Prisca Ulomi na Daudi Manongi, Kambikatoto
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi
amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA yenye urefu wa kilomita
265 ambao umefanyika kwenye eneo la Itigi, Manyoni mkoani Singida hadi eneo la
Kambikatoto, Mbeya. Ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu hiyo ni pamoja na ujenzi wa
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita 265, vituo vya kutolea huduma
za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na vituo vya kuongeza nguvu za mawasiliano.
Dkt. Yonazi amesema kuwa amefanya ziara hiyo ili kukagua ujenzi huo kwa lengo la
kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi huo ili kuona namna mkandarasi ametekeleza kazi
husika kwa kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni nane za kufanikisha ujenzi wa miundombinu
hiyo iliyojengwa eneo la Itigi, Manyoni hadi Kambikatoto
Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano, za uhakika na kwa gharama nafuu katika maeneo yote nchini nzima ili
kuhakikisha kuwa mawasiliano yanaendelea kutumika katika shughuli za kiuchumi na kijamii katika kuchochea maendeleo ya taifa letu
Naye Meneja Mradi wa ujenzi wa miundombinu hiyo, Rajab Mikumwo wa Kampuni ya
Raddy Fibre Solutions ambaye ni mkandarasi aliyejenga miundombinu hiyo amemweleza
Dkt. Yonazi kuwa, kampuni yao imetekeleza ujenzi wa miundombinu hiyo kwa mujibu wa
matakwa ya mkataba na tayari nyaya za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano zimelazwa
ardhini na katika baadhi ya maeneo nyaya hizo zimepitishwa juu ya nguzo kuendana na
jiografia ya eneo husika endapo kuna mto au mwamba ili kuhakikisha kuwa mawasiliano
yanapatikana kwa uhakika mwanzo hadi mwisho wa eneo husika
Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema kuwa tayari Serikali
imefikisha miundombinu hiyo kwenye maeneo ya mipaka ya nchi za jirani zinazopakana na
Tanzania na sasa hatua zinaendelea za kufikisha mawasiliano hayo mpakani mwa DRC Congo
na Tanzania ili nchi jirani ziendelee kutumia na kunufaika na miundombinu hiyo
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Mhandisi
Nikusubila Maiko
amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo utawezesha watoa huduma za
mawasiliano nchini kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa kuwa tayari watoa
huduma hao wamewasilisha mahitaji hayo Wizarani ambapo ujenzi wa miundombinu hiyo
utaongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi
walio kwenye maeneo hayo ambapo miundombinu hiyo imejengwa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi
akikagua kituo cha maunganisho ya Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa wakati wa
ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya mkongo huo kutoka Manyoni,
Singida mpaka Kambikatoto mkoani Mbeya.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi
akisoma kipimo kinachoonesha urefu na ubora wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa
akiwa kwenye kituo cha kutolea huduma za Mkongo cha Rungwa wakati ziara yake
ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya mkongo huo kutoka Manyoni, Singida mpaka
Kambikatoto mkoani Mbeya.
Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya TEHAMA kutoka Wizara ya Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Nikusubila Maiko akifafanua jambo
kwa Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonaz juu ya ubora wa Mkongo wa
Mawasiliano wa Taifa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu huyo ya kukagua ujenzi wa
miundombinu ya mkongo huo kutoka Mnyon, Singidai mpaka Kambikatoto, Mbeya