Home » » Rais Magufuli kuandika historia miaka 55 ya Uhuru

Rais Magufuli kuandika historia miaka 55 ya Uhuru

Written By CCMdijitali on Thursday, December 8, 2016 | December 08, 2016

RAIS John Magufuli
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko  - Habari Leo


RAIS John Magufuli leo anatarajiwa kuongoza Watanzania katika kilele cha maadhimisho ya Miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara, yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki sherehe hizo.

Kaulimbiu katika maadhimisho hayo ni “Tuunge mkono jitihada za kupinga rushwa na ufisadi na tuimarishe uchumi wa viwanda kwa maendeleo yetu.”

Maadhimisho hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza tangu Dk Magufuli kuingia madarakani kutokana na mwaka jana kuzisitisha na kutaka kuadhimishwa kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini.

Rais Magufuli aliagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa maadhimisho hayo zaidi ya Sh bilioni nne kutumika kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.

Katika maadhimisho hayo yatahudhuriwa na marais wa nchi jirani na viongozi wastaafu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema wiki hii kwamba sherehe hizo zitapambwa gwaride la heshima lililoandaliwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na Magereza.

Pia kutakuwa na maonesho ya kwata la kimya kimya pamoja na makomandoo wa JWTZ, burudani za vikundi vya muziki wa kizazi kipya na kizazi cha zamani pamoja na ngoma za asili kutoka mikoa ya Mbeya, Pwani, Lindi na Zanzibar.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa aliwataka Watanzania kusherehekea sikukuu hiyo kwa kumuenzi Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere kwa kuzingatia na kuendeleza misingi aliyoacha ambayo marais wote waliomfuata waliisimamia.

Msekwa ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema katika maadhimisho hayo ni vema kumkumbuka Nyerere na wenzake walioshiriki kupigania kwa kutambua kuwa haukuja kama mvua na bila waoa katika nyakati hizi hali ingekuwaje?

Alisema ni vema kuangalia kwa jinsi alivyopambana na changamoto mbalimbali wakati wa kugombania uhuru na jinsi alivyokuwa akitumia busara na kuona mbali kuwashauri wenzake na kutoa mfano katika moja ya kikao, wenzake walishauri kususia, lakini yeye aliona mbali kwa kuwataka kushiriki kwani kususia kwao kungetoa mwanya kwa wakoloni kuzidi kuwatawala.

Pia Msekwa alisema hivyo ni vema Watanzania kumuenzi kwa kuona mbali kwa kila maamuzi wanayofanya na kuacha kuangalia hapo walipo pekee huku akieleza bayana kuwa kwa yaliyofanyika tangu uhuru kila mtu anayaona na haihitaji kuambiwa.

Aidha, alisema jambo lingine la kujifunza kwa Nyerere kwa wakati huu ni kutowakubalia wale waliokuwa wakitaka uraia kwa Tanganyika uwe kwa Waafrika pekee na kuwaacha waliokuwa na asili ya Kihindi na wengineo na kuwaeleza kuwa kwa wakati ule wanapambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na wao wanataka kufanya ubaguzi Tanganyika.

Wakati huo huo, mradi wa upanuzi wa barabara mpya ya Bagamoyo eneo la Morocco- Mwenge jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 ambayo ilikuwa ikifanyiwa upanuzi kutokana na fedha za sherehe hizo kwa mwaka jana, umekamilika.

Alipoingia madarakani Rais John Magufuli alisitisha sherehe za Uhuru mwaka jana na kuagiza fedha hizo, zikafanye upanuzi wa barabara hiyo na badala yake maadhimisho ya siku hiyo yalifanyika kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi), Joseph Nyamhanga alisema upanuzi wa barabara hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali katika kutafuta suluhisho la kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.

Nyamhanga alisema kwa mujibu wa takwimu za Desemba, 2015, magari yanayopita katika barabara hiyo kwa siku ni 12,484.

“Kufuatia agizo la Rais kwamba sherehe za Uhuru ambazo zingeadhimishwa Desemba 9, mwaka jana zisifanyike na badala yake fedha ambazo zingetumika zielekezwe katika upanuzi wa barabara ya Morocco-Mwenge, Wakala wa Barabara (TANROADS) imetekeleza kazi hiyo katika mpango wa Sanifu na Jenga ambapo Mkandarasi alisanifu na kujenga barabara hii,” alieleza Katibu Mkuu.

Alisema mradi huo umetekelezwa kwa miezi sita ambako ulisainiwa Januari 5, 2016 na kazi ilianza siku hiyo na hatimaye kukamilika Mei, 2016.

Alisema mradi ulitekelezwa kwa kupanua eneo la ujenzi na kuongeza njia mbili zenye upana wa mita 3.25 kila moja na kufanya barabara kuwa njia tano ambazo zimepunguza msongamano wa magari katika Barabara ya Morocco- Mwenge ambayo inaunganisha barabara muhimu za Kawawa na Sam Nujoma.

Alisema upanuzi wa barabara hiyo umefanywa sanjari na uboreshaji wa taa za kuongozea magari katika eneo hilo.

Aidha, alisema pamoja na mafanikio hayo, kulikuwa na changamaoto ya kugundulika kwa mabomba mengi ya maji safi katika eneo la ujenzi kulitatuliwa kwa mkandarasi kufanya kazi kwa ushirikiano na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO) katika kuyahamisha au kuyalinda ili yasiharibike.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link