Home » , » RAIS DKT MAGUFULI AKUTANA NA ALHAJ ALIKO DANGOTE IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

RAIS DKT MAGUFULI AKUTANA NA ALHAJ ALIKO DANGOTE IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Written By CCMdijitali on Saturday, December 10, 2016 | December 10, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara Alhaji Aliko Dangote Ikulu jijini Dar es Salaam.
₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋₋
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
leo tarehe 10 Desemba 2016, amekutana na kufanya mazungumzo na
Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo  Mtwara, Alhaji Aliko Dangote.

Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemhakikishia mfanyabiashara
huyo kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa
wawekezaji wote nchini katika
kutimiza lengo lake la kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Rais Magufuli amesema kuhusu kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote
kilichopo Mkoani Mtwara hapakuwa na tatizo lolote ila kulikuwa na watu  ambao  
walitaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi
huo kwa kufanya biashara za ujanja kitu ambacho serikali yake haikiruhusu.

Amemtaka Dangote kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC ambacho ni chombo
cha serikali badala ya kutumia watu ambao wamekuwa
na nia ya kutengeneza faida tu.

''Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha uwasiliane na viongozi wa serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya
ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili '' amesema
Rais Magufuli.

Dokta Magufuli amesema Dangote ametaka eneo dogo ambalo angelitumia  
kusafirishia saruji yake wakajitokeza watu ambao wametaka kumuuzia kwa
shilingi bilioni 43  kitu ambacho hakina uhalisia wowote bali ni watu ambao wanataka kutengeneza faida kitu ambacho hakiwezekani.

Kwa upande wake mmiliki wa Kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote
ameshangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa amefunga kiwanda kwa sababu
amekatazwa kuagiza makaa ya mawe toka nje ya Tanzania kitu ambacho amesema
hakiingii akilini kwa sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora
kuliko kuagiza nje.

Katika kuthibitisha hilo,  tayari Mfanyabiashara
huyo ameingiza malori mapya 600 kwa ajili ya kusambazia saruji yake. Ameongeza
kuwa lengo la kufanya biashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida pia ana
lengo la kuisaidia serikali ya Tanzania kutengeneza ajira hivyo hana sababu ya
kuagiza mali ghafi toka nje ya nchi  ambazo zinapatikana nchini.

Alhaji Dangote amemuhakikishia Rais magufuli kuwa ataendelea kufanya kazi na Serikali ya  Tanzania  na kamwe hana nia yoyote ya kufunga kiwanda chake kama inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari bali ana mpango wa kuangalia fursa nyingine zaidi za uwekezaji hapa
nchini kutokana na uwepo wa sera nzuri za uwekezaji chini ya
Serikali ya Awamu ya Tano.

Katika hatua nyingine Rais Dkt.John Pombe Magufuli amemuapisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Olonyokie Ole-Sendeka anayechukua nafasi ya Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Wengine walioapishwa na Rais Magufuli ni Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye anakuwa  Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo (Kilimo), Dkt. Maria Sasabo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Dkt. Aloyce K. Nzuki kuwa
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Bibi Grace Alfred Martin
kuwa Balozi (Mkuu wa Itifaki).
 Jaffar Haniu,
Naibu Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU.
Dar es Salaam.
10 Desemba,2016.
──────────────────────

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika kikao cha pamoja na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara Alhaji Aliko Dangote aliyeambatana na ujumbe wake Ikulu jijini Dar es Salaam.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara Alhaji Aliko Dangote mara baada ya kumaliza kwa kikao chao Ikulu jijini Dar es Salaam.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mara baada ya kumaliza kikao chake na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara Alhaji Aliko Dangote Ikulu jijini Dar es Salaam.


Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara Alhaji Aliko Dangote akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam. 


Picha na Video na IKULU.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link