Home » » Wasomi, wanasiasa wachambua 2017

Wasomi, wanasiasa wachambua 2017

Written By CCMdijitali on Friday, December 29, 2017 | December 29, 2017

Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk Charles Kitima

 Imeandikwa na Matern Kayera - Habari Leo

WASOMI na Wanasiasa maarufu nchini wamesema kuwa wanaridhishwa na hali ya kisiasa iliyopo nchini kwa kipindi chote cha mwaka 2017.

Kuridhishwa huko kumetokana na hali ya utulivu na utendaji makini wa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inajali watu wake. Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk Charles Kitima aliliambia gazeti hili jana kuwa wananchi wameridhika kutokana na utendaji wa serikali.

Alisema serikali iliyopo madarakani imejali kwa kiasi kikubwa maisha ya watu wake hasa katika suala la usalama. Dk Kitima alisema pamoja na changamoto za kiusalama zilizotokea kwenye baadhi ya maeneo nchini kama vile Kibiti mkoani Pwani, hali ya usalama nchini bado nzuri.

“Watu wanafuata sheria, lakini pia utendaji wa watumishi wa umma nao umebadilika na umekuwa mzuri, kwa kipindi hiki tumeona wananchi wakihudumiwa vizuri kwenye taasisi za umma,” alieleza Dk Kitima. Hoja hiyo ya kuwepo kwa mabadiliko chanya ya kisiasa nchini imeungwa mkono na Mbunge wa Mbinga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sixtus Mapunda.

Mapunda alisema kuwa hali ya kisiasa inazungumzwa katika maeneo matatu, yaani kiuchumi, kijamii na kisiasa. Alisema kwa kipindi cha mwaka 2017, hali ya kisiasa katika uchumi imekuwa nzuri na tulivu kutokana na kuwepo kwa uhakika wa chakula nchini. Alisema taifa lina chakula cha kutosha na kinapatikana kwa urahisi hali inayoleta utulivu. Kwa mujibu wa Mapunda, uwepo wa chakula cha kutosha unadhihirishwa na kuwepo kwa ziada ya chakula hasa mahindi katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Mbinga.

Mbali na utoshelevu wa chakula unaoleta utulivu, Mapunda amesema katika nyanja ya uchumi pia kumekuwa na ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na manunuzi ya ndege mpya.
Akitolea mfano kuanza kwa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na baadaye Kigoma, pamoja na ununuzi wa ndege mpya, Mapunda alisema mambo hayo ni muhimu siyo tu kiuchumi lakini pia katika kuleta utulivu wa kisiasa. Alisema kutokana na Serikali kununua ndege mpya, wananchi wengi wanamudu kusafiri kutokana na kushuka kwa bei.

Alisema haikuwa rahisi zamani kwa watu wengi kusafiri kwa ndege kutoka Dar es Salaam hadi Songea kwa kuwa nauli yake ilikuwa Sh milioni 1.2 tofauti na sasa ambapo nauli ni kati ya Sh 280,000 na 360,000. “Kisiasa, serikali imefanikiwa kuweka utulivu nchini; watu wanafuata utawala wa sheria na hakuna aliye juu ya sheria, watu wa chini ambao hawakuwa na sauti kwa muda mrefu, hivi sasa wanajisikia kuwa nchi hii ni ya kwao,”alieleza Mapunda.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema kisiasa, taifa limefanikiwa kulinda na kuheshimu tunu muhimu kama vile amani, umoja na Muungano na kuweka kando migawanyiko kwa misingi ya kikanda na migogoro kama vile ya wafugaji na wakulima. Kwa mujibu wa Dk Bana, kisiasa pia kumefanyika maamuzi magumu na mazuri kwa mambo muhimu ya kitaifa.

Aliyataja baadhi ya maamuzi hayo kuwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi pamoja na vigogo mbalimbali kufikishwa mahakamani. Mambo mengine ni msamaha wa kihistoria wa wafungwa uliofanywa na Rais Magufuli. Alisema kitendo cha Rais kutoa msamaha kwa wafungwa waliohukumiwa kunyongwa na wengine kifungo cha maisha, kimeleta upenda na furaha kwa wananchi.

Changamoto Pamoja na mafanikio hayo kisiasa na kiuchumi, bado zipo changamoto kadhaa zilizoelezwa kuhitaji kufanyiwa kazi likiwemo suala la katiba mpya, fursa za wanasiasa kufanya shughuli zao pamoja na ajira kwa vijana.

Akizungumzia baadhi ya changamoto hizo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu alisema kuwa hali ya kisiasa nchini kwa mwaka 2017 haikuwa nzuri kutokana na kukamatwa kwa baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa na kisha kuachiliwa bila maelezo.

Alisema ili kujenga demokrasia ya vyama vingi na yenye ushindani, inatakiwa suala la mchakato wa kupata katiba mpya uendelee hadi mwisho kwa kipindi cha mwaka 2018. Alisema mambo kama vile vita dhidi ya ufisadi na rushwa yatafanikiwa kama yatawekwa kwenye katiba.

Kwa upande wake, Dk Kitima alisema kuwa mahusiano ya vyama vya siasa kwa mwaka 2017 hayakuwa mazuri. Alisema ni vyema vyama vya siasa kujenga tabia ya kuwa na majadiliano kwa mambo muhimu ya kitaifa kama vile uchumi wa viwanda. Kuhusua tatizo la ajira kwa vijana, Dk Kitima alisema linasababishwa na ukosefu wa shughuli za kiuchumi ambazo zingewaunganisha na masoko ya nje.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link