Home » » Vyombo vya habari viache kupotosha

Vyombo vya habari viache kupotosha

Written By CCMdijitali on Sunday, December 11, 2016 | December 11, 2016

UMEFIKA wakati sasa vyombo vyote vya habari nchini vione umuhimu wa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa vitendo, badala ya kuendeleza uandishi wa mazoea usiojali haki ya kumpa mwananchi habari zenye ukweli na uhakika, ili aweze kufanya uamuzi kuhusu mambo mbalimbali yanayoihusu nchi yake.

Ikumbukwe kuwa, wananchi wengi wanategemea kupata taarifa tofauti kupitia vyombo vya habari mbalimbali vya ndani na nje ya nchi, jambo linalodhihirisha wazi kuwa wanaviamini kwa asilimia kubwa.

Kwa kipindi kirefu sasa, baadhi ya vyombo vya habari nchini vimeonekana kuwa mstari wa mbele kukiuka maadili ya taaluma ya habari, kutokana na jinsi vinavyoendeleza uandishi wa habari usiojali ukweli wala kuzingatia haki, hivyo kuvifanya viwe madaraja ya kuvusha taarifa za uchochezi zinazolenga kubomoa na si kujenga kama inavyotegemewa.

Ni jambo la aibu na la kustaajabisha kuona baadhi ya vyombo vya habari vinavyotegemewa kutoa taarifa zenye ukweli nchini, vikitumika kusambaza taarifa za uongo, hivyo kuupotosha umma na kuusababisha ufanye uamuzi usio sahihi pindi unapotakiwa kufanya uamuzi kuhusu ushiriki kwenye masuala mbalimbali ndani ya nchi, ikiwemo uwekezaji.

Ni vizuri wanahabari wakaelewa kuwa wananchi wanatumia taarifa mbalimbali zinazosambazwa na vyombo vya habari ili kuamua hatua ya kuchukua katika kushiriki shughuli za maendeleo kwenye nchi yao, kama vile uzalishaji, uwekezaji na shughuli nyingine, zikiwemo za kisiasa .

Kuwapotosha wananchi kwa taarifa zisizo na ukweli ni kuwasukuma kufanya uamuzi usiofaa. Jambo la msingi kwa wanaopotosha ni kuacha kufanya hivyo mara moja kwa kutii miiko ya uandishi bora wa habari, ambayo ni pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.

Jana mwekezaji mkubwa kutoka Nigeria, Alhaji Aliko Dangote, anayemiliki kiwanda cha kuzalisha saruji mkoani Mtwara alizungumza Ikulu, Dar es Salaam kuhusu sakata lake lililozungumzwa sana na vyombo vya habari mbalimbali nchini na kueleza kuwa baadhi vilipotosha.

Huku akionesha kusikitishwa na vyombo hivyo vya habari vilivyojinyima haki ya kutafuta ukweli kuhusu sababu za kufunga kiwanda chake hicho, Dangote alivishangaa waziwazi na kueleza kuwa hakufunga kiwanda chake kwa sababu inayoelezwa kuwa ni kuzuiwa kununua makaa ya mawe kutoka Afrika ya Kusini, jambo aliloeleza kuwa ni upotoshaji.

Mambo hayo yote wanahabari ambao Dangote aliwashangaa jana waliyapuuza na kuacha kuwaambia Watanzania kwa malengo yao, ikiwemo kuwachonganisha na Serikali yao na kuwakimbiza wawekezaji.

Tunatoa wito kwa vyombo vya habari kuwa makini kwani ni haya ya kuudhi yenye kukosa upekuzi sahihi katika masuala yanayohitaji upekuzi makini yanayofanya watu waonekane wa hovyo na wasiokuwa wazalendo.

Tunapaswa kutambua kabla hatujarekebishwa na sheria, kujirekebisha na kuacha kuwa sehemu ya wapiga dili ili tusiwatie nyong’o wawekezaji wenye nia safi na taifa letu.

  Imeandikwa na Mhariri    - Habari Leo

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link