Home » » Magufuli: Tutatumbua hadharani

Magufuli: Tutatumbua hadharani

Written By CCMdijitali on Saturday, December 10, 2016 | December 10, 2016

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi waliojitokeza katika sherehe za miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

 Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko     | Habari Leo

SERIKALI imepania kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu waliozoea kutumbua hadharani mali za Watanzania, wala rushwa na mafisadi ili kutetea haki za wanyonge kuwawezesha kufaidi matunda ya nchi yao. Akitoa salamu za sherehe za Miaka 55 ya Uhuru katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana, Rais John Magufuli alisema Serikali ya Awamu ya Tano inaimarisha vita dhidi ya rushwa kwa sababu rushwa ni saratani katika jamii.

“Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuchukua hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwatumbua hadharani wale waliozoea kutumbua hadharani mali za Watanzania na tutaendelea kuchukua hatua kali katika masuala ya rushwa na ufisadi, kwa sababu rushwa ni saratani," alisisitiza Rais Magufuli.


Alisema katika mwaka mmoja wa utawala wake kumekuwa na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ufisadi kwa baadhi ya watendaji na kubainika wafanyakazi hewa 19,000, kaya masikini hewa 55,000 na wanafunzi hewa 65,000, mambo ambayo hayana budi kudhibitiwa ipasavyo.

Alisisitiza kuwa lengo la hatua hizo zote ni kuboresha maslahi ya Watanzania wote badala ya wachache, hivyo kuwataka kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ufisadi kama huo na rushwa.

“Tunataka kuondoa uonevu kwa wananchi wanyonge waweze kunufaika na Tanzania yao,” alifafanua na kuwakumbusha Watanzania kuendelea kudumisha amani, utulivu na kuwafichua wale wanaotaka kuivuruga amani.

Sambamba na hayo, aliwataka kuimarisha mshikamano, kuulinda muungano na kila mmoja kuchapa kazi ili kujiletea maendeleo.

Alisema katika miaka 55 ya Uhuru yamepatikana mafanikio mengi, kwani Tanzania ya leo ni tofauti na ile iliyokuwa mwaka 1961 ,ambapo yeye alikuwa na umri wa miaka miwili tu.

Rais Magufuli alisema tangu wakati huo, mipaka yote ya nchi iko salama na kuendesha mambo yake kwa kujiamulia yenyewe huku ikiwa imara yenye umoja na mshikamano bila kubaguana kwa misingi yoyote huku wakidumisha muungano, hivyo Watanzania lazima wajipongeze.

Alisema katika miaka hiyo, miundombinu mbalimbali ya kiuchumi imejengwa pamoja na huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na elimu na afya zimeboreshwa na kusogezwa karibu na wananchi tofauti na zamani watu ambapo watu walilazimika kutembea muda mrefu kutafuta huduma hizo.

Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali imejipanga kufanya kazi, kwani viongozi wote aliowateua wanamsaidia vizuri na kuomba Watanzania kuwapa ushirikiano akisisitiza serikali haitawaangusha katika kutekeleza ahadi zake, ikiwa ni pamoja na kutatua kero bila ubaguzi.

“Napenda kuchukua nafasi hii kueleza kuwa serikali yangu itaendelea kuziendeleza jitihada zilizofanywa na serikali zilizotangulia na kujitahidi kutatua changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa zimeanza kutatuliwa,” alisema.


Alisema matunda ya juhudi hizo ni pamoja na kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kutoka wastani wa Sh milioni 877 hadi kufikia Sh trilioni 1.2 kwa mwezi, kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari kwa kutengewa Sh bilioni 18 kila mwezi, kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa shule za msingi, sekondari huku idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu nayo ikiendelea kupaa na kuongezewa kiasi cha mikopo ya elimu ya juu.

Alifafanua pia kwamba serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya umeme, ujenzi wa barabara na reli, meli na kuvutia wawekezaji kujenga viwanda kufikia lengo la uchumi wa kati.

Alisema serikali itakusudia kuongeza ndege nyingine nne ili kufanya idadi ya ndege mpya kufikia sita, kwani tayari mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400 zimeshawasili nchini tangu Septemba mwaka huu na kwamba nyingine mbili zinatarajiwa kuwasili nchini katikati ya mwaka kesho na nyingine kubwa mwaka 2018 na tayari wameanza majadiliano.

Rais alisema wamenunua ndege hizo ili kujenga uchumi na utalii wa nchi, kwani bila miundombinu kama hiyo ni vigumu kujenga uchumi imara.

Katika salamu zake pia kwa watanzania, alisema kuanzia mwakani sherehe za Uhuru zitafanyika makao makuu ya nchi mkoani Dodoma na kuungwa mkono na viongozi mbalimbali wakiwemo wananchi wa kawaida waliohudhuria sherehe za jana.

Wakizungumza baada ya maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa chama cha ACT – Wazalendo, Anna Mghwira alisema kumbukumbu ni nzuri ya uhuru, kwani nchi imejitahidi kufikia uhuru kamili hivyo kujipanga kutekeleza katika sekta mbalimbali yahitaji kwenda polepole katika kukabiliana na changamoto za uhuru.

Alisema kuhamishia maadhimisho hayo Dodoma ni uamuzi mzuri, kwani itasaidia katika kupeleka hamasa mikoani badala ya kila mwaka kufanyika katika sehemu moja ya nchi.

Mkuu wa Mkoa Mteule wa Njombe, Christopher Ole Sendeka alisema maadhimisho hayo yamefana na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuongoza nchi vizuri na kuendeleza amani iliyopo.

Alitaka Watanzania kumuunga mkono Rais Magufuli katika kutekeleza misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya kupambana na rushwa. Baadhi ya wananchi walioshiriki kwenye maadhimisho hayo, walielezea kufurahishwa na jinsi yalivyofana, huku wakitaka maonesho ya ndege za vita, halaiki na askari wa miavuli yaongezwe katika sherehe zijazo.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia wananchi waliohudhuria sherehe za miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama wakati wimbo wa Taifa ulipokuwa ukipigwa uwanjani hapo.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais Mstaafu wa Awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi mara baada ya Kuwasili katika uwanja wa Uhuru.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda mara baada ya kuwasili

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link