WAKATI akielekea kutimiza mwaka mmoja akiwa madarakani, wiki hii Rais John Magufuli alifanya ziara ya siku mbili nchini Kenya kwa mwaliko wa Rais Uhuru wa Kenyatta wa Jamhuri ya Kenya. Hii ilikuwa ni ziara yake ya tatu nje ya nchi tangu aingie madarakani mwezi kama huu mwaka jana. Ziara nyingine alizokwishafanya nje ya nchi ni pamoja na ya Rwanda na Uganda.
Mwanasheria, mhadhiri na mchambuzi wa mambo mbali wa Kenya, Profesa Patrick Lumumba ni miongoni mwa watu wa nje ya nchi ambao wamekuwa wakikoshwa na uongozi wa Rais Magufuli.
Tangu Desemba mwaka jana, ikiwa ni siku chache tu tangu Rais John Magufuli ashike madaraka, profesa huyu anayeheshimika sana Afrika, alionesha kufurahishwa, kuridhika na kumtabiria makubwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania.
Katika mjadala mmoja unaopatikana katika (www.youtube.com/watch?v=9VunShPDovY)
MAGUFULI IS THE REAL DEAL-PLO Lumumba and Barrack Mulaka on Magufuli
MAGUFULI IS THE REAL DEAL-PLO Lumumba and Barrack Mulaka on Magufuli
Profesa huyo wa sheria, maarufu kama PLO Lumumba, anakaririwa akisema kwa Kiingereza kuwa Magufuli ni ‘real deal’, akimaanisha ni kiongozi shupavu ambaye anachokifanya haigizi bali ndivyo alivyo.
Profesa huyo anasema: "Naweza kukuhakikishia kwamba taswira na mtazamo wa Mwalimu Nyerere sasa vinajitokeza dhahiri kwa Rais Magufuli."
Anaendelea: "Na wale wanaodhani kwamba, haya anayoyafanya ni nguvu ya soda wakidhani yanayotokana na msukumo wa uchaguzi, watakuja kushangaa sana.
“Huyu ni mtu ambaye ndani ya miaka 10 ataonesha njia kuhusu uongozi bora na uliotukuka katika eneo hili la Afrika Mashariki.
Mimi si mtabiri …, lakini angalia hali itakavyokuwa." Siku chache baadaye, Profesa Lumumba, ambaye aliwahi kuongoza Kamati ya Maadili na Kupambana na Rushwa ya Kenya, (EACC), pia alisikika akimpongeza Magufuli kupitia mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Alikaririwa akisema, Magufuli amechukua njia sahihi ambayo anaamini muda si mrefu, Watanzania wataanza kunufaika na uongozi wake.
“Rais Magufuli amedhihirisha kwamba yeye kauli yake ni kutenda kazi na amedhihirisha kwamba uongozi mzuri ni utumishi si usultani. Kwa hivyo kwa Watanzania wengi na wadadisi wengi hizi ni hatua ambazo zinashabikiwa na kusifiwa," alikaririwa akisema.
Akaongeza kwamba hatua ya Rais Magufuli ya kupambana na ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma ni jambo ambalo wananchi wengi wa kawaida wanatazamia kuliona kwa rais wao na kwamba hilo litaisaidia sana Tanzania kupiga hatua kimaendeleo.
Akasema hatua ya Rais Magufuli kushiriki katika shughuli za usafi mwaka jana, ilimaanisha pia kwamba yuko tayari kuisafisha Tanzania nzima, si katika mazingira pekee bali pia dhidi ya ufisadi na kuhakikisha wananchi wanaishi maisha mazuri.
Alirudia kusema katika mahojiano hayo na BBC kwamba hatua anazochukua Rais Magufuli si za kujionesha bali anafuata nyayo za marais waliofanya kazi ya kutukuka Afrika kwa ajili ya wananchi na si matumbo yao.
Akawataja viongozi hao ni Mwalimu Nyerere na Kwame Nkrumah wa Ghana.
