirikishwa katika kila hatua ya uwekezaji (Bottom up approach) ili kuwepo na maridhiano baina ya wawekezaji na wananchi wa meneo husika.
- Uhifadhi hasa katika eneo la Ngorongoro na Loliondo; mkuu wa Mkoa alitaka kuwepo mpango wa uhifadhi ambao hautaathiriwa na mifugo wala ongezeko la idadi ya watu na kuwepo na mikakati wa kudhibiti ongezeko la mifugo ndani ya Kreta ya Ngorongoro.
- Chakula cha Njaa; Rc Gambo alisema Serikali itakaa kuona namna bora ya kupitia matamko mbalimbali yaliyotolewa na viongozi wa awamu iliyopita ya kuwapatia Wananchi magunia kumi bure kwa kila Kaya ili kumaliza tatizo la njaa. Pia alisema Serikali ya Mkoa itakaa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kuangalia namna bora ya kuboresha mpango wa chakula cha bei nafuu kutoka NFRA.
- Baraza la wafugaji; Mkuu wa Mkoa alisema ni muhimu baraza la hilo kufanyiwa upembuzi yakinifu katika mambo yafuatayo:
- Kuangalia kama Baraza hilo linafanya kazi kwa kuzingatia Sheria na Taratibu
- Kama malengo yaliyokusudiwa kuanzisha Baraza hilo yanafikiwa
- Ufanyike ukaguzi kwa matumizi ya Fedha walizopewa kwa kipindi cha miaka mitano maana malalamiko ya matumizi mabaya ya fedha yamekuwa mengi.
“Ikumbukwe kwamba Baraza Hilo la wafugaji la Ngorongoro linapewa zaidi ya TSH 2.5 Billion kila mwaka fedha ambayo ni zaidi ya mapato ya ndani ya Halimashauri ya Ngorongoro” alisisitiza Mhe. Gambo.
- Rc Gambo pia aliagiza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kukamilisha ahadi yake ya Madawati 2000 kwa kumalizia haraka madawati 1500 yaliyobakia ili kusiwe na mtoto yeyote anaye kaa chini Wilayani Ngorongongoro.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha alihitimisha ziara yake kwa kuwataka Madiwani na Wataalam kila mmoja kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria na Taratibu, pia aliahidi kuwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo ili kutafuta ufumbuzi wa haraka wa changamoto zinazoikabili Wilaya ya Ngorongoro.
Imetolewana:
Nteghenjwa Hosseah
Afisa Habari