Home » » WAZIRI UMMY ATAKA HOSPITALI YA MWALIMU NYERERE KUTOA HUDUMA ZA UBOBEZI

WAZIRI UMMY ATAKA HOSPITALI YA MWALIMU NYERERE KUTOA HUDUMA ZA UBOBEZI

Written By CCMdijitali on Monday, February 7, 2022 | February 07, 2022


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu

 
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema anataka Hospitali ya kumbukumbu ya Mwl. J.K. Nyerere kutoa huduma za ubobezi katika magonjwa ya mifupa na ajali maeneo ya kanda wa ziwa ili kupunguza rufaa na kero kwa wananchi kwenda Hospitali nyingine kutafuta huduma.


Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Hospitali hiyo na kujionea huduma za afya zinavyotolewa pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo.

"Tunataka watu wa Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na mikoa ya jirani wenye matatizo ya mifupa badala ya kwenda MOI waje wapate huduma hiyo hapa". Amesema Waziri Ummy.


Waziri Ummy ameongeza kuwa lengo la kuleta huduma hizo katika Hospitali ya Mwl. Nyerere ni kuinua mkoa wa Mara ili kumuenzi Baba wa taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.


Aidha, Waziri Ummy amesema ameshaelekeza Taasisi ya Mifupa ya MOI kuja katika Hospitali hiyo na kuweka tawi la taasisi hiyo na kuanza kutoa huduma za mifupa na ajali.


Ameongeza kuwa Serikali imetoa fedha nyingi ili kuboresha huduma za saratani katika Hospitali ya Bugando na mkakati uliopo ni kuifanya hospitali hiyo kujikita katika matibabu ya saratani huku Hospitali ya rufaa ya Chato itakua ni kituo cha kutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya Moyo ili kuipunguzia mzigo Taasisi ya Jakaya Kikwete.


Katika ziara hiyo Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Afya kupitia na kujiridhisha makadirio ya maombi ya fedha za kumalizia ujenzi wa Hospitali hiyo huku Waziri Ummy akimuahidi kupeleka makadirio hayo ndani ya mwezi mmoja baada ya kujiridhisha.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link