“Rais Magufuli ameonesha Unyerere na Unkrumah na nina hakika kwamba atawadhihirishia watu kuwa yeye ni mtu mwenye azma njema na Tanzania itakuwa nchi ya kupigiwa mfano katika siku za usoni,” alisema.
Aidha, hivi karibuni, akiwa kwenye mkutano nchini Ghana, Profesa Lumumba katika kuzungumzia hali ya uongozi katika nchi za Afrika, aliendelea kueleza namna anavyomkubali Magufuli. Katika video fupi iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ilimuonesha mwanasheria na mwanasiasa huyo nguli akisema:
"Miongoni mwenu wapo ambao wanatarajia kuwania uongozi kisiasa. Lakini swali la msingi la kujiuliza ni hili: Kwa nini unataka kuongoza?
"Katika Afrika, njia nyepesi ya kupata utajiri wa harakaharaka ambao huwezi kuutolea maelezo namna ulivyopatikana ni kuingia katika uongozi wa kisiasa. Kama unataka kupata utajiri bila kuufanyia kazi kwa namna yoyote basi ingia kwenye siasa za Afrika.
"Huo ndio ukweli, nenda kila mahala Afrika isipokuwa kwa watu wachache sana. Mtu pekee anayeonekana kwa sasa mintarafu suala zima hilo (la kutumikia wananchi na siyo kutafuta utajiri) ni Rais wa Tanzania, John Magufuli.
"Waliobaki katika Afrika... Sijui... Mtanisamehe mimi ni mgeni hapa (Ghana). (Viongozi wetu wengi) wanawinda na kujikusanyia majumba, magari na pesa na hiyo ndio maana uongozi wa Afrika hauwavutii watu wazuri kabisa, wanaume au wanawake.
"Na kwa bahati mbaya sana, wapiga kura nao wanaruhusu kununuliwa kwa pesa, na sina hakika kama hilo linatokea pia hapa Ghana.
"Wapiga kura wa Afrika nao wanatazamia kuhongwa na wagombea ili waweze kuwapigia kura," alisema Profesa huyo ambaye ameshiriki katika mikutano na makongamano kadhaa Afrika.
Katika kipande hicho cha video, Profesa anamalizia kusema kwamba, kama Afrika haitapambana na ukabila (kuchagua mtu kwa ukabila) na rushwa, basi ijue kwamba bara hili halitaweza kamwe kupata viongozi wazuri. Katika baadhi ya nukuu za Profesa Lumumba aliwahi kusema:
"Tunaishi katika bara ambalo tunawapigia makofi na kuwashangilia wezi lakini tunawanyanyasa watu wazuri."
Kadhalika katika nukuu zake maarufu ni hii aliyopata kusema: "Tuna madaktari ambao tumewasomesha lakini tunapokuwa wagonjwa, hasa tabaka la wanasiasa, tunakimbilia London kwa kuwa hatuna imani na madaktari wetu wala hospitali zetu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba rushwa imekita mizizi katika mfumo wetu wa maisha kiasi kwamba hatuwezi kufikiria hali za hospitali zetu za taifa." Profesa huyu pia aliwahi kusema katika nukuu yake nyingine:
"Tunachagua wezi kwa kuzingatia ukabila au ukubwa wa pochi zao (pesa) na bado tunatarajia wafanye mema. Haiwezekani." Pia nukuu yake nyingine ni hii: "Kiongozi mzuri na makini lazima atambuliwe kwa uwezo na uzuri wake na kiongozi dhaifu lazima atambuliwe kwa udhaifu wake."
Aliwahi kunukuliwa pia akisema: "Sisi (Afrika) tunachagua wezi, fisi ili wawalinde mbuzi lakini wakati mbuzi wetu wanapoliwa (na hao fisi) tunashangaa. Tunashangaa nini?" Profesa Patrick Lumumba aliyezaliwa Julai 17 mwaka 1962 nchini Kenya, ni Wakili wa Mahakama Kuu za Kenya na Tanzania.
Pia ni Mhadhiri wa Sheria katika Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Nairobi.
Habari Leo