Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi |
MHE. NDEJEMBI KUONGOZA KIKAO CHA UTATUZI WA MIUNDOMBINU ILIYOHARIBIKA KWENYE MRADI WA NYUMBA ZA WATUMISHI MOROGORO
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Deogratius Ndejembi ameazimia kufanya kikao na Watumishi Housing,
TARURA, MORUWASA, TANESCO na wakazi wa Kata ya Mkundi mkoani Morogoro
wanaoishi kwenye nyumba za Mradi wa Watumishi Housing ili kutatua
changamoto ya miundombinu iliyoharibiwa na mvua kwenye nyumba hizo za
gharama nafuu zilizojengwa kwa ajili kuwapangisha na kuwauzia Watumishi
wa Umma na wanachama wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii.
Mhe.
Ndejembi amefanya uamuzi huo akiwa mkoani Morogoro baada ya kukagua
Mradi wa nyumba zilizojengwa na Watumishi Housing katika Kata ya Mkundi
mjini Morogoro na kukuta miundombinu ya eneo hilo imeharibika kutokana
na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
Naibu
Waziri Ndejembi amesema atafanya kikao hicho siku ya Jumamosi ya tarehe
19 Februari, 2022 ili kuwawezesha wakazi wengi wa eneo hilo ambao ni
Watumishi wa Umma kushiriki kikamilifu.
Akiwa
katika ukaguzi wa miundombinu ya eneo hilo, Mhe. Ndejembi amejionea
madhara ya mvua zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo na kusababisha
nyumba hizo kuingiliwa na maji ya mvua ambayo imebomoa ukuta na mfereji
wa kuzuia maji kuingia katika makazi hayo na hatimaye kuharibu nyumba
mbili pamoja na vitu vya ndani vya nyumba hizo.
Mara
baada ya kumaliza ukaguzi wa maeneo yaliyoathirika na mvua
zinazoendelea kunyesha, Mhe. Ndejembi alikagua pia sehemu ambapo
mkusanyiko wa maji unaanzia na kuona kuna umuhimu wa kuzishirikisha
taasisi nyingine na wananchi ili kuweza kulimaliza kabisa tatizo hilo.
Ili
kukabiliana na athari zilizojitokeza kabla ya kufanyika kwa kikao rasmi
cha utatuzi wa tatizo la uharibifu wa miundombinu ya eneo hilo, Mhe.
Ndejembi amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dkt. Fred
Msemwa kuhakikisha anachukua hatua za haraka za kuimarisha miundombinu
ya ndani ya makazi hayo ambayo imeharibika, ikiwa ni pamoja na kuendelea
kushirikiana na taasisi nyingine katika kutafuta suluhu ya kudumu kabla
ya kikao chake alichoelekeza kufanyika Februari 19, 2022.