Home » , » Hukumu ukatili kwa wanawake, watoto kuharakishwa

Hukumu ukatili kwa wanawake, watoto kuharakishwa

Written By CCMdijitali on Saturday, November 26, 2016 | November 26, 2016

Habari Leo 

SERIKALI imeanzisha utaratibu wa kuharakisha kesi zinazohusu unyanyasaji na ukatili wa wanawake na wasichama wadogo ili hukumu zitolewe mapema na wahusika watakaokutwa na hatia wafungwe haraka.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akizungumza baada ya matembezi yaliyoandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLDAF), na mashirika ya kutetea haki za binadamu, ikiwa ni kuelekea siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zilizoanza jana hadi Desemba 10.

Waziri Ummy alisema serikali haiwezi kuendelea kuvumilia kuona wanaume wakijihusisha na mapenzi na wasichana wadogo wakati wakiwaacha wanawake wakubwa.

Alisema ingawa sheria imerekebishwa na kuwa kali lakini bado kesi za matukio hayo zimekuwa zikichukua muda mrefu hivyo kuwanyima haki watu waliotendewa matukio ya udhalilishaji wa kingono ama ukatili.

Ummy alisema serikali imeamua kuanzisha utaratibu wa kuharakisha kesi hizo zinapofikishwa kwenye madawati ya jinsia polisi na mahakamani ili hukumu zitoke mapema.

Mratibu wa WiLDAF, Dk Judith Odunga, alisema takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa watoto wa kike wanaacha shule kabla ya kupevuka huku watoto wa kike wakikatisha masomo yao wakiwa shule za sekondari kuliko wa kiume.

Alisema mazingira yasiyo salama kwa shule yana madhara makubwa na kwamba watoto wanapokuwa shule na kufanyiwa ukatili wakingono wako katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya Ukimwi.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Maria Karadenizi alisema matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yako kwenye mataifa mbalimbali duniani na jitihada zinahitajika kwa ajili ya kuyamaliza.




Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiongea katika uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia  uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto kwake ni  Mkurugenzi wa  WiLDAF Dkt.Judith Odunga ,Balozi wa Ireland nchini Bw.Paul Sherlock(wa tatu kushoto), na Kamanda wa Polisi kanda maalum ACP Lucas Mkondya.
  Mkurugenzi wa WiLDAF Dkt.Judith Odunga akitoa neno la ufunguzi katika  uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia  uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.Kulia kwake ni Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu na ni  Mratibu Mkazi kutoka Umoja wa Mataifa nchini Bi.Maria Karadenizli 



Balozi wa Ireland nchini Bw.Paul Sherlock akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia  uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.kulia kwake ni  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,  Wazee na  Watoto Mhe.Ummy Mwalimu, Mkurugenzi wa WiLDAF Dkt.Judith Odunga, Kamanda wa Polisi kanda maalum ACP Lucas Mkondya na Mkuu wa Dawati la Jinsia,ACP Mary Nzoki.
Waandamaji kutoka Taasisi na Asasi mbalibali  wakionyesha ujumbe mbalimbali unaopinga ukatili wa kijinsia wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia  uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisaini katika ubao wenye kauli mbiu katika uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia  uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Video ⏩⏩


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link