Imeandikwa na Veronica Mheta - Habari Leo
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa kubuni mbinu za kuwakwamua vijana wa bodaboda kwa kuwakopesha pikipiki zaidi ya 200 bila ya riba.
Majaliwa alitoa pongezi hizo juzi jijini hapa kabla ya kuondoka na kurejea Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli nyingine za kikazi.
Alisema ubunifu alioufanya Gambo unapaswa kuigwa na viongozi wengine kwani amethubutu kuwafungulia vijana fursa za kujiajiri wenyewe na kujikwamua kuuchumi.
Alisema ingawa baadhi ya watu wasiopenda maendeleo wanatoa maneno mengi kuhusu pikipiki hizo, lakini anampa moyo Gambo akimtaka endelee kuwawezesha vijana ili waachane na mambo ya kujaa vijiweni kujadili vitu visivyofaa au kujiingiza katika mambo ya ajabu.
"Gambo nakupongeza kwa kuonesha mfano kwa vijana na wapo wanaobeza juu ya hili uliofanya wacha waongee maana hawajui ulipoanzia mkakati huu hadi hapa uliopo sasa. Ni kazi yao kusema lakini wewe songa mbele kuhakikisha vijana wanapata ajira kwani pikipiki hizi hazina marejesho bali wanarudisha fedha kidogo ili vijana wengine waweze kukopeshwa tena pikipiki," alisema.
Pia Majaliwa aliipongeza Benki ya TIB iliyotoa Sh milioni 20 kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha, ikiwa ni mchango wake kwenye mradi wa vijana unaosimamiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa ajili ya vijana.
Pia alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo ya TIB, Frank Nyabundege kwa kutoa pikipiki kumi na wadau waliowezesha pikipiki hizo kupatikana.
Pia ametoa rai kwa benki nyingine kuhakikisha wanatoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana hao ili waweze kufungua akaunti pamoja na kukata bima za maisha.