Meneja wa Ranch hiyo Ndg. Fidelis Ole Kashe akiwasilisha taarifa ya Shamba hilo kwenye Kikao maalum na Mkuu wa Mkoa wa Arusha pamoja na viongozi wa Wilaya.
Mkurugenzi wa TLCT Ndg. Boniface Ngimojiro akielezea muundo wa Taasisi hiyo yenye umiliki wa Shamba la Manyara Ranch.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha akitoa maelekezo ya kubadilisha Hati ya Umiliki wa shamba kutoka kwa TLCT kwenda kwa wananchi wa vijiji vya Elesilalei na Ortukai.
Mbunge wa LongIDO Mhe. Julius Kalanga(kulia) akiwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi katika ziara ya Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo akikagua Boma la Ngombe lililopo katika shamba la Manyara Ranch.
Eneo la malisho kwa ajili ya Ngombe 780 waliopo katika shamba hilo na Kondoo 300
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Monduli Mkoani Arusha pamoja na baraza la madiwani la wilaya hiyo kuhakikisha wanabadilisha umiliki wa shamba la Manyara ranch lenye ukubwa wa ekari 44,930 kutoka kwa taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust{TLCT} kwenda kwa wananchi wa vijiji viwili kama Rais wa awamu ya tatu Mhe. Benjamini William Mkapa alivyoagiza.
Rc Gambo alitoa agizo hilo katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kata ya Elesilalei na Makuyuni baada ya kutembelea miradi ya mamilioni ya fedha iliyopo ndani ya shamba hilo inayofadhiliwa na African Wildlife Foundation{AWF} na kuelezwa kero na changamoto zilizopo juu ya umiliki wa shamba hilo kwa taasisi ya TLCT.
Alisema nyaraka zinaonyesha wazi kuwa Shamba hilo lilitolewa kwa wananchi wa vijiji vya Elesilalei na Ortukai na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu mwaka 1999 kwa ajili ya kilimo na ufugaji lakini hilo halikufanyika badala yake taasisi ya TLCT ikajimilikisha shamba hilo kinyume na maagizo.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kutokana na hali hiyo ninawaagiza viongozi wote wa wilaya ya Monduli wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na baraza la madiwani kuhakikisha ndani ya muda mfupi wanabadilisha umilikiwa wa shamba hilo kutoka taasisi hiyo kwenda katika vijiji hivyo.
Gambo alisema serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli iko madarakani kwa ajili ya kuwahudumia wanyonge na watu wa hali ya chini na kamwe haiwezi kuona baadhi ya watu fulani wananufaika na rasilimali ya nchi kwa manufaa yao.
Alisema TLCT inamiliki shamba hilo kinyume na maagizo kwani shamba hilo lilipaswa kumilikiwa na vijiji hivyo kwa faida yao lakini walijitokeza wataalamu wakabadilisha maelekezo hayo na kujimilikisha kitu ambacho Serikali ya Awamu ya Tano haiwezi kulivumilia kamwe.
“Nimeagiza umiliki wa shamba hili unapaswa kubadilishwa haraka kwa kushirikisha vikao na kufuata taratibu zote za kisheria ikiwemo kupitishwa na baraza la madiwani ili wananchi waweze kunufaika na ardhi yao na sio watu wachache wanaolipwa mamilioni ya fedha bila ya sababu za msingi’’alisema Gambo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mhe. Julius Kalanga na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Isack Joseph wote kwa pamoja waliunga mkono wazo la Mkuu wa Mkoa na kusema kuwa watatoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha umiliki wa shamba hilo unabadilishwa na kwenda kwa vijiji hivyo.
Mkurugenzi wa TLCT Bonfance Ngimojiro alipopewa nafasi ya kujieleza katika mikutano hiyo miwili alisema kuwa taasisi hiyo inaongozwa na bodi ya wadhamini yenye wajumbe nane wakiongozwa na Mbunge wa zamani wa Mondul, Mhe. Edward Lowassa kama mwenyekiti wa Bodi hiyo.
Ngimonjiro alikiri kupata amri ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kutoka katika taasisi hiyo kwenda kwa wananchi wa vijiji hivyo viwili lakini yeye hawezi kujuwa ni kwa nini amri hiyo hadi jana haikutekelezwa.
Mkurugenzi huyo alisema yeye ni mwajiriwa tu ambaye hajalipwa mishahara kwa miaka zaidi ya minne sasa katika taasisi hiyo hivyo hawezi kujuwa kwa undani zaidi kushindikana kutekelezwa kwa amri hiyo kwani wakitafutwa wahusika wanaweza kuwa na majibu sahihi.
Naye Meneja wa AWF, Fidelis Ole Kashe yeye alisema kuwa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu sana ndani ya shamba hilo pamoja na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika shamba hilo ikiwemo shule,zahanati ,ufugaji wa kisasa na machinjio.
Kashe alisema utulivu ndio njia pekee itayofanya miradi iliyopo katika shamba hilo kuendelea vinginevyo wafadhili hao wanaweza kusikitisha kila kitu.
Alisema AWF imekuwa mstari wa mbele kufadhili miradi mbalimbali katika wilaya ya Monduli na nchini kwa ujumla na inapenda kuona fedha inazotoa zinafanya kazi iliyokusudiwa na sio vinginevyo.
Mwisho
Nteghenjwa Hosseah , Monduli