Home » » Ziara ya Majaliwa imeleta manufaa Arusha

Ziara ya Majaliwa imeleta manufaa Arusha

Written By CCMdijitali on Tuesday, December 6, 2016 | December 06, 2016


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipoingia kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kuhutubia mkutano wa hadhara Jumamosi, Desemba 03,2016


Imeandikwa na Mhariri - Habari Leo

Press Release:-

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anaendelea na ziara yake katika mkoa wa Arusha.

Yapo mambo mengi yamejitokeza katika ziara hiyo, ikiwemo kuhutubia wananchi katika maeneo mbalimbali, kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza maswali kutoka kwa wananchi na kutoa majibu pale pale na pengine kuagiza viongozi wanaohusika wayatatue.

Mathalani, juzi alitembelea Kituo cha Afya cha Levolosi, ambapo alielezwa na mmoja wa wagonjwa kuwa mtoto wake alifia tumboni, baada ya wauguzi na madaktari wa kituo hicho kuchelewa kumpatia matibabu.

Wakati anahudhuria kliniki, mtu huyo aliambiwa na daktari kuwa anatakiwa kujifungua kwa njia ya upasuaji na hawezi kujifungua kwa njia ya kawaida, hivyo aliwaambia manesi kuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji.

Lakini, wauguzi walimkatalia na kumlazimisha ajifungue kwa njia ya kawaida.
Alishindwa kuzaa kwa njia ya kawaida, ambapo baada ya muda manesi walimwambia kuwa mtoto amekufa, hivyo atafanyiwa upasuaji ili kuokoa maisha yake.

Huo ni unyama wa hali ya juu na haukutarajiwi ungetokea katika kituo kama hicho, kinachoendeshwa kwa kodi ya serikali. Hali kadhalika, unyama huo haukutarajiwa kufanywa na wauguzi wanaotakiwa kuzingatia weledi na maadili ya kazi.

Tunampongeza Waziri Mkuu kwa kumwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Frida Mokiti kubadilisha uongozi wa kituo hicho cha afya baada ya kulalamikiwa kuwa kinatoa huduma mbovu kwa wagonjwa, hususan wajawazito.

Hatuhitaji madaktari au wauguzi wanaolipwa mishahara kwa kodi ya wananchi, kusumbua na kunyanyasa wagonjwa.

Tuna imani madudu aliyoyaona Waziri Mkuu huko Levolosi, hayapo huko tu bali yapo katika maeneo mengine nchini. Katika maeneo kadhaa nchini, bado kuna wananchi wanaumizwa na watumishi wa serikali wababe na wanyanyasaji.

Tunasema hivyo kwa sababu siyo madaktari na wauguzi tu wanaofanya hivyo, bali wapo pia baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika mikoa mbalimbali, wanaoonea na kunyanyasa wanafunzi na wazazi bila kuchukuliwa hatua kali.

Tunaomba wakuu wa wilaya na mikoa kuanzia sasa waanze kuwachukulia hatua kali watumishi wote wababe na wanaofanya kazi kinyume cha maadili.

Jambo lingine lililotuvutia katika ziara hiyo ni agizo la kuwataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini, kujenga hospitali za wilaya ili kupunguza haraka msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za rufaa.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya kutembelea Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru. Tunatarajia hospitali hiyo ya Mount Meru, itaboresha haraka huduma na wodi zake ikiwemo wodi za wazazi, kujenga sehemu ya kuoshea vyombo kwa wagonjwa na kuwachukulia hatua kali madaktari na wauguzi wanaolalamikiwa na wananchi.

Jambo lingine lenye manufaa katika ziara hiyo ya Waziri Mkuu ni taarifa yake kwa wananchi kuwa serikali imetenga jumla ya Sh trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini ili kuwezesha wananchi kutumia nishati hiyo.

Hakika ziara hiyo imeleta manufaa mengi.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link