Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amezitaka Taasisi zinazohusika na kutoa huduma kuhakikisha wanashirikiana na Majukwaa ya Watumiaji katika kutoa ufafanuzi wa masuala mbali mbali ili kumlinda Mtumiaji.
Mhe. Hemed ametoa wito huo katika kilele cha Maandimisho ya Wiki ya Mtumiaji kilichofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil kikwajuni jijini Zanzibar.
Amesema ni vyema kwa Taasisi hizo kuzifanyia kazi kwa vitendo sheria na Kanuni zilizopo ili kuweza kumsaidia Mtumiaji kupata huduma bora bila ya kikwazo chochote kile.
Ameeleza kuwa wapo baadhi ya watumishi hawawajibiki ipasavyo na kusababisha wananchi kuumia kutokana na uzembe wa watumishi hao hivyo amewataka viongozi kusimamia Sheria ili kufikia lengo la Serikali ya Awamu ya Nane kuweza kurahisisha huduma kwa wananchi wake.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amezitaka Mamlaka husika kuangalia njia bora za kiuendeshaji kwa lengo la kuwalinda watumiaji wa huduma mbali mbali.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amezitaka Taasisi hizo kuandaa malengo madhubuti ya kila mwaka kuweza kuwafikia wananchi kujua haki na wajibu wao .
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amezitaka Taasisi husika zinazosimamia uingizwaji wa bidhaa Nchini kusimamia kutoingizwa nchini Bidhaa zisizokidhi vigezo ili kuwapunguzia wafanyabiashara wadogo wadogo kuingia katika hasara zinazoweza kuepukika.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Nishati na Madini Mhe. Shaibu Hassan Kaduwara ameeleza kuwa katika kujali na kuzingatia hali za wananchi wizara imeweza kushusha bei ya Watumiaji wa umeme kwa Asilimia Hamsini ili kurahisisha huduma kwa wananchi wa Zanzibar.
Mhe. Kaduwara ameeleza kuwa baraza la kuwawakilisha watumiaji wa huduma za maji na nishati zanzibar (CRC) wanaendelea kutoa Elimu kupitia njia mbali mbali kwa wananchi ili Watumiaji kujua haki na wajibu wao katika matumizi.
Nae Mwenyekiti wa Jukwaa la Watumiaji Tanzania Bwana Leo Ngowi ameeleza kuwa Jukwaa hilo humlinda Mtoaji na Mpokeaji katika kupata huduma kwa kuweka sera na sheria madhubuti ya kulinda haki hizo.
Ameeleza kuwa TCF ndani ya Miaka mitatu ijayo imepanga kufanya tafiti ya Sera na Sheria pamoja na kuzifanyia mapitio Sheria zilizopo kwa Maslahi ya Mtumiaji.
Siku ya Mtumiaji Duniani huadhimishwa kila ifika Machi 15 ya kila mwaka ambapo kauli Mbiu kwa mwaka huu inasema USAWA KATIKA HUDUMA ZA FEDHA ZA KIDGITALI.
……………………
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya makamu wa pili wa rais wa Zanzibar
15/03/2022