Imeandikwa na Mwandishi Maalumu - Habari Leo
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia kuona mamia ya vijana waliofaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanabaki nyumbani eti kwa kuwa hakuna madarasa ya kutosha.
“Serikali haitaridhika kuona vijana waliofaulu vizuri wanashindwa kwenda kidato cha kwanza. Halmashauri zilijua tangu mapema ni wanafunzi wangapi wanaenda shule za msingi kwa hiyo inataka kuona wote waliofaulu wanakwenda sekondari kwa asilimia 100,” amesema.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lindi baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye ikulu ndogo wilayani Nachingwea.
Waziri Mkuu aliwasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kutoa elimu ya bure kwa kila mtoto, hivyo itashangaza kuona watoto wengine wanafaulu na wanashindwa kujiunga na elimu ya sekondari.
“Tumesema elimu ni bure hakuna sababu ya kufanya wengine wasiende shule wakati azma ya Serikali ni kutoa elimu ya bure. Hakikisheni wote wanaingia katika chaguo la kwanza,” amesema.
Aliwataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimefaulisha wanafunzi, lakini hazina madarasa na madawati ya kutosha warudi mezani na kujipanga upya ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapangwa na kuanza na wenzao katika chaguo la kwanza, kwani wakisubiri chaguo la pili wanakuwa wamechelewa.
“Kama tumepokea vijana wengi kwenye udahili wa kidato cha kwanza, ni dhahiri kuwa tutapata vijana wengi watakaomaliza kidato cha nne. Sote tunajua kuna agizo la kila tarafa kuwa na sekondari moja ya kidato cha tano na sita, nataka utekelezaji wa agizo hili usimamiwe kuanzia sasa.”
“Tafuteni moja kati ya shule kwenye tarafa zenu na ipandishwe hadhi kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa ya bwalo, jiko, mabweni, mifumo ya maji, madarasa na vyoo vya kutosha,” amesema.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa na mkewe Mery Majaliwa wakifurahia ngoma ya kikosi cha JKT
843KJ kilichopo Nachingwea ambacho kilikuwepo katika mapokezi ya Waziri Mkuu katika uwanja wa ndege wa Nachingwea .Picha na Chris Mfinanga
843KJ kilichopo Nachingwea ambacho kilikuwepo katika mapokezi ya Waziri Mkuu katika uwanja wa ndege wa Nachingwea .Picha na Chris Mfinanga