Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amepiga marufuku shughuli za uchimbaji wa madini katika hifadhi ya mapango ya Amboni mkoani Tanga.
Katika
ziara aliyoifanya mkoani Tanga Januari 17, 2022 Dkt. Jafo alisema
kitendo cha wachimbaji hao kufanya shughuli hizo kinachohusisha ulipuaji
wa baruti juu ya miamba ya mapango hayo kinahatarisha maisha ya watu
wanaotembelea mapango hayo.
Alibaini
kuwa watu wanaojihusisha na uchimbaji wa madini hayo yakiwemo kokoto
hawana cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) hivyo kutokuwa
na uhalali wa kufanya shughuli hizo katika eneo hilo la kihistoria.
Alisema
kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira kosa kisheria kwa mtu
kufanya shughuli zozote bila kujisajili na kupewa cheti kutoka Baraza la
Taifa na Hifadhi ya Mazingira (NEMC).
“Mmeniambia wanaingia wanafunzi takriban 500 wanakuja kujifunza kwa vitendo kuna wengine wanasoma historia wengine Jiolojia wanakuja kuangalia asili ya haya mapango, sasa kwa shughuli hizo zinafanyia juu ya mwamba hazipaswi kufanyika hilo haliwezekani,” alisema.