Imeandikwa na Veronica Mheta, Arusha - Habari Leo
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amerudisha mikononi mwa Halmashauri ya Jiji la Arusha eneo la wazi Kilombero jijini humo ili wafanyabiashara waendelee na shughuli zao. Eneo hilo lilichukuliwa kinyemela.
Majaliwa ametoa uamuzi huo jijini Arusha wakati alipozungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kukatisha ziara yake mkoani hapa na kuahidi kurudi tena kumalizia ziara hiyo.
Amesema eneo hilo awali lilikuwa ni kwa ajili ya wafanyabiashara kuuza bidhaa zao hapo pamoja na wanawake, lakini cha kushangaza wajanja wachache walilichukua eneo hilo kwa kuuziana na baadhi ya watu huku wafanyabiashara wakifukuzwa.
Kwa mujibu wa waziri Mkuu, alipokuwa katika ziara yake Arusha Mjini, alifika eneo hilo na kujionea jinsi lilivyozungushwa uzio wa matofali huku wafanyabiashara wakishindwa kuuza bidhaa zao hapo, hivyo kuanzia juzi eneo hilo mmiliki halali ni serikali chini ya Jiji la Arusha.
“Rais ameridhia eneo hili kurudishwa kwa wafanyabiashara na natoa rai kwa Jiji la Arusha kupitia kwa Mkurugenzi Athumani Kihamia kuhakikisha pamoja na madiwani wanapanga matumizi sahihi yatakayowasaidia wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao eneo lile," alisema.
Pia alitoa rai kwa benki ya TIB pamoja na taasisi nyingine zinazotoa mikopo kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao inayohusu ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Mara baada ya uamuzi huo baadhi ya wafanyabiashara wa Jiji la Arusha walimpongeza Majaliwa kwa kurudisha eneo hilo ambalo awali walikuwa wakiligombania na baadhi ya wafanyabiashara walikimbilia soko la NMC, ambalo halina huduma muhimu kama vyoo na mahali pa kujihifadhi na mvua.
Mmoja kati ya wafanyabiashara hao, Lucas Samweli aliupongeza uongozi wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kwa kufungua fursa za wafanyabiashara wanyonge ikiwemo kuruhusiwa kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya katikati ya mji ili waweze kupata wateja na kupata fedha zinazowasaidia kujikwamua kimaisha.