MASHINE ZA KUCHANGANYA CHUMVI NA MADINI JOTO
DODOMA-24/02/2022
Wizara
ya Afya imekabidhi mashine tano za kisasa za kuchanganya chumvi na madini joto
kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI zilizotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania
kupitia shirika la Kimataifa la Nutrition Intenational kwa ajili ya kusimikwa
katika Mikoa ya Tanga, Pwani na Mtwara ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa
chumvi yenye kiwango cha kutosha cha
madini joto nchini.
Akizungumza
wakati wa kukabidhi mashine hizo kwa katibu mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, katibu
mkuu wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Utafiti uliofanyika nchini mwaka
2019 ulibaini Tanzania inazalisha chumvi Tani 330,712 kwa mwaka na kati ya Chumvi
hiyo Tani 141, 22 ambapo ni sawa na asilimia 43 haiwekwi madini joto hivyo ujio
wa mashine hizo utasaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye madini hayo.
Prof
Makubi amesema mashine hizo ambazo zimetengenezwa nchini na wataalamu kutoka
VETA zimeweza kugharimu kiasi cha shilingi milioni 55 huku gharama ya mashine
moja ikigharamu kiasi cha shilingi milioni 11 na kusaidia kuokoa milioni 14 kwa
kila mashine endapo zingeagizwa kutoka nje ya nchi.
“Mwaka 2018 shirika la Nutrition International ilifadhili ununuzi wa mashine tatu zilizoagizwa kutoka Afrika Kusini kwa jumla ya Shilingi milioni 75 ambapo mashine moja iligharimu shilingi Milioni 25 na kusimikwa Halmashauri za Kilwa, Hanang na Meatu na zinaendelea kufanya kazi na safari hii mashine hizo zimeweza kutengenezwa na Watalaam wetu kutoka VETA kusaidia kuokoa shilingi milioni 14 kwa kila mashine” alisema Prof Makubi.
Awali
akitoa maelezo juu ya programu ya kuzuia upungufu wa madini joto nchini
Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna
amesema Madini joto ni moja ya kirutubisho muhimu kwa ukuaji mzuri wa akili na
mwili wa binadamu na endapo mtu atakuwa na upungufu wa madini joto basi anaweza
kupata madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na udumavu wa akili na mwili.
Dkt.
Germana amesema katika kukabiliana tatizo la upungufu wa madini joto Taasisi ya
Chakula na Lishe inatekeleza programu ya kuzuia upungufu wa madini joto nchini
kwa kutumia mkakati endelevu wa kuongeza madini joto kwenye chumvi (Universal
Salt Iodation) kuanzia miaka ya tisini na mkakati huo unalenga kuhakikisha kuwa
angalau asilimia tisini (90%) ya kaya zote nchini zinatumia chumvi yenye madini
joto ya kutosha kama inavyopendekezwa na shirika la afya duniani (WHO).
“Serikali kwa kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe kwa kushirikiana na wadau wengine tumefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu na mafunzo kwa wazalishaji chumvi kuhusu uzalishaji bora na uchanganyaji wa chumvi na madini joto, kuhakikisha upatikanaji wa madini joto, kutoa vifaa vya kupimia uwepo wa madini joto kwenye chumvi (Test Kits) na vile vya kuangalia kiwango cha madini joto yaliyomo kwenye chumvi (WYD mashines).”alisema Dkt Germana
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Nutrition International Dkt. Daniel
Nyagawa amesema katika Mpango mkakati wake wa miaka 6 ulioanza mwaka 2018 hadi
2024 shirika hilo limejielekeza kufanya kazi zake kwa karibu na Serikali na
Taasisi zake ili kwa pamoja kuweza
kupambana na utapiamlo na madhara yatokanayo na utapiamlo.
Dkt.
Nyagawa amesema kwa sasa wanafarijika kuona sasa Mashine hizi zitaweza
kupatikana nchini tena chini ya Taasisi ya Serikali hivyo zoezi la ugawaji wa
mashine hizi utakuwa endelevu wakati wowote zikihitajika na kuna uwezekano Tanzania ikavuka asilimia
61 ya kaya zinazotumia chumvi yenye madini joto toshelevu endapo zitatumika
kikamilifu.
Akizungumza
kwa niaba ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Katibu Mkuu Prof.
Riziki Shemdoe ameipongeza VETA kwa kuanza kutengeza mashine hizo kwa gharama
nafuu tofauti na zingeagizwa toka nje ya nchi na amewaagiza makatibu tawala wa
mikoa itakayopewa mashine hizo kuhakikisha
wanazitumia ipasavyo na siyo kwenda na kuzifungia stoo.
Nae Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Caroly Nombo amesema
kutengenezwa kwa mashine hizo na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) imejidhihisha
kuwa sasa wahitimu na wanafunzi wa vyuo hivyo vilivyopo nchi nzima sasa
wameanza kutatua changamoto
zinazoikabili jamii na wanaweza kutengeneza vitu amavyo vitapatikana kwa gharama
nafuu na kuokoa gharama za fedha za serikali endapo bidhaa hizo zitaagizwa nje
ya nchi.
Tanzania ina zaidi ya wazalisha wadogo wa Chumvi 7000 wanaotumia teknolojia duni za kuzalisha chumvi na wametawanyika katika maeneo mbalimbali ambayo hayafikiki kwa urahisi hivyo ujio wa mashine hizi utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha nguvu kinachozalishwa nchini bila kuweka madini chumvi ya kutosha.
Jackson E. Monela
Public Relation Officer
Tanzania Food and Nutrition Centre
22 Barack Obama Avenue
P.O BOX 977
Dar es salaam
Tanzania
Mobile:
+255 758-340162
+255-739-340162
Tel. Phones +255 22
2118137
Fax. +255 22 2116713
Website: www.tfnc.go.tz