Imeandikwa na Ikunda Erick | Habari Leo
MAELFU ya wananchi wa jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani jana walifurika kushuhudia maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara, yaliyofanywa jijini hapo huku yakinogeshwa na vikosi vya gwaride la pamoja la majeshi yote nchini.
Milango ya kuingia kwenye Uwanja wa Uhuru ilianza kufunguliwa alfajiri ya jana huku wananchi na wageni waalikwa kutoka kona mbalimbali za nchi wakimiminika uwanjani hapo hali iliyosababisha viwanja hivyo kufurika majira ya saa tatu asubuhi hivyo ikalazimu Uwanja wa Taifa kufunguliwa ili wananchi waingie.
Sherehe hizo zilifana kwa aina yake ambapo gwaride la pamoja lenye vikosi 10 vilivyoundwa na askari kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Polisi, Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa lilinogesha sherehe hizo huku maelfu ya wananchi na wageni wakishangilia kwa furaha.
Baada ya gwaride hilo kuingia uwanjani hapo saa tatu asubuhi, lilijipanga tayari kwa kumsubiri Amiri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli ambaye aliingia uwanjani hapo akiwa kwenye gari la wazi saa nne na kuzunguka uwanja huku akiwapungia mkono wananchi walioitika kwa vigelegele na shangwe jambo lililofanya uwanja mzima uliojaa watu kulipuka kwa furaha.
Kabla ya kukagua gwaride, Rais Magufuli alipigiwa mizinga 21 akakagua gwaride akiongozana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange alipokaribia mwisho wa kukagua alishindwa kuvumilia na kuamua kutembea kijeshi huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Moja ya matukio yaliyovutia zaidi uwanjani hapo ni umahiri wa kikundi cha Makomando wa jeshi la Ulinzi Tanzania, ambao walionesha matukio tisa ya ujasiri, ukakamavu na uimara wa miili na moja ya tukio lililofurahisha hadhira iliyokuwa uwanjani hapo ni lile la makomandoo wawili kuvuta gari kubwa ya jeshi aina ya IVECO.
Pia makomandoo hao walionesha uimara wa miili yao kwa kupasua matofali juu ya kifua cha mwenzao na onesho jingine ni lile la kulalia kibao cha misumari na kisha wenzao kupita juu yake. Maelfu ya wananchi walishangilia kwa kasi pale gwaride la kimyakimya lilipokuwa likionesha umahiri wao wa kucheza na silaha.
Aidha, katika gwaride la pamoja lenye vikosi 10, lilipita mbele ya Rais kwa mwendo pole na mwendo haraka huku kila kikosi kikionesha umahiri wake na kushangiliwa na wananchi na walipomaliza ndipo kikosi maalumiu cha wanajeshi wa maji kikapita mbele ya rais huku kila mmoja akibeba begi la kilogramu 65, lenye vitu na vyakula vya kutumia kwa siku saba.
Maadhimisho hayo pia yalipambwa na vikundi vya ngoma na kwaya ya pamoja ya majeshi hayo yaliyoimba wimbo maalumu wa kuimiza kaulimbiu ya kuunga mkono jitihada za kupinga rushwa na ufisadi na kuimarisha uchumi wa viwanda kwa maendeleo.
Wananchi walionekana kufurahishwa na maadhimisho hayo ambapo wengi wa waliohudhuria viwanjani hapo waliambatana wa familia zao na wakati maadhimisho yakihitimishwa, wengi wa wananchi waliondoka kwa utulivu viwanjani hapo wengi wao wakitembea kwa miguu kurudi mwakao.
Kikosi cha Maadhimisho cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kikionesha gwaride la kimyakimya mbele ya Amiri Jeshi mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa Uhuru.
Vikosi mbalimbali vya Majeshi vikipita mbele ya mgeni Rasmi kwa mwendo wa pole na Haraka katika sherehe za miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.