Baadhi ya Wakurugenzi wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakifuatilia Kikao cha Majumuisho cha Kamati ya Baraza l;a Wawakilishi ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa.
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wake Mh. Omar Seif Abeid akiwa pia Mwakilishi wa Jimbo la Konde Kaskazini Pemba wa Pili kutoka kushoto aliyevaa Koti na jeusi na kofia.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed wa Pili kutoka Kulia akijibu baadhi ya hoja za Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Taasisi za Umma Nchini zinaweza kupata ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake kitaifa endapo Serikali Kuu itaendelea kuzijengea uwezo na miundombinu imara taasisi hizo kwa faida ya kutoa huduma pana zaidi kwa Wananchi.
Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa walieleza hayo wakati wa Kikao cha majumuisho ya ziara waliyofanya kuangalia uwajibikaji katika Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Kikao hicho cha majumuisho kilichowakutanisha Viongozi watendaji wa Taasisi za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo kilifanyika ukumbi mdogo wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuongozwa na Mwenyekiti wa Mh. Omar Seif Abeid akiwa pia Mwakilishi wa Jimbo la Konde Kaskazini Pemba.
Wajumbe hao walisema zipo changamoto nyingi zinazozikumba Taasisi za Wizara hiyo wakizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na uchakavu wa gari za Tume ya Uchaguzi Zanzibar,asimilia 21% ya mgao wa nafasi za ajira katika Taasisi za Muungano pamoja na matumizi mabaya ya elimu ya mitandao inayopotosha Tamaduni za Jamii hasa Vijana.
Akigusia wimbi la changamoto ya Dawa za Kulevya zilizoathiri kwa kiasi Fulani kundi kubwa la Vijana, Mjumbe wa Kamati hiyo kutoka Jimbo la Mpendae Mh. Moh’d Said Dimwa alisema udhibiti wa Dawa za kulevya bado unaonekana kuwa mdogo hapa Nchini.
Mh. Dimwa alisema wakati umefika kwa Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi kuongeza nguvu za udhibiti wa tatizo hilo licha ya kwamba mazingira halisi ya Visiwa vya Unguja na Pemba kuzunguukwa na bahari pande zote.
Alisisitiza kwamba kinachopaswa kuchukuliwa hatua na kufanyiwa kazi kwa wakati huu ni jinsi wahusika wakuu wanaohusika na uingizaji wa biashara hiyo haramu wanavyofuatiliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria badala ya nguvu nyingi kuelekezwa kwa watumiaji wa Dawa hizo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Omar Seif Abeid aliishauri Tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar kuandaa mipango madhubuti ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kwenye changamoto hilo.
Mh. Omar alisema mipango hiyo ni vyema ikazingatiwa zaidi katika kuhakikisha ushiriki wa Wananchi katika sehemu mbali mbali hasa yale maeneo sugu yaliyoshamiri biashara hiyo wanasaidia katika mapambano dhidi ya Dawa za kulevya.
Akitoa ufafanuzi Afisa Mipango kutoka Tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar Nd. Khamis Omar Hassan alisema bado upo umuhimu wa Tume hiyo kuendelea kufanya kazi licha ya kasoro chache zinazokwaza katika uwajibikaji wake.
Nd. Omar alisema Tume hiyo imefanya kazi kubwa ya kutoa elimu inayohusu athari ya dawa za kulevya na kupatikana mafanikio makubwa yaliyochangia kupungua kwa matumizi ya Dawa za kulevya katika Majimbo yote ya Visiwa vya Zanzibar.
Afisa Mipango huyo kutoka Tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar aliiomba Serikali kuu kupitia Kamati hiyo kuipa meno Tume hiyo ili iweze kutekeleza vyema majukumu yake.
Akijibu baadhi ya hoja za Wajumbe wa Kamati hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed alisema Serikali itaendelea kujitahidi katika kuona janga la Dawa za kulevya linaondoka au kupungua kabisa nchini.
Waziri Aboud alifahamisha kwamba juhudi zitafanywa na Serikali kuaangalia njia muwafaka ya kuwatumia wataalamu wa udhibiti wa Dawa za Kulevya kutoa taaluma kwa Viongozi, Wananchi na hata vijana ili kuelewa kwa kina madhara ya janga hilo.
Aliwapongeza Wajumbe wa Kamati ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa kazi kubwa iliyofanya na kuandaa Taarifa nzuri ya ziara yao ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuleta uwiano wa ushirikiano baina ya Kamati hiyo na Taasisi walizozitembelea.
Ziara za Kamati mbali mbali za Baraza la Wawakilishi Zanzibar hufanywa kila baada ya miezi Mitatu kuangalia utekelezaji wa shughuli za Serikali katika Sekta tofauti hapa Nchini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
4/11/2016.