Home » » Miaka 55 ya Uhuru mengi yamefanyika

Miaka 55 ya Uhuru mengi yamefanyika

Written By CCMdijitali on Thursday, December 8, 2016 | December 08, 2016

 Imeandikwa na Frank Mvungi, Maelezo     - Habari Leo

LEO Watanzania wanaadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Nchi yetu inaadhimisha siku hii muhimu huku serikali ikipongezwa kwa mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi chote tangu awamu ya kwanza hadi awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Tukiimulika awamu hii ya tano, Watanzania walio wengi wameonekana kukunwa na kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli, kutokana na kushuhudia mengi mazuri japo ni katika kipindi kifupi tu cha uongozi wake.

Ni kwa mantiki hiyo, Watanzania wengi kesho watakuwa wanaadhimisha uhuru wa Tanzania bara huku wakimuombea kwa Mwenyezi Mungu amlinde Rais Magufuli na kumpa nguvu ya kuendelea na juhudi anazozifanya ili Watanzania wanufaike na yale mema anayoendelea nayo na yale aliyopanga kuwafanyia.

Baadhi ya mazuri yanayofanyika ni pamoja na kushuhudia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) likiwa na ndege mpya huku kukiwa na mikakati mingine ya kununua ndege nne zaidi zikiwemo kubwa na za kisasa.

Hii maana yake ni kwamba itaisaidia nchi kiuchumi hasa kwa kuzingatia kwamba itawezesha watalii kuja nchini moja kwa moja kutoka nchi zao.

Mikakati mingine inayotia faraja ni ya ujenzi wa reli ya kati kwa viwango vya kimataifa (standard gauge) huku pia kukiwa na mkakati wa kuisuka upya reli ya Uhuru (Tazara) inayomilikiwa kwa ubia baina yetu na Zambia ili izidi kuchanua kuliko ilivyo sasa.

Nchi yetu pia inaadhimisha miaka 55 ya Uhuru kukiwa na mabadiliko makubwa katika nyanja nyingi, ikiwa ni pamoja kudhibitiwa kwa ufisadi na kurejea kwa nidhamu kazini, hususani katika sekta ya umma.

Kutokana na utendaji uliotukuka wa rais wetu, wengi wanathubutu kusema kwamba amevaa viatu vya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na hususani kupitia kaulimbiu yake ya “Hapa Kazi Tu” inayoakisi kaulimbiu aliyoiasisi Baba wa Taifa ya “Uhuru Na Kazi”.

Kufanya kazi kwa bidii ni kielelezo cha uhuru wetu na msingi wa kujenga uchumi wa viwanda utakaosaidia kukuza uchumi kwa kasi zaidi katika kipindi hiki ambapo maendeleo yanahitaji watu kufanya kazi kwa bidii na weledi.

Uhuru wetu umekuwa kielelezo cha mafanikio tuliyoyapata katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, miundombinu, ujenzi na nyingine nyingi.

Siku kama ya kesho ya kila mwaka ni siku ya kutafakari hatua tuliyofikia tangu tupate uhuru na kuongeza juhudi kwa kufanya kazi bila kuchoka ili kuijenga Tanzania mpya ambayo tayari misingi imejengwa na waasisi wetu na kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu ni katika kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya asali na maziwa.

Kuimarika kwa huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni kielelezo kuwa tumeweza kuitekeleza ile dhana ya Uhuru ni Kazi na dhana nzima ya kuujitegemea vyema. Kwa hali hiyo, tunamuenzi vizuri Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambaye nyakati zote alisisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa nchi kujitegemea.

Serikali katika awamu zote, tangu ya kwanza hadi sasa zimekuwa zikiweka kipaumbele katika sekta takribani zote zinazochangia ustawi wa maisha ya wananchi ikiwemo elimu.

Hali hii imechangia kuongezeka kwa shule za msingi nchini, shule za sekondari na vyuo vikuu ambapo wakati wa uhuru hakukuwa na chuo kikuu hata kimoja lakini sasa tunavyo vyuo vikuu 48.

Bila shaka huwezi kupuuza kwamba haya si mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa katika kipindi cha miaka 55 katika eneo hilo moja tu la elimu. Utoaji wa elimu bure ni dhamira ya serikali ya awamu ya tano inayolenga kuhakikisha kuwa mtoto wa kitanzania, na hususani wa maskini, asishindwe kusoma kutokana na ada kwani, kama alivyosema Mwalimu Nyerere: "Ukitaka kumsaidia mtoto wa maskini, mpe elimu."

Mwalimu pia aliamini kwamba elimu ni zana muhimu, siyo tu katika kupambana na adui ujinga, bali pia maadui wengine wawili; maradhi na umaskini. Miundombinu ya barabara ni eneo lingine la kujivunia wakati kesho tunaposherehekea miaka 55 ya Uhuru.

Nchi yetu sasa inazo barabara za lami nyingi na madaraja ambayo yamerahisisha mawasiliano kati ya mkoa na mkoa, wilaya na wilaya, kata na kata hadi ngazi ya vijiji.

Wananchi wanafurahia matunda ya Uhuru wao na rasilimali za Taifa lao. Sekta ya maji pia imeimarika ukilinganisha na wakati wa uhuru ambapo moja ya miradi mikubwa iliyotekelezwa na serikali ni pamoja na huu wa maji wa Ziwa Victoria ambao umefanikisha kutoa maji katika ziwa hilo hadi Shinyanga na bado kuna mpango wa kuyafikisha hadi katika maeneo ya mkoa wa Tabora.

Sambamba na hilo, mradi mwingine muhimu mintarafu suala zaima la kuboresha huduma za maji ni upanuzi wa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ambayo imeanza kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Wananchi wote bila kujali itikadi zetu tunalo jukumu la kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa rasilimali za Taifa na miundombinu iliyopo kwa maslahi ya taifa kwa kuwafichua wale wote wanaokwamisha au kuhujumu nia njema ya Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Sherehe za Uhuru zitaadhimishwa kesho kitaifa jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Rais John Magufuli kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe mwaka mmoja uliopita. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni:

“Tuunge mkono jitihada za kupinga rushwa, ufisadi na kuimarisha uchumi wa viwanda kwa maendeleo yetu.” Kaulimbiu hii inasadifu yale ambayo kiongozi wetu mkuu anayasimamia, hivyo ni wajibu wetu Watanzania kuunga mkono juhudi hizi za kuwakwamua Watanzania kiuchumi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link