Baadhi ya Wananchi waliohudhuria Uzinduzi wa Jengo Jipya la Baraza la Maji Chake chake Pemba katika shamra shamra za maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Seif akizungumza na Wananchi na Watumishi wa Baraza la Mji Chake Cheka wakati wa hafla ya kulizindua Jengo Jipya la Baraza hilo ikiwa ni shamra shamra za Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed.
Haiba ya Jengo Jipya la Baraza la Mji wa Chake Chake linavyoonekana katika maeneo ya kando ya Bara bara ya Mji wa Chake kuelekea Macho Mane.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua rasmi Jengo Jipya la Baraza la Maji Chake chake Pemba ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Press
Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitamuonea
haya kwa kumfukuza kazi mara moja
Mtumishi yeyote wa Serikali au Taasisi za Umma atakayegundulika anatoa
huduma kwa Umma katika misingi ya
Kibaguzi.
Akizindua rasmi Jengo Jipya la Ofisi ya Baraza la
Mji la Chake chake Pemba ikiwa miongoni mwa shamra shamra za sherehe za
Maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alisema Serikali Kuu inataka kuona mabadiliko makubwa katika maeneo ya
Utawala.
Balozi Seif alisema Serikali imefanya mageuzi
makubwa katika mfumo uitwayo Ugatuzi na kuhamisha majukumu yake katika Serikali
za Mitaa kwa lengo la kuimarisha utoaji bora wa huduma mbali mbali kwa
Wananchi.
Alisema uhamishaji huo wa majukumu umeanza rasmi
Mwaka huu unaoendelea wa Fedha ambapo huduma za msingi kama vile elimu ya
maandalizi na Msingi, afya ikiwemo huduma za msingi za Kilimo sasa ziotakuwa chini ya dhamana ya
Serikali za Mitaa za maeneo husika.
Alieleza kwamba Wananchi wanapaswa kutambua kuwa
kitendo hicho cha kuwapelekea huduma karibu yao na huduma hizo zikatolewa
katika mazingira mazuri mfano wa Jengo hilo zina lengo la kuimarisha Utawala wa Demokrasia hapa Nchini.
Balozi Seif alifahamisha kwamba wakati Serikali Kuu
itabakia na mambo ya jumla kama vile uandaaji wa sera, kanuni na usimamizi wa
jumla uimarishaji huo wa Serikali za Mitaa unatoa nafasi na fursa pana kwa
Wananchi wajiongoze na kujitawala wenyewe katika maamuzi ya mambo
yanayowakabili wenyewe.
Aliwakumbusha Wananchi kwamba Madiwani
waliowachagua wanawajibika kwao
Wananchi, na pale watakapoona huduma wanazopaswa kupewa haziendi vyema wana
haki ya kuwawajibisha, kuwahoji sambamba na kutaka maelezo yatakayowaridhiosha
huku wakielewa kwamba hiyo ndio maana ya kuimarisha Demokrasia.
Hata Balozi Seif aliwaomba Wananchi waelewe kuwa
kujitawala kuna gharama zake ambazo hazina budi kulipwa na Wananchi wenyewe
wanaojitawala huku wakielewa kwamba Baraza la Mji ni lao linalotoa huduma kwao
ambazo ni gharama zinazotokana na ada wanazotowa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea
kutofurahishwa kwake na taarifa za Machinjio ya Wesha yasiyotumika vizuri na
kuachwa bila ya matunzo jambo ambalo halikubaliki na wahusika wanapaswa
kulishughulikia mara moja.
Balozi Seif
alionya kwamba wakati atalifuatilia suala hilo lazima Wananchi na watumishi
wa Mabaraza la Miji wathamini mali
wanazopatiwa ambazo hugharimu fedha nyingi na kuwataka Wananchi wa Chake
wakatae kuona mali zao zinatumika ovyo na hatimae kuharibika mapema.
Akitoa Taarifa za ujenzi wa Jengo hilo la Baraza la
Mji wa Chake Chake Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Nd. Khamis Mussa
Omar alisema ujenzi huo ni sehemu ya
Mradi Mkuu wa Huduma za Jamii Zanzibar {
ZUSP }.
Ndugu Mussa alisema changamoto ya ujenzi huo
ilitokana na ubovu wa Nguzo za asili ambazo Mkandarasi wa Mradi huo alilazimika
kujenga upya nguzo hizo na kuongezeka kwa gharama za ujenzi huo zilizofikia
asilimia 36.4%.
Alisema mradi huo Mkuu wa huduma za Jamii hadi
kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Bilioni Moja ambapo
tayari kwa awamu ya kwanza zimeshajengwa
Ngazi Nane za Kuvukia Wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyengine katika maeneo
ya Mabondeni.
Katibu Mkuu Mussa aliishukuru Benki ya Dunia { World
Bank } kwa kuendelea kuipatia Mikopo ya
Fedha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kutekeleza miradi mbali mbali ya
Maendeleo.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid
Salum Mohamed akimkaribisha Balozi
Seif kwenye Hafla hiyo alisema Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuweka Taa za Bara barani katika Miji yote
Mitatu ya Kisiwa cha Pemba.
Dr. Khalid alisema jumla ya Dola za Kimarekani 55
Milioni zitakazotolewa Mkopo na Benki ya
Dunia zitaelekezwa katika mradi huo muhimu kwa kustawisha Miji hizo sambamba na
kuweka haiba nzuri ya maeneo hayo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kustawisha maisha ya Wananchi wake kadri ya hali ya uchumi inavyozidi
kuongezeka mfano wa Mwaka 2016 uliopata mafanikio makubvwa kutokana na
kuongezeka kwa Pato la Taifa na kufikia hadi asilimia 6.8%.
Waziri Khalid alifahamisha kwamba nyongeza za
Mishahara zilizotolewa na Serikali zikaenda sambamba na upandishwaji wa
Pencheni kwa Wazee waliostaafu na wale waliofikia umri zaidi ya Miaka 70 ni
miongoni mwa mafanikio ya ongezeko hilo la Mapato ya Taifa.
Othman Khamkis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
9/1/2018.