Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Samwel Mhina (31) mkazi wa Temeke pamoja na wenzake 13 kwa tuhuma za kusambaza video katika mitandao ya kijamii kinyume na sheria.
Mhina ambaye ni mwandishi wa habari na mkurugenzi wa mtandao wa kijamii wa U-Turn Collection na wenzake wanatuhumiwa kusambaza video hiyo ikimuonesha mgonjwa akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Kamanda Muliro
Jumanne amesema kwamba "baada ya kusambazwa, Hospitali ya Taifa
Muhimbili na wafanyakazi wake walikuwa katika taharuki kubwa."
Muliro amesema baada ya video hiyo kusambaa na baadhi ya wafanyakazi wa Muhimbili kuhusishwa ililazimisha uchunguzi uanze mara moja ambapo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zilifanya uchunguzi huo. Baada ya watuhumiwa hao kukamatwa na kupekuliwa walikutwa na vifaa mbalimbali vya kielektroniki zikiwemo kamera, kalama za kiuchunguzi (spying pens), miwani ya kichunguzi, kofia zenye kamera, laptop, memory cards.