Serikali imewataka maafisa elimu kupanga muda wa kusikiliza kero za walimu na kuzitafutia ufumbuzi ili kuongeza morali ya walimu kufundisha. Agizo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Seleman Said Jafo alipokuwa
akiongea na walimu wa shule ya sekondari Segera iliyopo
wilayani Handeni, wakati wa ziara ya kiserikali
Wilayani Handeni na Mkoa wa Tanga.
Mhe.Jafo alisema kuwa wapo baadhi ya Maafisa elimu ambao
wanajifanya kuwa ni Miungu watu linapokuja suala la kusikiliza na
kutatua kero za walimu. Waziri Jafo alisema “Wapo walimu wanaotembea
umbali mrefu kufuata huduma makao makuu ya Halmashauri kwa wakubwa wao mara nyingi wameshindwa kutatuliwa kero zao hali inayopelekea usumbufu, Kuanzia leo 24/11/2016 napiga marufuku tabia hiyo”.
Aliongeza msisitizo kuwa Maafisa elimu wapo kwa lengo la kuwasikiliza walimu na kuwasaidia kutatua kero zao ili waweze kujikita katika ufundishaji wa wanafunzi. Alisema kuwa walimu ni watu muhimu sana nchini ila wamekuwa wakikatishwa tamaa na utendaji wa baadhi ya
maafisa elimu. Aliongeza kuwa kero kubwa ya walimu ni
kutokupanda madaraja kwa wakati na kutopata stahiki zao ikiwa ni
pamoja na posho za likizo,uhamisho na madai Mengine.
Wakati huohuo, Naibu Waziri aliiagiza Halmashauri ya
Wilaya ya Handeni kukamilisha miradi yote ya SEDP-II ambayo
haijakamilika kuhakikisha inakamilika kabla au ifikapo tarehe
20/12/2016. Alisema kuwa katika kusimamia miradi hiyo na miradi ya
maendeleo kwa ujumla kila mtu lazima atimize wajibu wake na kuhakikisha
fedha iliyotengwa na kutolewa inatumika vizuri na thamani yake kuonekana
kwa muda mrefu (value for money).
Picha ya pamoja ya Mhe. Selemani Said Jafo na waalimu wa shule ya sekondari ya Segera.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni akitoa utambulisho mfupi kwenye ukumbi wa Halmashauri.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Viongozi wakisikiliza kwa makini maagizo ya Naibu Waziri ikiwa ni pamoja na kuwa na usimamizi bora wa rasilimali fedha