BUNGE LARIDHISHWA NA JITIHADA ZA SERIKALI ZA KUPELEKA MAWASILIANO KWA WANANCHI
- Shilingi Bilioni 5.4 Zatumika Kujenga Minara 40 Mwanza
- Zaidi ya Wananchi 6,000 wa Kata ya Nyampande, Sengerema Wapata Mawasiliano
- Wananchi 2,500 kati ya 6,000 wanatumia Data kupitia Mnara wa Nyampande
- Asilimia 99 ya Mnara Uliojengwa Nyampande Unatumiwa na Wananchi
- Kamati Yakagua na Kupongeza Utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi
Na Prisca Ulomi, WHMTH, Mwanza
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhishwa
na jitihada za Serikali za kupeleka mawasiliano kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso wakati wa ziara ya
Kamati yake mkoani humo ya kukagua miradi ya huduma za mawasiliano iliyotekelezwa na Wizara
ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa wananchi wa Mkoa huo leo tarehe 16 Machi,
2022 ambapo kamati hiyo imekagua ujenzi wa mnara wa mawasiliano wa Nyampande na
upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye eneo hilo; kufuatilia utekelezaji wa operesheni ya
anwani za makazi; na kukagua mitambo ya Mkongo wa Mawasiliano ya Taifa
Mhe. Kakoso amesema kuwa Kamati imeridhishwa na ujenzi wa minara 40 ya simu unaoendelea
mkoani humo na wanaishukuru Wizara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa
kupeleka mawasiliano kwa wananchi kwenye maeneo ambayo hayakuwa na mvuto wa kibiashara
na amewataka wananchi kutambua kuwa matokeo haya yanatokana na Wabunge wa maeneo
haya ambao ni wawakilishi wa wananchi kuhakikisha kuwa Serikali inajenga minara hiyo na faida
inayopatikana itumike kutengeneza uchumi na huduma za maendeleo ya jamii kama vile kujenga
madarasa, zahanati ili wananchi wanufaike.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameieleza
Kamati kuwa ujenzi wa mnara huo wa mawasiliano umefanyika kwa ubia kati ya Serikali na
kampuni ya simu ya Vodacom ambapo Serikali imewapatia fedha Vodacom kama chachu ili
waweze kujenga mnara huo na amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Robert
Gabriel kwa utekelezaji mzuri unaoendelea wa operesheni ya anwani za makazi na kuwa chachu
kwa wengine.
Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mshiba amesema kuwa ujenzi wa minara 18 imekamilika; ujenzi
wa minara 22 utakamilika mwezi Juni mwaka huu 2022 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.4
kitatumika kujenga minara hiyo katika mkoa wa Mwanza ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi
maeneo ya pembezoni wanapata huduma za mawasiliano.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Sitholizwe Mdlalose amesema
kuwa kampuni yake iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kujenga minara ili wananchi
wapate huduma za mawasiliano ya uhakika.
Mhe. Mhandisi Gabriel amesema kuwa utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi
unaendelea vizuri ambapo jumla ya nyumba 643,298 kati ya nyumba 551,554 zimewekewa namba
sawa na asilimia 118.5; jumla ya anwani 103,558 zimesajiliwa katika mfumo wa NAPA sawa na
asilimia 15.8; na nguzo zinazoonesha majina ya barabara 6,007 zimewekwa kati ya nguzo 65,384
sawa na asilimia 9.1 ambapo elimu inaendelea kutolewa kwa wadau ili waweze kushiriki kikamilifu
utekelezaji wa mfumo huu na ukamilishwe ifikapo mwezi Mei, 2022.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari